NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
KUTOKANA na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na magonjwa ya moyo, wajawazito sasa watapimwa kuangalia mtoto aliye tumboni kama ameathirika na magonjwa hayo.
Uchunguzi wa magonjwa hayo ambao utaendeshwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), utahusisha ujawazito wa kuanzia wiki 18 na kuendelea.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa JKCI, Maulid Kikondo alisema uchunguzi huo utafanyika bure hospitalini hapo kwa siku tatu kuanzia Oktoba 12 hadi 14, mwaka huu.
“Tumegundua watoto wengi wanazaliwa na magonjwa ya moyo lakini upo utaalamu ambao wenzetu wamekuwa wakiutumia wa kupima ujauzito ukiwa na wiki 18 na kuendelea huweza kubaini mapema iwapo mtoto aliyeko tumboni ana matatizo au la.
“Mwenzetu Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Naiz Majani alikwenda nje ya nchi na akapata mafunzo, amerudi hivyo tutaanza kuwachunguza wajawazito,” alisema.
Alisema uchunguzi huo utafanywa kwa kutumia kifaa maalumu kiitwacho Fetal Echo-cardiology .
Kikondo alisema hawajaweka idadi maalumu ya wajawazito wanaotarajia kuwapima kwa kutumia kifaa hicho na amewataka wafike kwa muda uliopangwa.
“Kila atakayekuja atahudumiwa, mtoto anapogundulika kuwa na tatizo ni rahisi kutibiwa punde tu anapozaliwa na kuwa na afya njema akafurahia maisha kuliko akizaliwa na baadaye kugundulika kwa vile matibabu yake yanachukua muda ikizingatiwa wengi huletwa wakiwa wamechelewa,” alisema.
Kikondo alisema pamoja na hilo, Oktoba 9 hadi 16, mwaka huu wataendesha kambi nyingine ya upasuaji kwa watoto 30 wenye magonjwa hayo.
“Madaktari wa JKCI watafanya upasuaji huo kwa kushirikiana na madaktari wenzao kutoka Addis Ababa wa hospitali ya Al muntada,” alisema.