NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM
WATOTO 800 ambao asilimia 30 huugua saratani , kati ya watoto 2,500 wanaofikishwa katika vituo vya afya kupima ugonjwa huo.
Kutokana na hali hiyo, wazazi wameshauriwa kuwafikisha watoto wao katika vituo vya afya kupima ugonjwa huo kwa vile kundi hilo limeelezwa kusahaulika na badala yake wengi wao hufikishwa wakiwa na hali mbaya.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Asasi isiyo ya Serikali ya Marafiki wa Watoto wenye Saratani Tanzania, Janeth Manoni, alikuwa akizungumzia uhamasishaji na utoaji elimu juu ya saratani kwa watoto jana.
Uhamasishaji huo utahusisha kupima afya hasa ya magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na utafanyika Februari 18 mwaka huu katika viwanja vya Don Bosco, Dar es Salaam.
Alisema elimu juu ya ugonjwa huo kwa watoto inatakiwa kutolewa nchini kote si tu kwa wazazi lakini pia hata watoa huduma kwa sababu bado hawana uelewa.
“Utakuta mzazi anapoleta mtoto mwenye saratani anasema amekuwa akimpeleka hospitali na kueleza dalili ambazo mtoto anapata na huishia kupata dawa zisizo sahihi na matokeo yake ugonjwa kuenea zaidi,” alisema.
Alisema asasi hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Dini la Mtakatifu Don Bosco na wadau mbalimbali wakiwamo madaktari, imeandaa mkutano huo ambako pia itakuwapo michezo kwa watoto hao.
Naye Mhamasishaji wa Asasi hiyo, Renidius Rwezaula alisema madaktari 30 watakuwapo kutoa huduma ya upimaji afya kwa watoto na kutoa elimu bure.
“Wakati umefika kwa Watanzania kuanza kupima afya bila kusahau watoto wetu mara kwa mara kwa kuwa ugonjwa wa saratani unapoanza hauna maumivu jambo ambalo husababisha wagonjwa wengi kuletwa hospitali wakiwa wameathirika kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Rwezaula alisema mgeni rasmi katika kongamano hilo atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi.
Vilevile watakuwapo viongozi wa dini ambao pia watasaidia kutoa ushauri wa roho kwa wagonjwa.