27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

WaterAid yakabidhi vituo 12 vya kunawia mikono Dar

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

KATIKA kuadhimisha Siku ya Kunawa Mikono Duniani, shirika lisilo la kiserikali la WaterAid Tanzania, limekabidhi vituo 12 vya kunawia mikono kwenye maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.

Shirika hilo lenye makao makuu nchini Uingereza, limetoa vituo hivyo kwa kushirikiana na The Foreign, Commonwealth &Development Office(FCDO) na Uniliver ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali kusaidia Watanzania kunawa mikono kupambana na magonjwa ya kuambukiza ikiwamo Uviko-19.

Hafla ya kuzindua vituo hivyo ilifanyika leo Oktoba 15,2021 ambayo ni siku ya maadhimisho ya kunawa mikono duniani katika Hospitali ya Mwananyamala, huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni ‘Maisha Yetu Yako Mikononi Mwetu, Tutembee Pamoja’.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkaazi wa WatarAid Tanzania, Anna Mzinga, ametaja maeneo ambayo wameweka vituo hivyo vya kunawia mikono kuwa ni ofisi ya mkuu wa mkoa Dar es Salaam, Hospitali ya Mwanyamala, Hospitali ya Manzani Mmoja, Hospitali ya Temeke,Kituo cha Magufuli, Shule za msingo Malamba Mawili, Msasani na kituo cha daladala cha Mawasiliano.

Mkurugenzi Mkaazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga akizungumza katika hafla hiyo.

Anna ametoa wito kwa Serikali, kutoa kipaombele katika miundombinu ya usafi wa mikono kwenye vituo vya huduma za afya, shuleni na maeneo ya umma pamoja na uwepo wa miradi ya usafi.

“Pasipo na huduma sahihi za maji, usafi wa mazingira na vifaa vya kunawia mikono katika makazi, shule, vituo vya kutolea huduma za afya na taasisi nyingine basi mazingira yetu yatakuwa ni vyanzo vya magonjwa na kuacha jamii katika hatari ya kupata milipuko ya magonjwa ya kuambukiza na kuiningia gharama kubwa ya matibabu na kupoteza nguvu ya uzalishaji.

“Ukiondoa afua nyingine, wote ni mashahidi namna unawaji mikono umeongezeka nchini kwa kila sehemu ya biashara, taasisi na makazi kwa kuweka vifaa vya kunawia, maji na sabuni. Utaona Taifa tulivyopambana na Uviko 19 kupitia unawaji mikono,” amefafanua Anna.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Rashid Mfaume akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani kwenye viwanjan vya hospitali ya Mwananyamala leo

Aidha ameyaomba mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kuongeza uwekezaji katika usafi wa mikono kama jambo muhimu linaloendelea la utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa hafla hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akimwakilisha mkuu wa mkoa huo, Dk. Rashid Mfaume ameipongeza WaterAid na waandaaji wengine, huku akisisitiza kuwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.

Mfaume amesema maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na kijikinga dhidi Uviko 19 na kuanzia sasa huduma huduma sahihi za afya lazima kuzingatia upatikanaji wa maji.

Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Mfaume akimkabidhi cheti mmoja wa maofisa afya wa mkoa huyo

“Natoa wito kila Kaya iwe na vifaa vya kunawia mikono, pia sehemu za mikusanyiko. Wananchi wanatakiwa kutumia siku hii kuelimisha wengine,” amesema Mfaume kwa niama ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makalla.

Wadau waliohudhuria hafla hiyo

Dk. Mfaume ameeleza kuwa kunawa mikono kwa usahihi kunaepusha vifo vinavyotokana na magonjwa ya milipuko kwa asilimia 35 huku pia ukipunguza vifo vitokanavyo na maambukizi ya magonjwa ya mfumo wa hewa.

Naye Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo,amesema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2019-2021 unawaji mikono imeendelea kupewa kipaombele kwa jamii ya Watanzania ikiwamo mkoa huo.

Aidha Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dr Zavery Benela, ameishukuru WaterAid na kusema kituo cha kunawia mikono walichopata kitaongeza idadi ya sehemu walizonazo kwani kwa siku wanapokea watu zaidi ya 2000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles