Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka watendaji wa Wizara hiyo kutatua matatizo ya Watanzania bila kujali ni maskini au tajiri kwa kuwaweka tabaka moja wakati wa kuwahudumia.
Pia amewataka kusimamia zoezi la urasimishaji wa ardhi, ukusanyaji wa kodi, nidhamu mahala pa kazi pamoja na upangaji na umilikishaji wa ardhi.
Maagizo hayo ameyatoa leo Jumanne Mei 25 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, ambapo amewataka watendaji hao kujitahidi katika mikoa yao kuhakikisha wanatatua matatizo ya wananchi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Makamishna wa ardhi, Wasajili wasaidizi wa Mabaraza ya Nyumba, Wawakilishi wa Wafanyakazi kutoka mikoa 26 ya Tanzania , wakuu wa Idara na wawakilishi wa vitengo.
Waziri Lukuvi amesema watendaji hao wanatakiwa kutoa haki kwa kila mmoja bila kuangalia kama ni maskini ama tajiri kwa kuwaweka katika tabaka moja.
“Umilikishaji ni haki ya kila mtu,kila raia atazamwe kwa usawa, maskini, tajiri wote wawe katika tabaka moja,”amesema Lukuvi.
Aidha,Waziri Lukuvi amesema zoezi la urasimishaji kwa sasa katika maeneo mengi linafanywa na Makapuni binafsi wakati kazi hiyo ni ya kwao hivyo wananchi wengi wamekuwa wakitapeliwa jambo ambalo sio zuri.
“Hatuwazuii lakini haya mambo lazima yawekewe utaratibu, lazima yasimamiwe hata Chuo changu cha SUA kinalalamikiwa ni matapeli wamechukua hela kila mahali hata kule Dar es Salaam wachukuliwe hatua hata kama wapo serikalini bila kumwangalia mtu usoni tunataka urasimishaji usiokuwa na urasimu,”amesema Lukuvi.
Pia, amewataka kusimamia zoezi la upangaji na umilishaji ambapo amedai hategemei kuona kuna mtumishi katika wizara hiyo anasababisha migogoro.
“Ukusanyaji kodi nalo hili nawaombeni mlisimamie wengine wanakusanya asilimia 100 wengine chini ya hiyo lazima tuisaidie serikali katika ukusanyaji wa mapato. Simamieni nidhamu pahala pa kazi ili mambo yaende vizuri,”amesema.
Vilevile, Lukuvi amewataka Makamishna wa ardhi kuwa karibu na wakurugenzi wa Halmashauri ikiwa ni pamoja na kuwa wabunifu katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Waziri Lukuvi amesema katika ajira 38 zilizopatikana hivi karibuni kipaumbele kitakuwa ni kwa wapima ambapo amedai angalau kila Wilaya inatakiwa kuwa na mpima.