24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watendaji wasiosoma taarifa za mapato Kaliua waonywa

 Allan Vicent, Tabora

Watendaji wa vijiji na Kata katika Tarafa ya Igagala, Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora wasiowajibika ipasavyo kwa wananchi wao ikiwemo kutosoma taarifa za mapato na matumizi wameonywa na kutakiwa kubadilika. 

Onyo hilo limetolewa leo Juni 20, na  Ofisa Tarafa wa  Simon Malando alipokuwa akitoa semina elekezi kwa watumishi hao ikiwa ni kikao chake cha kwanza tangu aajiriwe kushika nafasi hiyo.

Amesema watendaji ni watumishi wa serikali ambao wamepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, hivyo wanapaswa kuhamasisha na kusimamia kikamilifu shughuli zote za maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.

Amesisitiza serikali ya Rais Dk. John Magufuli ni ya hapa kazi tu, hivyo mtumishi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia maendeleo ya wananchi anapaswa kutekeleza wajibu wake ipasavyo sio kuleta ujanja ujanja kazini.

Malando amebainisha kuwa baadhi ya watendaji, kazi yao ni kukaa ofisini tu badala ya kutembelea wananchi ili kusikiliza kero zao ikiwemo kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kupitia halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesikitishwa  na tabia ya baadhi ya watendaji wa vijiji kutosoma taarifa ya maendeleo ya vijiji vyao inayoonesha mapato na matumizi ya fedha za miradi katika mikutano ya hadhara.

“Natoa muda wa mwezi mmoja tu kila Mtendaji awe ameandaa na kusoma taarifa yake ya mapato na matumizi kwa wananchi, atakayeshindwa kutekeleza agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria,” amesema.

Malando amewataka Watendaji wa kata zote kusimamia utekelezaji wa agizo hilo katika maeneo yao na kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu, aidha aliagiza kila mmoja kutoa taarifa ya utekelezaji agizo hilo baada ya muda huo kuisha.

Aidha aliwakumbusha kuwa katika kikao kazi kilichofanyika Ikulu jijini Dar es salaam hivi karibuni serikali ilisisitiza sana kila mtendaji kutekeleza wajibu wake ipasavyo, uadilifu, uaminifu, kutembelea wananchi, kutatua migogoro na kutekeleza maagizo yote ya kampeni za kitaifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles