27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Watendaji msikwamishe malengo ya mahakama

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM


2016-oposiciones-auxilio-judicial

MAHAKAMA ni mahali ambako kila mmoja anaamini anaweza kupata haki yake kwa wakati.

Kutokana na ukweli huo mtu ama taasisi anapofikwa na jambo hukimbilia mahakamani kwa ajili ya kutafuta haki akiamini ataipata tena kwa wakati.

Wajibu wa mahakama ni kupokea mashauri mbalimbali yakiwamo ya jinai, kuyasikiliza na mwisho kutoa hukumu pale inapoona inafaa kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa.

Kinachotokea katika hukumu kiwe kizuri kwa upande mmoja ama kibaya kwa upande mwingine hiyo ndio haki ambayo mahakama iliona sahihi kuitoa.

Lakini pamoja na kufanya hivyo inatoa nafasi kwa anayeona hakuridhika kukata rufaa kuipinga hukumu hiyo katika mahakama ya juu, akiwa na sababu anazoona zinaweza kuzingatiwa haki yake ikapatikana.

Baada ya hukumu ama uamuzi uliosababisha kesi ikamalizika, wahusika husubiri kupata nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi ili aweze kukata rufaa.

Mazingira hayo yanaleta shida na wakati mwingine hukwamisha jitihada za kukata rufaa pale ambapo nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi unapochelewa.

Mfano hivi karibuni kuna kesi ya kughushi iliripotiwa kwamba, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini anakata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, lakini anasubiri mwenendo wa kesi.

Kesi hiyo inamhusu Edwin Igenge na Stellah Walter ambao waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu kwa mashtaka ya kughushi nyaraka mbalimbali kikiwamo cheti cha ndoa na hati za viapo.

Igenge na Walter walikuwa wakishtakiwa mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa, kwa mashtaka 12 ya kughushi na kuwasilisha nyaraka hizo za kughushi kinyume cha sheria, makosa hayo waliyafanya wakiwa katika ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu kati ya mwaka 2007 na 2009.

Mahakama ilitoa uamuzi huo Aprili mwaka huu lakini hadi leo rufaa hiyo haijawasilishwa kwa ajili ya kusikilizwa kwa sababu wanasubiri mwenendo wa kesi.

Hesabu za kawaida tangu walipoachiwa hadi kufikia sasa ni zaidi ya miezi sita, nani anayechelewesha rufaa hiyo kati ya DPP na makahama?

Kucheleweshwa kwa rufaa hiyo kumefanya mfanyakazi aliyerudi kazini Stellah kuanza kudai madai yake, swali la kujiuliza anawezaje kulipwa wakati Serikali inapinga kuachiwa kwake huru? Na je, atakaa hivyo hadi lini wakati rufaa hiyo haijawasilishwa?

Kitendo cha Serikali kuamua kukata rufaa kinaonyesha wazi kwamba hawakuridhishwa na uamuzi huo, kama hivyo ndivyo juhudi zifanyike shauri hilo liendelee katika hatua ya rufaa ili haki si tu itendeke, bali ionekane inatendeka na kwa wakati.

Mahakama imejiwekea utaratibu mzuri wa utendaji kazi kwa haraka, hivyo kasi ya kutoa nakala za hukumu na mwenendo wa kesi imekuwa kubwa, itakuwa inatia shaka kuona bado kuna mahakama ambazo zinachelewesha kukamilisha kazi kwa haraka mara baada ya kesi kumalizika.

Jaji Mkuu, Mohammed Othman Chande, amekuwa akisisitiza kazi kufanyika kwa haraka, mahakimu kumaliza kesi haraka ili kupunguza mrundikano wa mafaili bila sababu za msingi.

Mikakati iliyowekwa na mahakama inapaswa kutekelezwa kwa vitendo, haipendezi na inakatisha tamaa kuona wengine wanatekeleza huku wengine wakikwamisha juhudi hizo.

Hiyo ni kesi moja ya mfano lakini zipo kesi ambazo wahusika wanapandisha ngazi na kushuka wakifuatilia nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi.

Wachapaji wa hukumu na mwenendo wa kesi wanatakiwa kwenda na kasi ya mahakama, bila kufanya hivyo malengo yaliyowekwa hayatafikiwa na malalamiko kutoka kwa wananchi yataendelea kuwepo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles