Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Jumla ya Sh Milioni 10,000,000 jana zilitolewa na Benki ya NMB kwa wateja 100 waliojishindia katika droo ya 8 ya Mastabata Kivyakovyako.
Jana ilikuwa wiki ya 8 ya shindano la MastaBata kivyakovyako linalochezeshwa na Benki ya NMB kwa wateja wanaotumia kadi za Mastercard kwa ajili kufanya miamala popote nchini.
Afisa Mahusiano wa Benki ya NMB tawi la Kambarage jijini Dodoma, Shukuru Mhagama ambako droo hiyo ilifanyika Shukuru Mhagama, alisema walianza Desemba 24,2021 na droo itahitimishwa Machi 23,2022.
Mhagama alisema wateja wanaotumia Master Card kwenye posi za malipo, QT na mitandao ya kielekroniki ndiyo ambao wanaingia kwenye droo hiyo.
Alisema kila wiki wanapata washindi 100 ambao kila mmoja anajishindia kitita cha Sh100,000, kuna washindi 25 wa mwezi ambapo kila mmoja anashinda Sh Milioni 1 na mwisho wa shindano kutakuwa na droo kubwa ya washindi 30 kuondoka na Sh Milioni 3.
Akizungumzia droo hiyo, Mwakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Ibrahim Sikana alisema hakujawahi kuwa na kelele wala malalamiko katika droo zote za NMB hivyo wanaamini kila jambo huendeshwa kwa utaratibu ndani ya benki hiyo.
“NMB hawajawahi kuwa na malalamiko, michezo mingi wanayochezesha imekuwa ikifuata sheria na kanuni na washindi wanapatikana kihalali, naomba watu waendelee kutumia kadi hizo ili wawe kwenye nafasi ya kushinda,” alisema Sikana.
Hata hivyo baadhi ya watu jana walikosa bahati zao baada ya simu zao kutopokelewa zilipopigwa au hazikupatikana na sheria inataka simu ipigiwe mara tatu, mshindi asipopatikana basi bahati humwendea mwingine.
Awali Meneja wa Tawi la Kambarage Emiliana Wilson aliwataka wateja kuendelea kuiamini Benki ya NMB na kuitumia kwani ni Benki pendwa inayotoa huduma zake katika maeneo mengi nchini.
Emiliana alisema tangu shindano hilo lilipoanza mwishoni mwa Desemba, watu wengi wameshajishindia fedha nyingi hivyo akasisitiza matumizi sahihi ya kadi za Master Card.
Meneja alisema katika wiki hiyo ya 8 ya droo, wamejiandaa kutoa fedha nyingi kwa wateja wao lakini akasisitiza matumizi sahihi ya kadi hizo.