24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watatu zaidi wachukua fomu za urais CCM

nyalanduNA DEBORA SANJA, DODOMA

MBIO za urais zinaendelea kupamba moto baada ya makada wa CCM wanaochukua fomu kuwania kuteuliwa kugombea nafasi hiyo kupitia chama hicho kufikia 18.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ndiye alikuwa wa 16 kuchukua fomu hizo jana akifuatiwa na makada wengine wa chama hicho, Peter Nyalali na Leonce Mulenda
Nyalandu alifika Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma, akiwa ameambatana na mkewe Faraja Nyalandu na watoto wao wawili.
Akijibu swali kuhusu jinsi gani atadumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iwapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itatawaliwa na upinzani, alisema ni zaidi ya vyama vya siasa.
“Muungano wetu ni muungano wa mioyo, unazidi tofauti zetu za kidini, unazidi ukabila wetu na unazidi tofauti zetu za vyama vya siasa.
“Bila kujali nani atashinda, nitahakikisha ninashirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha unadumu hadi nchi nyingine zije zijifunze maana ya Utanzania wetu,” alisema.
Nyalandu alisema iwapo atashinda nafasi hiyo ataiongoza nchi bila kulipa visasi kwa kuwa anaamini katika umoja wa kitaifa.
“Nataka kuona Watanzania wote tunafanya kazi kwa pamoja, naamini tukifanya hivyo tunaweza kuishangaza dunia,” alisema.
Alisema yeye anachukua fomu ya kuwania urais huku akizifahamu changamoto za Watanzania pamoja na kazi kubwa waliyoifanya marais waliotangulia akiwamo Rais Jakaya Kikwete.

NYALALI
Kwa upande wake, Nyalali akizungumza na wanahabari mara baada ya kuchukua fomu, alisema ameamua kugombea nafasi hiyo kwa kuwa ni haki yake kiraia.
Alisema anataka kukuza demokrasia pamoja na kuleta mabadiliko chanya katika nyanja mbalimbali.
Nyalali alisema alikuwa ofisa mwandamizi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hadi mwaka 2007 alipomuomba Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama atoke nje ya jeshi ili alitumikie taifa katika nafasi nyingine.
“Mwaka 2010 niligombea ubunge Temeke nikashika nafasi ya tatu, mwaka huohuo nikagombea uspika, lakini chama kikaona nipishe nafasi hiyo kwa kuwa ilikuwa zamu ya mwanamke kushika nafasi hiyo,” alisema.
Alipoulizwa sababu za kuamua kugombea nafasi ya juu zaidi, Nyalali alisema alipogombea ubunge alipata kujua mahitaji ya Watanzania.
Akijibu swali sababu za kutokutangaza nia ili Watanzania wamjue, alisema siasa ni sayansi na kwamba siyo wote wanaomchagua rais.
“Watanzania wengi wananifahamu, nina kundi kubwa na ninaomba vyombo vya habari vinitangaze,” alisema.
Tofauti na wenzeke, mgombea huyo alifika makao makuu ya CCM kuchukua fomu akiwa amekodi teksi.

MULENDA
Naye Mulenda ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya High Quality Consultancy Limited (HQCL), alisema iwapo atapata nafasi hiyo atahakikisha CCM inakuwa imara.
“CCM haitakuwa joka la mdimu, tutahakikisha Serikali inatekeleza ilani zake na watumishi wa umma wakati wote wataongozwa na sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa,” alisema.
Alisema kinyume cha hilo mtumishi huyo atakuwa anajichimbia kaburi.
Mulenda alisema Serikali yake kupitia ilani ya CCM itakuwa ni sikivu, makini na inayojali shida za watu huku akijinasibu kuendeleza elimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles