28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Kigwangalla aja na bima ya afya kwa kila mwananchi

khamisNA RUTH MNKENI, DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla, ametangaza rasmi nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akitaja vipaumbele vikuu vitatu ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya.
Kigwangalla ambaye alitangaza nia yake hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Nzega mkoani Tabora, alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kwani ana dhamira njema, hofu ya Mungu na anachukia rushwa.
Alisema Tanzania ya sasa inahitaji kuongozwa na vijana ambao wana fikra mpya ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi na sio watu ambao wameongoza kwa kipindi kirefu.
Alisema vipaumbele vyake ni kuondoa umaskini, kutoa huduma bora kwa jamii na kudumisha utawala bora.
Dk. Kigwangalla alisema akichaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano, atahakikisha nchi inakuwa na rasilimali za kutosha na kuondokana na utegemezi.
Alisema Serikali atakayoiongoza akipewa ridhaa, haitategemea hata Sh 1 kutoka kwa wahisani na kwamba atahakikisha kila mtu anakuwa na bima ya afya.
Dk. Kigwangalla alisema ili kuhakikisha uchumi unakua kwa kiwango kinachostahili, asilimia 5 ya bajeti itapelekwa kwa wanasayansi kwa ajili ya utafiti.
Alisema atahakikisha anaanzisha mfuko wa kukopesha wafanyabiashara wadogo ili kukuza uchumi wa nchi na taifa kwa ujumla kwani Tanzania ina uwezo wa kujenga matajiri wa ndani ya nchi.
Dk. Kigwangalla anayetumia kaulimbiu ya ‘Fikiri tofauti, amua mabadiliko sasa’, alisema Serikali ina uwezo wa kukusanya bilioni 20 kila mwaka kutokana na utawala bora.
“Natamani kuijenga Tanzania ambayo wabunge watapeleka watoto wao kusomea katika shule za kata na sio kama ilivyo sasa ambapo wanawapeleka kwenye shule za watu binafsi,” alisema.
Pia alisema Watanzania waishio vijijini wanahitaji kujengewa mazingira mazuri kwani wengi wao wanategemea sekta ya kilimo.
Alisema endapo atapata ridhaa hiyo atahakikisha anadhibiti urasimu na kuweka uwajibikaji ili kuwa na mfumo mzuri wa uongozi.
Mbali na hayo alisema Serikali yake itawajibika kutoa mikopo ya nyumba, kuchora ramani ya nyumba zilizo bora, kuwa na Mfuko wa Taifa wa Madini, kupunguza misamaha ya kodi na kuwa na makusanyo makubwa ya kodi ili kupata fedha za ziada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles