26.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Watatu Kortini Bukoba kwa uhujumu uchumi

Nyemo Malecela – Kagera

ALIYEKUWA Meneja wa Kiwanda cha Kahawa cha Tanica, Linus Leopord, Mhasibu Mkuu wa kiwanda hicho, Didas Burchard na wafanyabiashara wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba kwa makosa 15 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na matumizi mabaya ya ofisi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni tatu kwa kiwanda hicho.

Wafanyabiashara waliofikishwa mahakamani katika kesi hiyo namba 1/2020, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, Neema Gesabile, ni Athumani Saidi Kazinja aka Alhaji Othumani Saidi Kazinja na Abdul Salami Saidi Kazinja wakazi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Katika kesi hiyo, watuhumiwa wanatetewa na mawakili wawili, Mathias Rweyemamu na Projestus Mulokozi wakati mawakili wa Jamhuri ni Juma Mahona, Haruna Shomari na Naila Chamba.

Kabla ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani, Taasisi ya Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kagera (Takukuru) ilitaja baadhi ya tuhuma zinazowakabili watuhumiwa hao kuwa ni uhujumu uchumi chini ya aya ya nne ya 4(1) (c) ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1) na 60 (20) ya sheria ya uhujumu uchumi.

Matumizi mabaya ya ofisi chini ya kifungu cha 96(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu, kukisababishia hasara kiwanda ya zaidi ya Sh bilioni 3 chini ya aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(20) ya sheria ya uhujumu uchumi.

Pamoja na ukwepaji wa kodi na utakatishaji wa fedha haramu chini ya sheria ya utakatishaji wa fedha haramu sheria namba 12.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kagera, John Joseph alisema uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo umebaini katika kipindi cha Januari 2018 hadi Desemba 2019, Linus na Didas wakiwa ni sehemu ya viongozi wa kiwanda cha Tanica walikuwa wakipokea kahawa isiyokuwa na ubora kutoka kwa Athumani na Abdul ambao pia ni wafanyabiashara wa matofali.

Alisema wafanyabiashara hao walikuwa hawana vibali vya kufanya biashara ya kahawa kwa mujibu wa sheria ya kahawa namba 347 wakati Linus na Didas wakinunua kahawa isiyo na ubora kwa hila na makusudi na kusababisha hasara ya Sh bilioni tatu kinyume cha sheria, hivyo kusababisha kiwanda kupata hasara.

Kiwanda cha Tanica kilichopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kinamilikiwa na vyama vya ushirika vya KCU, KDCU na wafanyakazi.

Kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, watuhumiwa wamerudishwa rumande wakisubiri kesi hiyo itakapotajwa tena Februari 25.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles