25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Hatma ya Kabendera kuwa huru kujulikana Februari 17

Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imekubali mawakili wa Jamhuri kukaa na mwandishi wa habari za uchunguzi,  Erick Kabendera kwa majadiliano ya mwisho ili kumaliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega baada ya jopo la mawakili likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kuwasilisha maombi hayo.

Nchimbi alidai kwa muda mrefu walikuwa wakifanya majadiliano na mawakili wa mshtakiwa na sasa wako katika hatua za kuandaa mkataba.

“Mchakato huu wa majadiliano unamuhusu mshtakiwa mwenyewe, tunaomba kuzungumza na mshtakiwa mwenyewe, leo (jana) tutakaa naye ili kukamilisha sehemu ya mwisho ya majadiliano ya kukiri kosa, tunaomba shauri lije Jumatatu,” alidai Nchimbi.

Akijibu hoja ya maombi hayo, wakili wa utetezi, Jebra Kambole alidai hawana pingamizi la mawakili kuzungumza na mshtakiwa na pia shauri hilo kuahirishwa hadi Jumatatu.

Hakimu Mtega alikubali maombi ya Jamhuri ya kukaa na mshtakiwa wajadiliane na kufikia makubaliano ya kumaliza kesi, hivyo aliiahirisha hadi Februari 17 ambapo hatima ya mshtakiwa huyo itajulikana.

Kabendera anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwamo la utakatishaji wa zaidi ya Sh milioni 173.

Katika shtaka la kwanza ilidaiwa kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 Kabendera alijihusisha na mtandao wa kihalifu kwa kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Shtaka la pili ilidaiwa kuwa katika kipindi hicho, bila ya sababu, alikwepa kodi ya Sh 173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la tatu, Kabendera anadaiwa kutakatisha Sh 173,247047.02 huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kujihusisha na genge la uhalifu na utakatishaji fedha.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,522FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles