32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania wanatarajia mabadiliko Wizara ya Madini

KAMA kuna wizara ambayo inamuumiza kichwa Rais Dk. John Magufuli, basi ni Wizara ya Madini.

Mbali ya utendaji, ndiyo wizara ambayo ndani ya miaka mitatu imeweza kuongozwa na mawaziri watatu kwa nyakati tofauti.

Hii ni dalili ya wazi kwamba kuna baadhi ya mambo hayendi sawa sawa, hali inayomfanya Rais Magufuli kufanya mabadiliko mara kwa mara katika wizara hiyo.

Ndani ya miaka hiyo kumeendelea kuwapo na malalamiko mengi, lakini kubwa zaidi ni namna gani dhahabu ya Tanzania inaweza kunufaisha taifa, badala yakundi la watu wachache.

Kwa mfano kuondolewa kwa aliyekuwa waziri wake, Angella Kairuki kunaelezwa kwamba alishindwa kusimamia mambo kadhaa makubwa.

Sababu mojawapo ni hali ya Tanzania kushindwa kuongoza katika nchi za Afrika Mashariki licha ya kuchimba dhahabu nyingi.

Nyingine vituo vya madini kwa ajili ya kuratibu uuzaji, kutofahamu zinapouzwa dhababu zilizochimbwa nchini na kiasi ambacho taifa linaingiza kutokana na biashara hiyo.

Jambo jingine, ni kukosekana kwa kanuni zinazoelekeza kuhusu utaratibu wa uchimbaji wa dhahabu, ikiwamo rekodi ya dhahabu iliyopatikana na mauzo yake.

Kiuhalisia mambo haya manne ni mazito  na ambayo katika kipindi chote cha utawala wa awamu ya tano hayajafanyika.

Tunaamini kutokuwapo kwa mambo haya kunaweza kuwa chanzo kikubwa cha  dhahabu hii kupita njia za panya.

Profesa Sospeter Muhongo ndiye waziri wa kwanza  wa madini kabla haijatengeneshwa na nishati katika Serikali ya awamu ya tano.

Hata hivyo Rais alimwondoa  baada ya ripoti ya mchanga wa madini (makinikia) kuwasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchunguzi, Profesa Abdulakarim Mruma.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Rais Magufuli amekuwa mkali kila kukicha na kuwataka mawaziri na watendaji wake kwenda kuweka mifumo ambayo itasaidia taifa kupata faida ya mauzo ya dhahabu.

Kasoro hizi ndizo zilizomfanya Rais Magufuli kumpandisha Dotto Biteko kuwa waziri kamili kutokana na sifa nyingi alizomwagia tangu akiwa mbunge wa kawaida.

Tunaamini sasa Waziri Biteko amewekwa sehemu mbayo ataitendea haki kisawasawa kutokana na uwezo wake alionao juu ya eneo hili.

Tunasisitiza hili kwa sababu haitakuwa vizuri tena  kurudia makosa ya watangulizi wake ambao  kwa namna moja au nyingine walishindwa kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili hapo.

Lakini haya yote yatatimia tu, kama wasaidizi, watumishi na watendaji wote wa wizara hii watafanya kazi kwa kushrikiana  na kutanguliza uzalando wa taifa.

Inawezekana Biteko akawa mzuri kwenye kusimamia, lakini watendaji wakawa wabovu kusimamia maelekezo yake.

Kama tulivyosema hapo juu, Tume ya Madini nayo inapaswa kutoka kwenye usingizi wa pono, kwa sababu  kushindwa kwake kutimiza wajibu ipasavyo ndiyo dalili ya mawaziri kutumbuliwa kila wakati.

Katika hili, tunamshauri waziri mwenye dhamana kuingilia tume hii kwa jicho la karibu zaidi ili isimamie vyema majukumu yake yakiwamo ya kuanzisha vituo vya kukusanyia na kuuzia dhahabu hizi ili kumpunguzia manung’uniko makubwa aliyonayo Rais Magufuli.

Sisi MTANZANIA, tunasema watumishi wa Wizara ya Madini wakijipanga vizuri kutakuwapo na mabadiliko makubwa na tija itapatikana.

Nivema wakazingatia ushauri uliotolewa na Rais Magufuli katika kuhakikisha mageuzi makubwa yanafanyika wizarani hapo ili taifa liweze kunufaika na rasilimali hii ya madini.

Iwekwe mikakati kwa ajili ya kudhibiti maeneo yote nyeti ambayo yanayonekana yatapunguza mianya ya upotevu wa dhahabu na mapato yake.

Tunamalizia kwa kuwasihi zaidi watumishi wa wizara hii kwa ujumla wake, kuwa nao wanapaswa kubadilika ili watimize majukumu yao vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles