27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WATANZANIA WAFANYE KILIMO KIBIASHARA HAI

NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM


cherry-tomatoes

KILIMO ndio msingi wa maisha ya binadamu na kwa Mtanzania, tunaambiwa daima kwamba kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi, kikiwa kinachangia asilimia kubwa ya pato la taifa na pia kilimo ni mwajiri kwa takribani asilimia 70 ya Watanzania.

Wakulima nchini Tanzania wametakiwa kulima kilimo cha biashara kwa mfumo wa kilimo hai ambapo mbolea  na dawa za kunyunyizia zitumike za asili badala ya zile za kisasa ili kuondokana na lishe hatarishi kwa afya ya walaji na pia kujiongezea kipato.

Hayo yamesemwa na mmoja wa wakulima wa kilimo hai wa mboga mboga mjini Arusha, Simon Mutire ambapo aliliambia MTANZANIA kuwa miaka ya nyuma alikuwa akitumia mbolea za viwandani zaidi hali ambayo inasababisha walaji wanakula vyakula hasa mboga mboga zenye sumu   ambavyo ni hatarishi kwa afya zao.

“Ilipofika mwaka 2014, walikuja wataalamu wa kilimo hai kutoka Italia ambapo walitembelea mashamba yetu yaliyopo Meru na Arusha Mjini na baada ya kufanya utafiti walibaini kuwa mboga nyingi zinazolimwa na wakulima wa Arusha zinawekwa dawa nyingi ambazo husababisha magonjwa kama vile saratani, kisukari na mengineyo,” alisema.

Jumla ya wakulima 40 kutoka vikundi 10 wamenufaika na mafunzo ambayo wataalamu hao waliyatoa kwao ambapo walifundishwa jinsi ya kuhifadhi mazingira yanayozunguka mashamba na matumizi ya mbolea za asili na dawa za asili za kunyunyizia mazao.

Vile vile wakulima hao walifundishwa jinsi ya kulima mboga mboga kwenye eneo dogo lakini kwa njia ambayo mkulima atavuna kiasi kikubwa cha mazao.

Mutire alisema aina mbalimbali za  mboga mboga hulimwa na wakulima hao  zikiwemo nyanya ndogo ndogo zijulikanazo kama cherry, kabeji, nyanya mshumaa, pilipili hoho na  matango.

“Mwitikio wa wateja waliokuja kununua mboga mboga zetu ulikuwa mzuri sana na tumekuwa tukitoa elimu katika jamii zinazotuzunguka na wateja wanaokuja kununua mboga juu ya umuhimu wa kula mboga na matunda yaliyolimwa kwa kutumia kilimo hai kwa manufaa ya kulinda afya zetu na vizazi vyetu pia,” alisema Mutire.

Aidha, mradi mwingine ujulikanao kama Holly Family Greenery ambao uko chini ya Kanisa Katoliki eneo la Njiro jijini Arusha, umeanzishwa na hutumia kilimo hai.

Msimamzi wa mradi huo, Enock Nanyaro, alisema awali kilimo hai cha biashara ya mboga mboga na matunda kilikuwa kinalipa sana lakini idadi ya wanunuzi imepungua hivi karibuni kutokana na hali mbaya ya mzunguko wa fedha ambao umesababisha wateja kupungua.

“Awali tulikuwa tunauza kiasi cha wastani wa kilogramu 70 kwa wiki, lakini mauzo yamepungua sana kwani kwa sasa tunauza wastani wa kilo 20 kwa wiki,” alisema.

Akaongeza kuwa wanunuzi wakubwa ni wananchi wa kawaida, maduka makubwa (supermarkets) na raia wa kigeni ambao hupendelea zaidi nyanya ndogo ndogo (cherries) au wengine huziita tunguja ambazo zina virutubisho kwa wingi kwa mwili wa binadamu.

Alisema kilo moja ya nyanya hizo aina ya ‘cherries’ iliuzwa kwa shilingi 6,000 lakini kutokana na hali ya kifedha miongoni mwa walaji kuwa ngumu bei imepunguzwa ambapo kwa sasa huuzwa kwa shilingi 5,000.

Kwa upande wa wateja wa kwenye maduka makubwa (supermarkets) kilo moja ya cherries ilikuwa ikiuzwa kwa kiasi cha shilingi 12,000 lakini kwa sasa bei imeshuka ambapo kilo moja inauzwa kwa shilingi kati ya 7,000 hadi 8,000 kulingana na maeneo.

Kwa upande wa upatikanaji wa mbegu za nyanya hizo, Nanyaro alisema zinapatikana katika maduka mbalimbali ambazo huletwa kutoka Holland na mbegu moja inauzwa shilingi 300.

“Mbegu moja ya nyanya hizo inauzwa kwa shilingi 300, lakini ikishaanza kuvunwa ina uwezo wa kuendelea kuzalisha kwa mwaka mzima,” alifafanua.

Aidha, kwa upande wa usalama wa mboga mboga hizo hasa mbegu za nyanya kwa afya ya mlaji, Nanyaro alisisitiza kuwa mbegu hizo ni salama na zimeshafanyiwa utafiti kabla ya kuanza kutumika nchini na zimeonekana kuwa zina ubora wa hali ya juu.

Aliongeza kuwa nyanya au mboga mboga zilizolimwa kwa njia ya kilimo hai zina uwezo wa kukaa siku saba bila kuharibika tofauti na zile zilizolimwa kwa njia ya dawa za kuulia wadudu za viwandani na mbolea ambazo huanza kuharibika baada ya siku tatu tu.

Hivyo basi wakati umefika kwa wakulima Watanzania hasa wa mboga mboga na matunda kuona umuhimu wa kutumia kilimo hai ili kupata mazao yenye ubora na rafiki kwa afya za walaji na pia kujiongezea kipato kwani soko kubwa la nje ya nchi hununua zaidi mazao ambayo hayana aina yoyote ya sumu zitokanazo na mbolea za viwandani na dawa za kunyunyizia.

Katika sehemu kubwa ya nchi yetu, ardhi imekuwa chanzo cha migogoro ya mara kwa mara kutokana na matumizi yake, ambapo jamii za wakulima na wafugaji zimekuwa zikigombana na hata wakati mwingine kusababisha maafa na kila moja ikisema inastahili kutumia ardhi hii.

Hii ni kwa sababu mkulima, baada ya kuona ardhi yake imechoka huamua kutafuta maeneo mengine yaliyo bora na kuanza kuyatumia. Wakati mwingine hulazimika kufyeka misitu ili kupata mashamba mapya, hali ambayo si tu inaharibu mazingira, lakini pia inaweza kuleta umasikini wa milele kwa kuwa  ardhi iliyoachwa awali huwa haitafutiwi njia mwafaka ya kuifanya irejee kwenye ubora wake.

Katika baadhi ya maeneo, wakulima wengine hutafuta mbolea, hasa za chumvi chumvi na kuzitumia katika ardhi ile inayoonekana kuzeeka. Lakini matatizo mengi huibuka kutokana na matumizi ya mbolea pamoja na dawa za kemikali kwenye kilimo. Hii ni kwa sababu mbolea hizi zina kemikali na zile dawa za kuua wadudu zina madhara yake kwani zina sumu isiyoonekana. Sumu hiyo ikiliwa huleta madhara kwa binadamu na udongo.

Aidha, mazao yatokanayo na kilimo cha mbolea hizi za kemikali yanaleta athari kubwa zisizoonekana kwa binadamu na hata wanyama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles