Na Upendo Mosha,Hai
Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, amewataka wananchi kuishi maisha mema ambayo yataacha alama na funzo duniani pindi watakapoondoka.
Prof. Mkenda ameyasema hayo leo Jumanne Juni 15, 2021 wakati wa mazishi ya Vicky Nsilo Swai, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kwanza Mwanamke wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, aluyefariki dunia Mei 31, 2021 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akitoa salamu za Serikali kwenye maziko ya Vicky, yaliyofanyika Kijiji cha Nkuu Sinde Machame, Prof. Mkenda amesema marehemu Vicky pamoja na kushika nyadhifa mbalimbali, ndani ya serikali na CCM na kwamba aliishi maisha mema ambayo yameacha funzo na alama duniani.
“Kuondokewa na kiongozi wetu huyu, Vicky ni pigo kubwa kwetu, hasa tukimkumbuka namna alivyojitoa enzi za uhai wake,wengi wanamkumbuka kama Mwenyekiti wa CCM Kilimanjaro ambaye alisimama kukijenga chama, lakini ni vizuri tukakimbuka familia hii ni familia ya wapigania uhuru.Â
“Walisimama kupigania ukombozi wa Afrika, na mtakumbuka familia hii ndiyo ilimkaribisha Nelison Mandela alipokuja nchini, hivyo pamoja na majonzi tuliyo nayo, tuadhimishe maisha yake, kwa kujivunia, historia iliyotukuka ya kulitumikia Taifa, tuendelee kumuenzi na kujifunza kutoka kwake,” amesema Prof.Mkenda.
Kwa upande wake Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Kanali mstaafu Ngemela Lubinga amesema Vicky enzi za uhai wake alitimiza wajibu wake kikamilifu katika kulitumikia taifa na chama na waliobaki wanao wajibu wa kuyaenzi maisha yake kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika eneo alilopo.