Nyemo Malecela, Kagera
Watanzania zaidi ya 15,000 wanatarajiwa kupata ajira kwenye mradi wa ujenzi la bomba la mafuta wenye thamani ya dola milioni 3.5 utakaoanza kujengwa hivi karibuni kutoka Ohima nchini Uganda hadi mkoani Tanga nchini Tanzania kupitia mkoani Kagera.
Takwimu hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani wakati wa semina ya kuzitambua fursa zilizopo katika uwekezaji huo, iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera ambayo iliwashirikisha viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wafanyabiashara na wadau wengine wa mradi huo.
Katika ujenzi wa mradi huo utakaopita katika mikoa nane nchini Tanzania, utakaomilika ndani ya miaka mitatu utatoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa ikiwemo wananchi wanaoishi jirani na litakapolazwa bomba hilo ambapo inadaiwa asilimia 80 za kazi zitakazofanywa katika utekelezaji wa mradi huo zitafanywa watanzania.
“Katika Wilaya 24 utakapopita mradi huo, wilaya nne ziko mkoani Kagera, utapita kwenye kata 34 zote zikiwa za mkoani Kagera, utakuwa na umbali wa kilometa 1,147 wakati kilometa 175 zikiwa mkoani Kagera.
Hivyo, sehemu kubwa ya mradi huu inapita mkoani Kagera, jambo ambalo linawapa fursa kubwa wananchi wa mkoa huo katika suala la ajira za kada zote pamoja na kuongeza wigo wa maendeleo ya mazingira na kiuchumi kwa ujumla,” alisema.
Dk. Kalemani alisema mbali na fursa ya ajira kwa Watanzania pia Mikoa ya Singida, Tabora na Simiyu ambayo inatarajiwa kugundulika mafuta itatumia bomba hilo kusafirisha nishati hiyo kwenda chini Uganda jambo ambalo litaongeza faida kwa watanzania.
“Tuna miradi ya gesi, tayari tumeshaanza mazungumzo na Uganda kwa ajili ya kupeleka nishati hiyo nchini humo hivyo tukifikia makubaliano tutatumia bomba hilo kuisafirisha. Serikali itaokoa gharama nyingi sana ambazo zingetumika kujenga bomba la kusafirishia gesi hiyo na badala yake litatumia bomba hilo la mafuta.
Kupitia ujenzi huo kodi zaidi ya dola milioni 250 na ushuru mwingine tofauti zitalipwa pamoja na fursa nyingine zikiwemo kukua kwa miji,” alisema Dk. Kalemani.
Pia Dk. Kalemani aliwataka watanzania wenye makampuni nchini yenye uwezo wa kufanya kazi katika ujenzi wa mradi huo wajisajiri kwene kanzi data ya EWURA ili wapate kipaumbele cha kupata kazi.
“Wanakagera mnatakiwa kutumia furusa hii kwa kushiriki kwa wingi, kuhakikisha wanatimiza majukumu yao katika zoezi la ujenzi wa mradi, kuufaidi mradi na kuulinda pia ili uendelee kuwanufaisha zaidia.”
Naye Mbunge wa jimbo la Ngara, Ndaisaba Luhoro amewataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kuchangamkia fursa zitakazopatikana katika ujenzi wa bomba hilo ili waweze kuongeza kipato chao cha kila siku.
“Sisi kama wabunge tunajukumu kubwa la kuwahamasisha wananchi wajiandae kuchangamkia fursa zilizopo katika ujenzi wa mradi huo ambazo ni kandarasi, utoaji wa huduma mbalimbali, uuzaji wa vyakula, uuzaji wa mifugo kwa ajili ya nyama, huduma za usafirishaji na nyinginezo.
Wakati huo huo mdau wa vyombo vya habari, Regina Zachwa ameiomba serikali kutenga fungu la fedha kwa ajili elimu kupitia vyombo vya habari hususani radio za kijamii (local radio) ili kuweza kuwafikia wananchi wengi walioko vijiji vya ndani waweze kuchangamkia fursa zinazopatikana katika uwekezaji huo.
“Utumiaji wa radio za kijamii katika utoaji wa elimu kwa wananchi ni muhimu kwa kuwa watanzania wengi walioko vijijini hawana uwezo wa kutumia mitandao ya kijamii kama website kupata elimu ya fursa zinazopatikana katika mradi huo,” alisema Regina.
Mbunge wa Viti Maalum mkoani Kagera, Neema Lugakira alisema wasiwasi wake ni kigezo cha watanzania hasa wanakagera wenye makampuni ambao wanatakiwa kujisajili kwenye kanzi data ya EWURA, ili ujisajili kwenye kanzi data hiyo ni lazima kampuni hiyo iwe imesajiliwa Brela wakati wananchi wengi wanafanya biashara katika sekta zisizo rasmi kwa hiyo wengi hawajajisajili Brela. Hivyo unatakiwa uaangaliwe utaratibu utaakaowawezesha nao kushiriki kikamilifu hata kama hawapo katika sekta rasmi.
Pia ushiriki wa watanzania ambao wanaoishi karibu na mradi kama vile bomba la mafuta na gesi, kuna kitu kinaitwa ‘social license’, yaani unakuwa na leseni zako zote za serikali lakini bado unatakiwa uwe na leseni ya kijamii, hivyo wale waliopo kwenye jamii ndio wenye jukumu kubwa la kulinda huo mradi kutokana na kila siku wako na huo mradi kwa hiyo tunatakiwa tuone ni namna gani serikali itawasaidia katika fursa za ajira kutakuwa na aina ya kada ya ajira kutakuwa na asilimia 10 za ajira wapewe watu wanaotoka pembezoni ya mradi.