AVELINE KITOMARY NA COSTANCIA MUTAHABA
-DAR ES SALAAM
WATU watano wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam kwa mashtaka mawili likiwamo la kuiba fedha.
Waliofikishwa kortini ni James Tumka (32) mkazi wa Tabata, Gaiety Milambwe (31) mkazi wa Bunju, Mwajabu Hamisi (25) mkazi wa Gongolamboto, Cecilia Mjema (29) na Germana Paschal (27) wakazi wa Sinza.
Wakisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Anifa Mwingira, Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Matarasa Hamisi alidai mnamo Aprili 9 na 12 mwaka 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa walitenda kosa la kula njama kwa ajili ya kutenda kosa la wizi.
Katika shtaka la pili, washtakiwa kwa pamoja kati ya tarehe 9 na 12 mwaka 2017 eneo la Mlimani City Wilaya ya Kinondoni waliiba Sh 62,144,245 mali ya Kampuni ya Delta Agra Ltd ambapo walichukua fedha hizo kama waajiriwa.
Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo huku upande wa Jamhuri ukisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe kwa ajili ya hoja za awali.
Hakimu Mwingira alisema dhamana iko wazi kwa kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka katika taasisi zinazotambulika kisheria, ambao watatoa bondi ya Sh milioni 2 kwa kila mmoja. Washtakiwa wanne walikidhi masharti ya dhamana na kuachiwa huku mshtakiwa namba tano alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi kesi yao itakaposomwa tena Aprili 11, mwaka huu