Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewataka wataalamu elekezi wa tathmini ya athari kwa mazingira kubadilika katika utendaji tasnia hiyo iendelee kukua na kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya taifa.
Hayo aliyasema Dar es Salaam mwishini mwa wiki, wakati akifungua mkutano wa pili wa mwaka wa Chama cha Wataalamu Elekezi wa Tathmini Athari za Mazingira, ukaguzi na vibali vya awali.
Alisema wataalamu hao wana umuhimu mkubwa katika ujenzi wa uchumi, lakini lazima wabadilike namna ya utendaji wao wa kazi.
“Katika changamoto za namna ya ufahamu na kufanya wa tathimini na ukaguzi wa mazingira nyie kama chama mna uwezo wa kujipanga kuanzisha programu za mafunzo na kubadilishana uzoefu kwa kufanya hivo itasaidia kuboresha na kuimarisha uwezo wenu wa katika utendaji,’’ alisema Makamba.
Alisema suala la tathimini za athari kwa mazingira linapewa kipaumbele kwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Kuna changamoto kadhaa kwenye usajiri wa wataalam elekezi wa mazingira kuhusu ulipwaji wa ada za mwaka ambako serikali inapoteza mapato yake.
“Taarifa ya NEMC inaonyesha mwaka 2018 wataalam binafsi wanadaiwa Sh milioni 600 na makampuni yanadaiwa Sh milioni 250 kama ada za mwaka,” alisema.
Alisema serikali inawatambua wataalam na kazi zao kwa wale wasiolipa ada za mwaka katika tasnia hii walipe mara moja kabla hatua kali za sheria hazijachukuliwa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Vedast Makota alisema Baraza limejipanga kufanya marekebisho kwenye kanuni ya tozo na ada pamoja na kanuni ya tathimini athari kwa mazingira..
Dk. Makota alisema hadi kufikia mwezi wa nne mwaka huu, NEMC iliweza kutoa kanuni mpya ya ada na tozo ya baraza ambayo kimsingi ilizingatia malalamiko ya wananchi ambao walikuwa wanatozwa katika ada na tozo mbalimbali.
“Hapo awali miradi ilikuwa inatozwa kwa asilimia ya gharama ya uwekezaji lakini kwa sasa tumeliondoa na kuweka viwango ambavyo vitakuwa rafiki kwa wawekezaji,’’ alisema Dk. Makota.
Alisema kwa sasa miradi midogo inatozwa kuanzia milioni mbili tofauti na hapo awali ilikuwa inatozwa kuanzia milioni 10 ambako miradi ya serikali inatozwa Sh milioni 50 kulingana na gharama za uwekezaji wa mradi lakini ilikuwa Sh milioni 500 hadiSh milioni 600.
Dk. Makota alisema kanuni mpya walizozitoa Septemba mwaka huu kwa upande wa sekta ya viwanda, mwekezaji anaruhusiwa kuomba kibali hata kama hajakamilisha matakwa ya msingi kwenye andiko la awali ambako masharti yanamtaka kuwa ndani ya miezi minne awe amepata cheti.
Mwenyekiti wa Chama cha Wataalam Elekezi wa Mazingira Tanzania, Profesa Hussein Sosovele, alisema kama chama kimejipanga kufanikisha azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025 kwa kufanya uchambuzi yakinifu juu ya tathmini ya uwekezaji na kuainisha namna uwekezaji huo utakavyoleta tija bila kuharibu mazingira.
“Chama kitaishauri serikali juu ya namna bora ya kutumia rasilimali bila kuharibu mazingira kwa kiasi ambacho hakitaweza kurekebishika,’’ alisema Prof. Sosovele.