Na SHEILA KATIKULA- MWANZA
WANANCHI wa Mkoa wa Mwanza, wameombwa kujiepusha na migogoro mbalimbali ili kupunguza kesi zilizopo mahakamani.
Wito ulitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Uhuru, Dk Derick Nyasebwa kwenye sherehe za kuhitimisha mafunzo ya awali kwa wahitimu 68 ya uangalizi wa jamii yaliyoandaliwa na Shirika la Mfumo na Muundo wa Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA).
Dk Nyasebwa alisema wapo baadhi ya watu hufanya migogoro kuwa chanzo cha kujipatia kipato.
Alisema migogoro husababisha kukosa amani na furaha na husababisha magonjwa hivyo ni vema katika maisha kujiepusha nayo.
Alisema katika baadhi ya nchi zenye migogoro mikubwa huita wajumbe kutoka sehemu mbalimbali ili waweze kusuluhisha kesi zao.
“Binafsi sipendi migogoro iwepo sehemu yoyote, ila wapo baadhi ya watu wamefanya (migogoro) kama sehemu ya maisha yao, pindi wanapokuwa na kesi wakisuluhishwa hawataki kufikia mwafaka kwa sababu hujipatia fedha kwa kazi hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya kitega uchumi,”alisema Nyasebwa.
Naye Mwanasheria wa Kujitegemea, Remigius Mainde alisema lengo la Mujata ni kutokomeza uhalifu, kuelimisha jamii ili waweze kufanya mambo mema na kupunguza kesi zilizopo mahakamani za uhalifu.
Alisema ni vema vijana kutimiza malengo ya Mujata kwa kufanya majukumu yao waliyofundishwa ili kupunguza vitendo vya uhalifu na waweze kusaidia kundi hilo na kutoka katika mazingira ya uhalifu ili jamii iwe sehemu salama na kujiepusha na kupokea rushwa.
“Watimize malengo yao na wajiepushe na vitendo vya rushwa pindi watakaposhawishiwa kwani vijana huingia kwenye makundi hatalishi na kufanya uhalifu na kuvunja amani,”alisema Mainde.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa shirika hilo, Jacob Matiko, alisema waliamua kuanzisha mafunzo hayo kanda ya ziwa baada kuona changamoto nyingi zinawakabili vijana kwani wapo watu huwashawishi vijana hao na kufanya uhalifu kupelekea kuvuanja wa amani.
Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mwanza, Boniphace Nkobe, aliwataka vijana hao kutumia mafunzo yao vyema kwa kufichua watu ambao wanawaficha watoto wenye walemavu ndani na kukosa haki zao za msingi.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Ayub Michael alishukru shirika hilo kwa kuandaa mafunzo hayo ya miezi mwili ambayo atasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu.