Na Safina Sarwatt, Singida
Timu ya watalaamu wa kilimo, wenyeviti wa vijiji wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Salehe Mkwizu wamefanya ziara ya mafunzo wilayani Manyoni mkoani Singinda lengo likiwa nikujifunza kilimo cha korosho kama zao la kimkakati.
Katika ziara hiyo mafunzo Mkwizu ameambata na baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Mwanga ambapo wametembelea mashamba korosho yaliyoko katika kijiji cha Masigati katika Jimbo la Manyoni Mashariki yenye zaidi ya ekari 22.
Akizungumza leo Desemba 22, baada ya ziara hiyo ya mafunzo Mkwizu amesema kuwa wamekuja kujifunza kutoka kwa wataalamu wa Manyoni kwani katika wilaya ambazo korosho ni zao la kimkakati na wilaya ya Mwanga nayo pia ni mojawapo, hivyo wamekuja kuona ni jinsi gani Manyoni inafanikiwa katika uzalishaji wa zao hilo.
Mkwizu amesema kuwa wamefurahishwa na kwamba sasa nao wanaenda kuanza kutumia mafunzo hayo waliyoyapata kutoka kwa wataalamu ili waweze kuanzisha kilimo hicho cha korosho wilayani Mwanga.
Aidha, Mkwizu amesema kuwa mazingira ya Mwanga na wilaya Manyoni yanafanana, hivyo kuna tija ya kuendelea kujifunza mengi kutoka Manyoni na kwamba kuna haja pia ya kuungana kwa pamoja ili siku moja na wao pia waje wawe kama Manyoni.
“Niseme tumefurahishwa sana na jinsi ambavyo mmetupokea na kutupatia huu utalaam na kwamba tunawaahidi kwenda kuanza sasa na ikifika wakati tutawaita mje muone yale ambayo mmetufundisha, jinsi tunavyoyatekeleza lakini pia niombe msituchoke tutaendelea kuhitaji ushauri wenu wa kila hali ili nasi tuweze kutekeleza mpango huu wa kuifanya korosho kuwa zao la kimkakati Wilaya ya Mwanga.
“Mpango wetu ni kuhakikisha kuwa tunatekeleza ilani ya Chama Cha Mpinduzi(CCM) ambayo imeagiza kuwa kila halmashauri ziwe na mazao ya kimkakati na sisi Mwanga tumechagua Korosho kwa upande wa kata za Kivisini, Jipe na Kigonigoni.
“Hivyo tunayaishi maono na mawazo ya Rais Dk. Joseph Magufuli ambaye anataka Tanzania ya Viwanda kwa kuwa amedhamiria kuimarisha uchumi wetu,” amesema Mkwizu.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Manyoni, Diwani wa viti maalum, Blandina Mawala amesema kuwa wamefurahishwa na umoja huo wa baraza la madiwani kutoka Mwanga kuja kutembelea Manyoni lakini pia kuona miradi ambayo inaendelezwa Manyoni na hasa zao la kimkakati la korosho.
Mawala amesema kuwa Halmashaur ya Wilaya ya Manyoni inasimamia kikamilifu kuona kwamba ilani ya CCM ya kuboresha kilimo na inakuwa na tija na inatekelezwa kikamilifu na hasa katika uboreshaji wa mazao ya kimkakati kama vile zao la korosho.
“Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashaur na kwa niaba ya Mbunge, Dk. Pius Chaya na waheshimiwa madiwani wote niwapongeze kwa hatua mliyochukua ya kuona Manyoni inafaa kuwa chachu na tija ya nyie kujifunza hivyo niseme mmetuamini sana nasi tutaendelea kuwa sehemu ya kushirikiana nanyi kwa jinsi ambavyo mmetuamini hatutawaangusha karibuni tena tutakuwa pamoja na hata sasa mkihitaji wataalamu kutoka Manyoni kuja Mwanga basi niseme tu wako tayari watakuja hivyo niwashukuru sana,”amesema Mawala.
Hata hivyo timu hiyo ya watalamu na madiwani wamefanikiwa pia kutembelea kiwanda cha kubambua korosho.