25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wasomi walivyoibua changamoto mitaala ya elimu nchini

ELIZABETH HOMBO

PAMOJA na mikakati ya Serikali na taasisi mbalimbali ya kuinua elimu ya Tanzania lakini bado imegubikwa na changamoto kadhaa.

Wadau mbalimbali wanapendekeza kupitiwa upya kwa mitaala ya elimu kutokana na sera za sasa za Serikali kufikia uchumi wa viwanda.

Wadau hao walizungumzia changamoto hizo za elimu na namna ya kuzitatua walipochangia mada katika Tamasha la 11 la kitaaluma la Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wiki iliyopita.

Akichangia mada kuhusu Mapitio ya Mitaala ya Tanzania inayopelekea kuwa na uchumi wa viwanda, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Sauti),Profesa Kalafunja Osaki, anasema ili kuiwezesha sera ya viwanda, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wajengewe uwezo huo kabla ya kufika mbali.

“Mitaala inatakiwa itengenezwe katika hali ambayo itabeba mambo matatu ambayo ni uelewa, maendeleo ya mtu binafsi na ujuzi.

“Ni muhimu kumpa mwanafunzi uwanja wa kufanya mambo anayoweza badala ya kufikiri kwamba kila mtu anatamani kuwa profesa au kuwa na shahada,”anasema Profesa Osaki.

Naye Mhadhiri wa elimu Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Duce), Dk. Subirego Kejo anasema ujuzi unaotakiwa kutolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya uchumi wa viwanda ni pamoja na ule uliopo kwenye masoko ya sayansi.

“Kuwezeshwa kwa teknolojia ya habari na mawasiliano, kukuza ubunifu na kutatua matatizo, kujenga tabia ya kujiwekea akiba na kuwekeza, kufanya kazi kwa bidii uzalishaji mali, ujasiriamali na kuwa na nidhamu.

“Kuna ubora ambao unatakiwa kuendelezwa kwa ajili ya Taifa hili. Hayo yote yanatakiwa kujengwa katika hatua za mwanzo za maisha ya binadamu. Mwanafunzi wa chini akifundishwa mapema atachangia katika ukuaji wa uchumi,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kalage anasema kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, ‘elimu inatakiwa imsaidie mwanafunzi kutambua mazingira yake na kumsaidia kukabili changamoto za leo.

Anasema kwa kuzingatia maneno hayo, kila mmoja katika jamii anahitaji kujiuliza je elimu ya hapa nchini inawaandaa wanafunzi kwa hilo.

“Watu wengi huonekana kuwa na wasiwasi kuhusu hili. Ndiyo sababu kuna mahitaji ya ongezeko kubwa la kujiuliza hali ya elimu yetu leo. Hali kadhalika aina ya elimu na mfumo unaotumiwa kuwasilisha ambao unahitajika kuhakikisha uchumi wa nchi yetu kupitia viwanda unatimia ifikapo mwaka 2025.

“Kwa kweli, kuna ongezeko la wazi na wakati mwingine kukata tamaa lakini kushindwa kuonyesha kwa wazi kuhusu elimu kwa ujumla katika ngazi zote ukizingatia changamoto nyingi zinazoendelea kuikabili mfumo wetu wa elimu.  

“Tukiendelea kutafakari kuhusu jamii yenye uelewa na hususan ‘umuhimu wa elimu katika jitihada za Tanzania kuwa uchumi wa viwanda’ kuna maswali kadhaa ya kuvutia ambayo ninajisikia niwahusishe kuchangamsha mawazo yetu.

“Je, mfumo wa sasa wa elimu unaweza kutoa matarajio yetu ya kufanya Tanzania nchi ya pato la kati ifikapo 2025 kupitia viwanda?

“Je, mtaala wa sasa unakidhi mahitaji ya mwanafunzi moja moja na jamii kwa ujumla, Je, wahitimu wetu vyuoni wanapata ujuzi sahihi wa soko la ajira?

“Kwa maneno mengine, kwa kiwango gani tathimini ya sasa inaonyesha utendaji halisi wa mwanafunzi? Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, ‘kazi ya ufanisi inapaswa kuwa sehemu muhimu ya mtaala wa shule na kutoa uzoefu wa kujifunza kwa njia ya ushirikiano wa nadharia na mazoezi. Umuhimu wa mitihani unapaswa kupunguzwa’.

“Je, walimu wetu wamehamasishwa na wenyewe wamejitolea kutekeleza majukumu yao ya kitaaluma?

“Jamii yenye uelewa inachipuka duniani kote. Ni aina gani ya usaidizi inatolewa kwa sasa kuwawezesha walimu ili nao wawasaidie wanafunzi kuendelea ustadi muhimu?

“Masuala mengi ya kuzingatia, maswali mengi ya kuuliza. Lakini maswali haya na mengine mengi yatatusaidia kutafakari upya na kufikiri tena, ikiwa tuna mfumo wa elimu sahihi wa kutoa mpango wetu wa kutamani kuwa nchi ya kipato cha kati kufikia mwaka wa 2025,” anasema.  

Aidha katika tamasha hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Abdullah Hamza alitoa utafiti wake kuhusu watoto wenye umri mdogo kutumishwa migodini na mashambani.

Anasema alibaini hilo baada ya kufanya utafiti huo katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Urambo mkoani Tabora, Ilula mkoani Iringa ambapo maeneo hayo yalilenga namna watoto wanavyotumikishwa katika mashamba ya kibiashara.

Dk. Hamza anasema kwa upande wa migodi, waliangalia mgodi wa dhahabu wa Buhemba mkoani Mara, mgodi wa chumvi wa Uvinza mkoani Kigoma na mgodi wa Tanzanite-Mererani mkoani Manyara.

“Utafiti wetu ulikuwa wa watu 471 ambapo katika kila kijiji tulihoji watu 78, mgawanyo wa watoto 30, wazazi 30, walimu 10, maofisa elimu 5, wamiliki wa mashamba na migodi 3.

“Tulitumia interview na mijadala ya makundi na katika mashamba tuliwakuta watoto wanatumikishwa mashambani na katika migodi ya Uvinza na Buhemba,”anasema Dk. Hamza.

Anasema walipowahoji watoto hao sababu za kufanya kazi, walisema wanaishi na bibi zao hivyo wanalazimika kufanya kazi ili wawapelekee hela ya chakula nyumbani.

“Walitueleza kuwa wanafanya hivyo ili waishi kwani bibi zao hawana uwezo, hivyo mara nyingi hufanya kazi hizo siku za Jumamosi na Jumapili na muda wa jioni wakitoka shule lakini pia wapo ambao walilazimika kuacha shule na kujikita katika kazi.

“Wengine pia wanafanya kazi hizo kwa sababu ya tamaa mfano mwenzao aliwaringishia hela hivyo na yeye anaenda kufanya kazi ili apate hela, pia wengine ni kwa sababu wanalelewa na mzazi mmoja.

“Pia wazazi wengine walitueleza kuwa wanawapeleka watoto mashambani lengo likiwa ni kuwafundisha kazi na wala si kuwatumikisha,”anasema Dk. Hamza.

Akizungumzia kuhusu wamiliki wa mashamba na migodi walipohojiwa, walisema wanachukua watoto kufanya kazi kwa sababu sio wabishi na wanapatikana kirahisi.

“Wanasema yaani ukiwatajia kiasi cha fedha hawabishi hata kama kidogo wao wanakubali na wana bidii ya kufanya kazi, pia unaweza kuwakopa na ni watiifu,”anasema.

Akizungumzia kuhusu mashamba ya biashara katika eneo la Ilula, anasema walibaini asilimia 93 ya watoto kati ya miaka 7-17 wanafanyishwa kazi za kulima katika siku za Jumamosi na Jumapili pamoja muda wa jioni baada ya kutoka shule.

Kwa upande wa mgodi wa Buhemba, anasema walibaini asilimia 80 ya watoto kati ya miaka 6-18 wanafanya kazi katika migodi, ingawa asilimia 60 ya wazazi walisema wanaofanya kazi hizo ni wale waliotimiza miaka 18.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu, Profesa Rwekaza Mukandala anasema ili kupiga hatua za maendeleo mataifa ya Afrika yanahitaji elimu ya kujitegemea ambayo inachanganya vizuri nadharia na vitendo.

“Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa mbali sana, tunahitaji elimu ya kujitegemea ambayo inachanganya vizuri nadharia na vitendo.

“Kwa hiyo wanafunzi wanaohitimu wanakuwa wameiva wana nadharia ya kutosha, kwa sababu huwezi kutenda vitendo bila kuwa na nadharia ya uelewa wa misingi ya maisha, lakini vilevile wawe wamefundishwa namna ya kutenda wana uzoefu, wamefanya majaribio.

“Kwa hiyo wanakuwa ni watendaji wazuri si wanaozubaa zubaa, pili wawe ni watu wanaoweza kujituma siyo wanaosubiri tu kuajiriwa, kwa hiyo ni kurudi tu mimi nadhani sera nyingi zipo na tukianzia sera ya Mwalimu Nyerere na kuzisimamia vizuri.

“Mwaka jana tulifanya utafiti kuhusu ubinafsishaji hasa wa migodi na mashamba ya tumbaku na mazao mengine na kuhusu uajiri wa watoto wadogo ambao kutokana na ajira hizo wanashindwa kwenda shule” alisema Profesa Mkandala.

Kuhusu sera ya elimu bure, anasema hiyo ni hatua moja muhimu na nzuri, lakini juhudi zinahitajika ikiwa ni pamoja na kuongeza vifaa, walimu, madarasa na kuhakikisha miundombinu na mazingira ya kutoa elimu yanakuwa bora.   

 “Bado watoto wenye umri wa kwenda shule hawajaweza kwenda shule na hiyo ni kwa sababu mbalimbali wengine ni kwa sababu ya umaskini, wengine ni kwa sababu ya vishawishi mbalimbali, kwa hiyo linalojitokeza katika huu mjadala ni kwamba sheria zimeshapitishwa zisimamiwe vizuri, zitekelezwe watu wote wenye umri wa kwenda shule waende.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk. Lucas Mkonongwa, anasema ili kukomesha ajira kwa watoto, sheria kali zinapaswa kuchukuliwa kama inavyofanyika kwa watu wanaokutwa na nyara za serikali.

“Tatizo ni kwamba hatujaweka kipaumbele kama tulivyofanya kipaumbele kwa mambo mengine kama nyara za Serikali, leo hii ukikamatwa na bangi unachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Ukikamatwa na ngozi ya chui unachukuliwa hatua kali za kisheria ukikamatwa na madini bila utaratibu unachukuliwa hatua kali za kisheria kwanini hatuwachukulii hatua kali za kisheria za namna hiyo hio wale wanaotumikisha,” anasema Dk. Mkonongwa.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva anasema awamu ya tano imejitahidi kwa kuwepo elimu bure lakini bado kumekuwa na changamoto ya watoto wengi kutokwenda shule.

Mwakilishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Felister Mauya anasema kuna masuala ambayo hayapewi kipaumbele mfano katika kata zipo shule lakini mtoto anapelekwa kusoma shule ya mbali.

“Sasa mtoto anapopelekwa shule ya mbali mzazi nauli anapataje? Hivyo lazima mazingira mazuri ya mtoto kusoma yaandaliwe.

“Changamoto nyingine ni rushwa ambapo wazazi wamekuwa wakiozesha watoto ili wapewe ng’ombe au fedha, hivyo kila mmoja lazima awe mlinzi katika jamii kutokomeza ndoa za utotoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles