29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wasomi waichambua Ukawa

ukawaSHABANI MATUTU NA PATRICIA KIMELEMETA
SIKU moja baada ya Kamati Maalumu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutoa mapendekezo ya ugawaji wa majimbo 211 kati ya 239, wasomi na wachambuzi wa siasa wametoa maoni yao.
Wakizungumza na MTANZANIA jana, wasomi na wachambuzi hao wa siasa pamoja na mambo mengine, walisema bado Ukawa wanatakiwa kueleza umma namna watakavyoandaa ilani yao na kuinadi mbele ya wananchi.

DK. BANA
Akitoa maoni yake jijini Dar es Salaam, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema anatamani kuona Ukawa wanafanikiwa kuwa mbadala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dk. Bana alisema pamoja na kutamani CCM iondoke madarakani, lakini anataka kujua kama sheria za nchi zilifuatwa katika kugawana majimbo vyama washirika wa Ukawa.
“Sisi tungetaka CCM iondoke, hata mimi binafsi ningetaka kuwe na mbadala, lakini najiuliza, kwa mgawanyo huu, ruzuku itakwenda wapi? Chadema au Ukawa kwa sababu sheria inatambua Chadema na si Ukawa.
“Sijui Pemba Chadema wameachiwa majimbo mangapi. Je, mgawanyo huo ni wa kitaifa au wa kikanda? Kila chama kina wagombea wangapi? NCCR na Chadema wana majimbo mangapi Ruvuma, au wanataka kuigawa nchi vipande vipande?” alihoji Dk. Bana.

PROFESA SEMBOJA
Profesa Haji Semboja, alisema katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mambo kadhaa huibuka ila suala la muhimu ni kuhakikisha vyama vinateua watu wenye sifa na wenye kukubalika kwenye maeneo yao.
“Hizo ni mbinu tu za kutafuta ushindi, lakini wanapaswa kujiuliza je, wanaowachagua wanakubalika kwenye maeneo hayo? Bila ya kufanya hivyo ni sawa na kupoteza muda,” alisema Profesa Semboja ambaye ni mtaalamu wa uchumi.
Alisema kila chama kina aina yake ya kutafuta ushindi, lakini wanapaswa kuangalia kipindi hiki wananchi wengi wana uelewa zaidi, hivyo wanapaswa kuweka watu makini ambao wataweza kuwasaidia kufanikisha mipango yao ya kushinda uchaguzi.

PROFESA MPANGALA
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala, alisema hata kama kuna chama kinachounda Ukawa kina mikakati yake ya ushindi, lakini wanatakiwa kushirikiana ili waweze kufanikiwa kwa pamoja.
Alisema katika mkakati huo, ikiwa watatoa sera yao ya kupeleka utawala kwenye kanda hawatafanikiwa kwa sababu imekaa kitendaji zaidi na siyo kwenye kampeni.
Kauli za wasomi hao zimekuja ikiwa ni siku moja baada ya gazeti hili kuripoti kuhusu Kamati Maalumu ya Ukawa, kukamilisha kazi ya ugawaji wa majimbo 211 ambayo ni sawa na asilimia 88 kati ya majimbo yote 239.
Kamati hiyo ilishindwa kuafikiana katika majimbo 28 ambayo yanasubiri uamuzi wa wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa, ambao watamaliza kiporo hicho mwezi huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa juu wa umoja huo, kutangaza mkakati wa kusimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana majimbo ya uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Ukawa ni umoja ulioanzishwa Februari mwaka jana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba, ukiundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo maalumu, mgawanyo wa majimbo kwa Mkoa wa Dar es Salaam umeangalia vigezo vya kukubalika kwa mtu pamoja na yalipo makao makuu ya chama.
Kutokana na hali hiyo, Chadema imekubaliwa itasimamisha wagombea katika majimbo ya Ubungo, Kawe, Kinondoni na Ukonga, huku CUF ikiachiwa majimbo ya Segerea, Temeke na Kigamboni na NCCR-Mageuzi ikipewa Ilala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles