31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Spika amzuia Zitto kuachia ubunge

Na Fredy Azzah, Dodoma
AZMA ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), ya kujiuzulu ubunge imegonga mwamba baada ya kuelezwa kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, amemzuia kufanya hivyo, imefahamika.
Zitto ambaye alikuwa ameshafanya maandalizi ya kuaga jana ndani ya Bunge, alijikuta akigonga mwamba dakika za mwisho baada ya kuingia bungeni na kuelezwa na mmoja wa maofisa wa Bunge kuwa suala lake la kutoa hotuba limeahirishwa na Spika Makinda akitakiwa kwanza kuifanyia marekebisho.
Kabla ya kuingia bungeni, Zitto alikuwa akibadilishana mawazo na mwanasheria wake, Albert Msando, huku akiwa ameshika jalada maalumu ambalo ndani yake kulikuwa na hotuba ambayo angeisoma.
Dalili za Zitto kuachia ngazi zilianza kuonekana jana asubuhi baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kutoa tangazo kuwa kikao cha jioni kitaongozwa na Spika wa Bunge na sio yeye.
Ilipotimu saa 11:30 jioni, Zitto alitinga katika viwanja vya Bunge, akitumia muda mwingi kutaniana na waandishi wa habari huku akiwa anazungumza na simu ya mkononi.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, ili kupata ufafanuzi wa taarifa za kujiuzulu kwa Zitto, alisema hana taarifa zozote za suala hilo.
Zitto ambaye alianza kuwawakilisha wananchi wa Kigoma Kaskazini kwenye Bunge la tisa kwa tiketi ya Chadema, alitarajiwa kukamilisha safari yake hiyo kwenye Bunge la 10, mkutano wa 19, kikao cha tatu baada ya chama chake kutangaza kumvua uanachama.
Mwanzoni Zitto alitarajiwa kuchukua uamuzi huo juzi, lakini aliahirisha baada ya Spika Makinda kumtaka afanye naye kikao.
Katika kikao cha juzi, Zitto alichangia kwenye Muswada wa Sheria ya Kudhibiti Ajira za Wageni wa Mwaka 2014, ambapo watu wengi walifikiri angetumia fursa hiyo kuaga.
Juma lililopita, Zitto aliwaaga wananchi wa Kigoma Kaskazini na kusema hatogombea tena ubunge kwenye jimbo hilo, akisema ataendelea kuwatumikia akiwa sehemu nyingine.
Machi 10, Mwanasheria wa Chama cha Chadema, Tundu Lissu, alitangaza kumvua uanachama Zitto, baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi yake.
Mara baada ya Zitto kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge juzi na waandishi wa habari kutaka kujua hatima yake, kutokana na kuhudhuria bungeni ilihali chama chake kimetangaza kumvua uanachama, alisema: “Jamani si mmeona nimekuja na nimechangia kama mwingine yeyote?”
Swali: Lakini kuna tetesi kuwa ulikuja leo kwa lengo la kutangaza kujiuzulu?
Jibu: Zitabaki kuwa tetesi tu, lakini muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi. Ngoja kwanza niende kwa Spika ameniita.
Swali: Kwa Spika mnaenda kuzungumzia suala hilihili la tetesi (kujiuzulu) ama?
Jibu: Siwezi kuyazungumzia hayo bwana.

Licha ya Chadema kutangaza kumvua Zitto ubunge, juzi Spika Makinda, alisema licha ya kusikia kwenye vyombo vya habari habari hizo, hadi sasa hajapata taarifa rasmi.
“Suala hili lilikuwa mahakamani, kwahiyo uamuzi wake mpaka sisi tuupate rasmi siyo kusikia tu kwenye mitandao huko, mpaka sasa sisi hatujapata taarifa rasmi,” alisema Makinda.
Alisema Bunge litakapopata taarifa hizo, litachukua hatua kwa mujibu wa sheria na kwamba kwa muda uliobaki sasa, hakutakuwa na uchaguzi wa ubunge kujaza nafasi itakayokuwa imeachwa wazi.
“Sheria inasema ikiwa imebaki miezi 12 kabla ya kikao cha 20 ambacho huwa ndiyo cha mwisho, uchaguzi hauwezi kufanyika, na kwa mujibu wa mabadiliko ya ratiba zetu, kikao cha bajeti ndiyo kitakuwa cha 20 amacho kinaisha Julai,” alisema Makinda.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, Zitto alisema hatima yake ya kisiasa baada ya kutimulia Chadema itajulikana juma hili.
“Ni nini kinachokuja baada ya hapo (tutakijua vizuri wiki hii). Hatujajua kama Chadema wameandika barua kwa Spika ili kunitangaza kuwa jimbo liko wazi, kama wameandika tutakaa kujua ni nini cha kufanya.
“Baada ya ile kesi yangu kwisha, ilipaswa taratibu zifuatwe, hadi sasa sijapata taarifa zozote za kufukuzwa, ndiyo maana nasema hadi wiki hii iishe tutajua,” alisema.
Machi 10, mwaka huu, Chadema iilitangaza kumvua rasmi uanachama Zitto.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupa kesi iliyofunguliwa na Zitto dhidi ya Bodi ya Udhamini ya chama hicho na katibu wake, Dk. Wilibrod Slaa.
Kesi hiyo ilitupwa na Jaji Richard Mziray baada ya kupitia hoja za mapingamizi matano yaliyowasilishwa na mawakili wa Chadema.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo wa mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alizungumza na waandishi wa habari na kusema tangu Zitto alipokishtaki chama hicho mahakamani, kwa mujibu wa kanuni na maadili ya viongozi wa chama alishajifukuzisha uanachama.
“Kwa mujibu wa kanuni zinazohusu maadili ya viongozi ya chama chetu, kanuni ya 10 inaeleza kuwa pale mwanachama anapokishtaki chama mahakamani anakuwa amejifukuzisha uanachama,” alisema Lissu.
Kutokana na hali hiyo Lissu alisema tangu walipowachukulia hatua aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Kitila Mkumbo, walishamalizana na Zitto bali kilichokuwa kimebaki ni kusubiri uamuzi wa mahakama.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya chama, kanuni ya maadili ya wabunge na madiwani, Zitto si mwanachama wa Chadema na wala si mbunge wa Kigoma Kaskazini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles