Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya Chama Cha Mapiduzi (CCM) kutangaza vigogo 32 wanaounda kamati ya kampeni ya mgombea urais wa chama hicho, baadhi ya wachambuzi na wasomi wameikosoa timu hiyo wakisema haina jipya.
Akizungumza jana kwa simu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudens Mpangala, alisema anashangazwa na wingi wa wajumbe wa timu hiyo akisema ni dhahiri mwaka huu chama hicho tawala kinakabiliwa na upinzani mkali.
“Nimeshangazwa na uwingi wa wajumbe, hii inaonyesha kwamba mwaka huu CCM inakabiliwa na upinzani mkali kutoka upinzani. Ukiangalia wajumbe wote ni wakereketwa wa chama na wengine ni wale waliogombea urais,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema timu hiyo iliyopewa jina la ‘ushindi’ ina kazi kubwa ya kuwashawishi Watanzania wakichague tena chama hicho kwa sababu kinakabiliwa na uovu mwingi.
“Kwanza CCM kwenye kampeni ina kazi mbili, moja ikiwa ni kuwaeleza na kuwashawishi watawafanyia nini Watanzania, pili wana ‘madhambi’ mengi zikiwamo kashfa mbalimbali hivyo wana kazi ya kujisafisha na sijui wataanzia wapi,”alisema Profesa Mpangala.
Alitoa rai kwa vyama vya siasa katika kipindi hiki kufanya kampeni za ustaarabu ya kuwashawishi Watanzania na wasijikite katika kuwajadili watu.
BASHIRU ALLY
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema timu hiyo haina jipya kwa sababu tangu mwaka 1995 chama hicho kimekuwa kikiunda timu ya aina hiyo.
“Sina maoni kwa sababu timu hiyo haina jipya, tangu mwaka 1995 CCM imekuwa ikiunda timu ya aina hiyo na ikiongozwa na Abdulrahman Kinana na imekuwa ikishinda na sasa wenyewe wamesema ni timu ya ushindi, sasa sisi tuchambue nini? Tusubiri kwanza wakishindwa ndiyo tutapima,”alisema Bashiru Ally.
Dk. BISIMBA
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema Watanzania wa sasa wamepevuka na si rahisi kuwaeleza jambo la mzaha.
“Binafsi bado sijaona hata hiyo ilani yao. Lakini wakija na hoja za nguvu wataweza kuwashawishi watanzania, vile vile watanzania wa leo wamepevuka si rahisi kuwaeleza jambo mzahamzaha wakakuelewa,”alisema Bisimba.
Juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitangaza timu hiyo ambayo itaongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Kamati hiyo pia ina wajumbe ambao walitemwa kwenye mbio za urais ndani ya CCM, wajumbe wa Kamati ya Bunge iliyochunguza suala la Richmond na wajumbe ambao walikuwa kambi ya mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa.
Pia wapo makada maarufu kwa vijembe dhidi ya wapinzani na wale ambao walishaweka bayana uhasimu wao na Waziri Mkuu huyo wa zamani.