26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wasomi waanzisha taasisi ya kodi

NA MWANDISHI WETU
VIJANA wanane wenye elimu ya vyuo vikuu wameanzisha taasisi yao itakayokuwa ikijihusisha na masuala ya elimu ya ulipaji kodi.
Taasisi hiyo iitwayo CTA ilitangazwa jana jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi waaanzilishi.
Akizungumza katika mkutano huo, Msemaji wa taasisi hiyo, Victor Lukomanya, alisema wamelazimika kuianzisha baada ya kuona sehemu kubwa ya Watanzania wenye sifa za kulipa kodi hawafanyi hivyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema taasisi yao itakuwa na jukumu la kuwasiliana na Serikali na kuwaeleza njia sahihi za kuwafanya wananchi waone fahari kulipa kodi kama inavyofanyika katika baadhi ya nchi duniani.
“Tafiti zilizofanywa kwa nyakati tofauti katika nchi za Chile, Peru, Afrika Kusini, Jamaica, Kenya, Nigeria na Mauritius, zimeonyesha kwamba, maendeleo katika nchi hizo yalitokana na ulipaji kodi.
“Katika nchi hizo, elimu ya kodi ilitolewa kwa watu wa kada mbalimbali ikiwamo walimu, wanafunzi, wafanyabiashara na wengineo wengi.
“Baada ya elimu hiyo kutolewa kupitia tovuti, vyombo vya habari, michezo, mikutano ya ndani na ya hadhara, malumbano ya hoja na kwenye makongamano, wananchi walielewa umuhimu wa kodi na kuamua kuanza kulipa kama kawaida.
“Kwa hiyo, kwa kuwa sisi tunataka nchi yetu ipige hatua na kuendelea, sisi kama wasomi wa nchi hii tumeamua kuanzisha taasisi hii kwa nia njema kabisa ili tulikomboe taifa letu,” alisema Lukomanya.
Kwa mujibu wa Lukomanya, moja ya tatizo kubwa linalorudisha nyuma maendeleo ya Tanzania ni wananchi kukwepa kodi, kwa sababu hawana elimu ya umuhimu wa kodi jambo ambalo wanataka kukabiliana nalo ili nchi iweze kusonga mbele.
Naye Katibu wa CTA, Merchior Sanga, alisema pamoja na kuanzisha taasisi hiyo wakijua changamoto watakazokabiliana nazo, hawatakata tamaa kwa kuwa wanataka Tanzania iwe nchi bora kimaendeleo kama zilivyo nchi nyingine duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles