26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WASICHANA WATIKISA KIDATO CHA PILI

NA AZIZA  MASOUD- DAR ES SALAAM


WANAFUNZI  wasichana waliofanya mtihani wa kidato cha pili mwaka jana, wameongoza kwa kushika nafasi ya kwanza hadi ya 10.

Akitangaza matokeo hayo pamoja na ya darasa la nne jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema shule binafsi ndizo zilizoingia katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.

Dk. Msonde alisema katika mtihani wa upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili (FTNA) uliofanywa Novemba 13 mpaka 24 mwaka jana, wanafunzi 521,759 waliandikishwa na kati yao waliosajiliwa ni 486,742, sawa na asilimia 93.29 .

Alisema  katika matokeo ya mwaka huu wanafunzi walioingia katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa ni wasichana  pekee.

“Wanafunzi 10 bora kitaifa ambao wote ni wasichana ambao wametoka katika Shule ya Feza wasichana ya Dar es Salaam  iliyotoa mwanafunzi wa nafasi ya kwanza na ya pili wakati Shule ya Canossa ya Dar es Salaam ikitoa kuanzia mshindi wa tatu mpaka wa nane na nafasi ya tisa na 10 zimeshikwa na wanafunzi wa Shule ya Precious Blood ya Arusha,” alisema Dk. Msonde.

Aliwataja watahiniwa 10 bora kitaifa ambao pia wamo katika orodha ya wasichana 10 bora kitaifa kuwa ni Shamimu Mohamed, Rukia Abdallah kutoka Shule ya Sekondari ya Feza Wasichana, mshindi wa tatu na wa nne ni Jacqueline Kivuyo na Marina Kasumba  kutoka Shule ya Sekondari ya Canossa.

Mshindi wa tano aliyeingia katika 10 bora ni Kate Penina Mgabo, wa sita ni Sylivia Tibenda, wa saba ni Zuhura Sapi na wa nane ni Gladys Maluli, wote kutoka Shule ya Sekondari ya Canossa.

Dk. Msonde aliwataja wanafunzi walioshika nafasi ya tisa na ya kumi kuwa ni Elizabeth Kimaro na Magdalena Munisi wote kutoka Precious Blood ya Arusha.

Alisema kati ya wanafunzi 486,742 waliofanya mtihani wa upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili watahiniwa 433,453 ambao ni sawa na asilimia 89.32 wamepata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu.

“Kati ya hao wasichana wapo 224,736 sawa na asilimia 88.55 na wavulana ni 208,717 sawa na asilimia 90.17 ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo watahiniwa 372,228  sawa na asilimia 91.02 walipata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu ,” alisema Dk. Msonde.

Alisema idadi ya watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza mpaka la tatu ni 195,742 sawa na asilimia 40.34, kati ya hao wasichana ni 88,167 sawa na asilimia 34.75 na wavulana 107,575  sawa na asilimia 46.48.

Dk. Msonde alisema wanafunzi 51,087  sawa na asilimia 10.68 wameshindwa  kupata alama za kuwawezesha  kuendelea na kidato cha tatu.

Alisema kwa matokeo hayo, baraza pia limepanga ubora wa shule kwa kutumia kigezo cha wastani wa pointi ambapo kati ya shule 100 zilizofanya vizuri kitaifa, shule 10 bora ni za binafsi.

Alizitaja shule hizo kuwa ni Shule ya Sekondari ya Kemebos ya mkoani Kagera iliyokuwa na watahiniwa 43, nafasi ya pili imeshikwa na Shule ya Sekondari Canossa ya Dar es Salaam iliyokuwa na wataniwa 104 na ya tatu ni Shule ya Wasichana ya St.Francis ya Mbeya iliyokuwa na watahiniwa 92.

Alisema Shule ya Wavulana ya Marian ya Pwani iliyokuwa na wanafunzi 105 ikishika nafasi ya nne.

“Nafasi ya tano imeshikwa na Shule ya Kilimanjaro Islamic iliyopo Arusha iliyokuwa wanafunzi 73 , wakati Precious Blood ya Arusha iliyokuwa na watahiniwa 92 ikishika nafasi ya sita,” alisema Dk. Msonde.

Katika orodha hiyo, Dk. Msonde aliitaja Shule ya Sekondari St. Augustine-Tagata ya Dar es Salaam iliyokuwa na wanafunzi 134  kuwa imeshika nafasi ya saba na Shule ya Sekondari Don Bosco Seminary ya Iringa iliyokuwa na watahiniwa 65 imeshika nafasi ya nane.

Alisema Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian ya mkoani Pwani iliyokuwa na watahiniwa 103 imeshika nafasi ya tisa wakati nafasi ya 10 imeshikwa na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Anwarite ya Kilimanjaro iliyokuwa na watahiniwa 54.

Aidha Dk.Msonde alitaja shule 10 za mwisho kitaifa kuwa ni Malegesi iliyokuwa watahiniwa 133, Ukata ya mkoani Ruvuma iliyokuwa na watahiniwa 41, Mswaha ya Tanga iliyokuwa na watahiniwa 145.

Alizitaja nyingine kuwa ni Mlungui iliyopo Tanga iliyokuwa watahiniwa 124, Madangwa ya Lindi iliyokuwa watahiniwa 155 na Mayo Day ya Tanga iliyokuwa watahiniwa 144.

Katika mlolongo huo alizitaja pia shule za Lengo ya Mtwara iliyokuwa na wanafunzi 140, Kwemashai ya Tanga iliyokuwa na wanafunzi 83, Mbwei ya Tanga iliyokuwa na wanafunzi 51 na Zirai ya Tanga iliyokuwa na wanafunzi 80.

Alisema ufaulu wa wanafunzi katika masomo  ya msingi yaani, Geografia, Kiswahili, Kiingereza, Fizikia, Kemia na Hisabati umepanda ikilinganishwa na mwaka 2016.

Kwamba ufaulu wa  masomo ya Uraia, Historia na Biologia umeshuka ukilinganishwa na mwaka 2016 huku somo la Kiswahili  likipata ufaulu mzuri zaidi wa asilimia 91.92 wakati somo lenye ufaulu wa chini likiwa hisabati ambalo lina ufaulu wa asilimia 32.00.

Aidha NECTA limezuia matokeo kwa wanafunzi 105 ambao waliugua ama kupata matatizo na kushindwa kufanya mtihani huo kwa masomo yote au baadhi.  Wanafunzi hao wamepewa fursa ya kufanya mtihani huo tena mwaka huu kwa mujibu wa kifungu cha 30(1) cha kanuni za mtihani…….

Kwa habari zaidi jipatie nakala yako ya MTANZANIA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles