30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wasichana vinara matokeo kidato cha VI

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha sita, huku ufaulu ukiwa umeongezeka kutoka asilimia 97.58 mwaka jana hadi 98.32 mwaka huu.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, wasichana waliofaulu ni 37,219 sawa na asilimia 99.11 ya wote waliofanya mtihani, huku wavulana waliofaulu wakiwa ni 50,850 sawa na asilimia 97.75.

Akitangaza matokeo hayo jana mjini Unguja Zanzibar, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema ufaulu huo umeongezeka ikiwa ni sawa na asilimia 0.74.

Alisema mtihani huo uliofanyika Mei 6 hadi 23, mwaka huu, watahiniwa 91,298 walisajiliwa wakiwamo wasichana 37,948 sawa na asilimia 41.56 na wavulana 53,350 sawa na asilimia 58.44.

Dk. Msonde alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa, wa shule walikuwa 80,216 na wa kujitegemea 11, 082.

Alisema kati ya watahiniwa 91,298 waliosajiliwa kufanya mtihani, 90,001 sawa na asilimia 98.58 ndio waliofanya na 1,297 sawa na asilimia 1.42 hawakufanya kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ugonjwa na utoro.

Dk. Msonde alisema kwa watahiniwa wa shule, kati ya 80,216 waliosajiliwa, 79,770 sawa na asilimia 99,44 walifanya mtihani ambapo wasichana walikuwa 33,883 sawa na asilimia 99.57 na wavulana 45,887 sawa asilimia  99.35. Watahiniwa 446 sawa na asilimia 0.56 hawakufanya mtihani.

Alisema watahiniwa wa kujitegemea kati ya 11,082 waliosajiliwa, 10,231 sawa na asilimia 92.32 walifanya mtihani na 851 sawa na asilimia 7.68 hawakufanya.

“Watahiniwa 88,069 sawa na asilimia 98.32 ya watahiniwa waliofanya mtihani wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 37,219 sawa na asilimia 99.11 wakati wavulana waliofaulu ni 50,850 sawa na asilimia 97.75. Mwaka 2018 watahiniwa waliofaulu walikuwa 83,581 sawa na asilimia 97.58,” alisema Dk. Msonde.

Kuhusu ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule, alisema unaonesha watahiniwa 76,655 sawa na asilimia 96.61 wamefaulu katika daraja la kwanza na pili.

Dk. Msonde alisema katika madaraja hayo, wamo wasichana 32,887 sawa na asilimia 97.22 na wavulana 43,768 sawa na asilimia 96.15.

“Takwimu za ufaulu kwa watahiniwa wa shule mwaka 2019 ikilinganishwa na mwaka 2018 zinaonyesha kuwa ufaulu katika masomo ya Geography, Kiswahili, English Language, French Language, Arabic Language, Physics, Chemistry, Agriculture, Computer Science, Basic Applied Mathematics, Advanced Mathematics, Economics, Commerce na Food and Human Nutrition umepanda ikilinganishwa na mwaka 2018.

“Ufaulu katika masomo ya General Studies, History, Biology na Accountancy umeshuka kidogo ikilinganishwa na mwaka 2018,” alisema Dk. Msonde.

SHULE KUMI BORA KITAIFA

Aidha, Dk. Msonde alizitaja shule kumi bora kitaifa kuwa ni pamoja na Kisimiri (Arusha), Feza Boys (Dar es Salaam), Ahmes (Pwani), Mwandet (Arusha) na Tabora Boys (Tabora).

Nyingine ni Kibaha (Pwani), Feza Girls (Dar es Salaam), St. Marys (Mazinde Juu-Tanga), Canossa (Dar es Salaam) na Kemebos (Kagera).

SHULE KUMI ZA MWISHO

Alizitaja shule kumi za mwisho kuwa ni pamoja na Nyamunga (Mara), Haile Selassie (Mjini Magharibi – Unguja), Tumekuja (Mjini Magharibi – Unguja), Bumangi (Mara) na Buturi (Mara).

Nyingine ni Mpendae (Mjini Magharibi – Unguja), Eckernforde (Tanga), Nsimbo (Katavi), Mondo (Dodoma) na Kiembesamaki A Islamic (Mjini Magharibi – Unguja).

WATAHINIWA BORA MASOMO YA SAYANSI

Dk. Msonde aliwataja watahiniwa kumi bora katika masomo ya Sayansi kuwa ni pamoja na Faith Matee (St Marys – Tanga), Herman Kamugisha (Kisimiri – Arusha), Levina Chami (St Mary Goreti – Kilimanjaro), Benius Eustace (Mzumbe – Morogoro) na Augostino Omari (Ilboru – Arusha).

Wengine ni Satrumin Shirima (Temeke – Dar es Salaam), Khalid Abdallah (Feza Boys – Dar es Salaam), Assad Msangi (Feza Boys – Dar es Salaam), Peter Riima (Kibaha – Pwani) na Augustine Kamba (Feza Boys – Dar es Salaam).

WASICHANA KUMI BORA MASOMO YA SAYANSI

Dk. Msonde alisema kwa upande wa wasichana waliofanya vizuri masomo ya Sayansi ni Faith Matee (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Levina Chami (St Mary Goreti – Kilimanjaro), Wahida Janguo (Feza Girls – Dar es Salaam), Vannesa Rutabana (Tabora Girls – Tabora).

Wengine ni Pielina Figowole (Tabora Girls – Tabora), Loveness Mloge (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Wahda Uzia (Zanzibar Feza – Mjini Magharibi), Beatrice Mwella (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Consolata Matee (St Marys Mazinde Juu – Tanga) na Maimuna Mshana (Marian Girls – Pwani).

WAVULANA KUMI BORA MASOMO YA SAYANSI

Kwa upande wa wavulana waliofanya vizuri masomo ya Sayansi, Dk. Msonde aliwataja Herman Kamugisha (Kisimiri – Arusha), Benius Eustace (Mzumbe – Morogoro), Augostino Omari (Ilboru – Arusha), Satrumin Shirima (Temeke – Dar es Salaam) na Khalid Abdallah (Feza Boys – Dar es Salaam).

Wengine ni Assad Msangi (Feza Boys – Dar es Salaam), Peter Riima (Kibaha – Pwani), Augustine Kamba (Feza Boys – Dar es Salaam), Shedrack Siame (Uwata – Mbeya) na Noel Maro (St Mary Goreti – Kilimanjaro).


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Feza wakiwapongeza wahitimu wa kidato cha sita wa shule hiyo, Khalid Hussein Abdallah (kulia) aliyeshika nafasi ya tano wavulana  na Assad Yahya Msangi aliyeshika nafasi ya sita katika matokeo yaliyotangazwa,Dar es Salaam jana.PICHA SILVAN KIWALE



KUMI BORA MASOMO YA LUGHA NA SANAA

Aliwataja watahiniwa kumi bora masomo ya lugha na sanaa kuwa ni Victor Mtui (Feza Boys – Dar es Salaam), Paula Lujwangana (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Blandina Nyange (St Marys Mazinde Juu – Tanga) na Eva Shitindi (Machame Girls – Kilimanjaro).

Wengine ni Ruhinda Mashimu (Gaeuta Adventist – Geita), Anita Massawe (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Karim Muhibu (Nyangao – Lindi), Anold Msuya (Dareda – Manyara), Latifa Mrosso (Ahmes – Pwani) na Elibariki Balinyanga (Lukole – Kagera).

WASICHANA BORA MASOMO YA LUGHA NA SANAA

Aliwataja wasichana kumi bora masomo ya lugha na sanaa kuwa ni Paula Lujwangana (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Blandina Nyange (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Eva Shitindi (Machame Girls – Kilimanjaro), Ruhinda Mashimu (Gaeuta Adventist – Geita).

Wengine ni Anita Massawe (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Latifa Mrosso (Ahmes – Pwani), Mwanakombo Ramadhani (Mtwara Girls – Mtwara), Katarina Shao (Kisimiri – Arusha), Pakusana Chaula (St Marys Mazinde Juu – Tanga), Minnah Mtingwa (Feza Girls – Dar es Salaam) na Jasintha Deogratias (Lukole – Kagera).

WAVULANA BORA MASOMO YA LUGHA NA SANAA

Dk. Msonde aliwataja wavulana kumi bora wa masomo ya lugha na sanaa kuwa ni Victor Mtui (Feza Boys – Dar es Salaam), Ruhinda Machimu (Geita Adventist – Geita), Karim Muhibu (Nyangao – Lindi), Anold Msuya (Dareda – Manyara) na Elibariki Baliyanga (Lukole – Kagera).

Wengine ni Joseph Komba (Kisimiri – Arusha), Malugu Maganyala (Feza Boys – Dar es Salaam), Daud Mbukwa (Kisimiri – Arusha), Frank Mwampembe (Lukole – Kagera) na Paschal Nhumba (Kagera).

KUMI BORA MASOMO YA BIASHARA

Dk. Msonde aliwataja watahiniwa kumi bora masomo ya biashara kuwa ni pamoja na Noreen Lyimo (Baobab – Pwani), Astone Ngaeje (Kibaha – Pwani), Doreen Lipambila (Benjamin William Mkapa – Dar es Salaam) na Gift Mwakikusi (Tusiime – Dar es Salaam).

Wengine ni Emmanuel Chila (Alpha – Dar es Salaam), Mery Samwel (Weruweru – Kilimanjaro), Glory Kandonga (Weruweru – Kilimanjaro), Merciana Msechu (Mpanda Girls – Katavi), Getrude Ndongo (St Christina Girls – Tanga) na Athuman William (Umbwe – Kilimanjaro).

MATOKEO YALIYOZUILIWA

Dk. Msonde alisema baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 20 kwa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo.

Alisema watahiniwa hao wamepewa fursa ya kufanya mtihani wa kidato cha sita Mei mwaka 2020 kama watahiniwa wa shule.

MATOKEO YALIYOFUTWA

Katibu huyo mtendaji wa Necta, alisema baraza hilo limefuta matokeo yote ya watahiniwa 14 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani.

Alisema kati ya watahiniwa hao, tisa ni wa shule na watano ni wa kujitegemea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles