27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

“Wasichana niwahanga wa biashara haramu ya binadamu kwa asilimia 90”

Na Nyemo Malecela, Kagera

Imetajwa asilimia 90 ya waathirika wa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu nchini ni wasichana wenye umri kati ya miaka 12 na 19.

Takwimu hiyo imetajwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa wa Serikali na Taasisi binafsi wanaohusika na usimamizi na utekelezaji wa sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu yaliyofanyika Mjini Bukoba mkoani Kagera kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kupambana na kuthibiti biashara hiyo.

Mgeni rasmi katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Tanzania Relief Initiative (TRI) na kudhaminiwa na Serikali ya Canada kupitia Ubalozi wake nchini alikuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Dk. Ntemi Kilekamajenga.

Dk. Ntemi amesema biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu inashika nafasi ya tatu nchini na duniani kwa ukubwa na faida ikitanguliwa na biashara ya dawa za kulevya na biashara ya silaha.

“Kutokana na biashara hii kukua kwa kasi na kushamiri nchini na duniani, serikali ya Canada imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa miaka miwili sasa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa serikali hasa maafisa mbalimbali wa serikali na taasisi za ulinzi na usalama zinazohusika na usimamizi na utekelezaji wa sheria ya kuzuia usafirishaji wa binadamu.

“Tayari mafunzo hayo yameshafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kahama na Kagera,” amesema Dk. Ntemi.

Amesema biashara hiyo ni mwendelezo wa utumwa inayojulikana kama utumwa maomboleo na kuwa biashara hiyo ilianza mwishoni mwa karne ya 18 na kushamiri zaidi mwanzoni mwa karne ya 19 katika bara la Asia na Ulaya.

Amezitaja sababu za kushamiri kwa biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu kuwa ni kuibuka kwa soko la ngono katika nchi mbalimbali duniani, biashara ya viungo vya binadamu kama vile figo kwa watu wenye uwezo kifedha wanaokabiliwa na magonjwa ya kuharibika kwa baadhi ya viungo vyao ambao uwaua na kuchuka viungo wanavyohitaji.

Sababu nyingine ni kuwatumia binadamu hao katika biashara haramu kama ubebaji na uuzaji wa dawa za kulevya, vitendo haramu kama kushiriki kwenye vita na ugaidi wakati watu wenye ulemavu wakitumiwa kuomba misaada barabarani.

Dk. Ntemi aliongeza kuwa binadamu hao wanaosafirishwa uuzwa kama bidhaa nyingine yoyote inayouzika sokoni wanapofikishwa kwenye nchi wanazoahidiwa kupelekwa kwa ajili ya kupatiwa ajira nzuri.

“Mbaya zaidi biashara hii inahusisha unyanyasaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao usababisha mateso makubwa kwa binadamu hao kama vile kupigwa, kubakwa, kunyimwa chakula, kufanyishwa kazi nbila malipo, kunyang’anywa hati zao za kusafiria na kuuzwa kwa hati ya ajira.

“Pia binadamu hawa hufanyishwa kazi bila mapumziko, kulazimishwa kutoa mimba pamoja na kupata mateso mengine yanayosababisha vifo vyao,” amesema Dk. Ntemi.

Dk. Ntemi ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawaongezea uwezo na ufanisi zaidi Mahakimu katika kushughulikia mashitaka yanayohusiana na uharifu huo.

Pia aliiomba serikali ya Canada kuendelea kuisaidia serikali ya Tanzania kufadhili mafunzo hayo ili watendaji wengi zaidi wapate uelewa wa kupambana na biashara hiyo.

“Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani imekuwa ikitajwa kuwa chanzo cha upatikanaji wa watu wanaokwenda kutumikishwa nchi za nje na pia ni mapito ya watu wanaosafirishwa kutoka nchi jirani kwenda nchi nyingine kutumikishwa.

“Wakati huo huo Tanzania ikitajwa pia kuwa majicho ya watu waliosafirishwa kutoka nchi nyingine wanaoletwa nchini kwa lengo la kutumikishwa,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Ieleweke biashara hii ufanywa kwa usiri mkubwa na ufanywa na watu wanaofahamika kwa familia za wahanga au wahanga wenyewe lakini hata baada ya madhara ya biashara hiyo taarifa uwa hazitolewi kwa vyombo vya usalama.

“Biashara hii nchini inafanyika sana katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Kigoma, Kagera, Geita, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Lindi, Mtwara na Zanzibar,” amesema.

Alisema usafirishaji haramu wa binadamu wa ndani ya nchi ni mkubwa zaidi ukilinganisha na watanzania wanaopelekwa nje ya nchi.

“Kwa kipindi cha kuanzia Julai 2020 hadi Desemba 2021, sekretarieti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na wadau wengine walifanikiwa kuokoa wahanga 2,018 wa usafirshwaji haramu wa binadamu kwa upande wa Tanzania Bara kati yao wakiwemo raia kutoka nchi za Burundi, Kenya na nyinginezo.

‘Julai 2020 hadi Juni 2021 kulikuwa na jumla ya kesi saba za usafirishaji haramu wa binadamu zilizokuwa zinaendelea katika mahakama mbalimbali hapa nchini zikihusisha wafanyabiashara 26, na hadi kufikia Desemba 31, 2021 kulikuwa na wafungwa 20 waliokuwa wanatumikia adhabu ya vifungo mbalimbali katika magereza tofauti nchini ambao waligundulika kuwa na hatia ya kukiuka sheria ya kuuza binadamu,” amesema.

Dk. Ntemi alisema hadi sasa serikali imefanya jitihada za kukomesha biashara hiyo kwa kutoa elimu kwa wasimamia sheria ili kuwajengea uwezo wa kupeleza kesi zinazohusiana na biashara hiyo, kuandaa majalada ya kesi pamoja na kutoa hukumu sahihi.

“Pia imeyanyang’anya leseni makampuni yaliyopewa vibali vya kuwatafutia watanzania ajira nje ya nchi, kuongeza juhudi za kuelimisha jamii namna ya kuepuka na kutambua athari za biashara hiyo pamoja,” amesema.

Mkurungenzi wa Taasisi ya Tanzania Relief Initiative (TRI), Edwin Mugabira amesema biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu inashika nafasi ya tatu duniani kwa ukubwa na kwa faida ikitanguliwa na biashara ya dawa za kulevya, biashara ya silaha.

“Wafanyabiashara wa biashara ya usafirishaji wa binadamu ni wanufaika wakubwa kwani wanatengeneza faida ya zaidi ya dola bilioni 150 za Marekani kwa mwaka, na asilimia 90 ya wahanga biashara hii kwa Tanzania ni watoto wa kike wenye umri wa miaka 12 hadi 29,” amesema Mugabira.

Ameongeza kuwa wameamua kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Uhamiaji, Magereza, Polisi, Waendesha Mashtaka, Maafisa Ustawi, Mahakimu mkoani Kagera kwa sababu biashara hiyo imeongezeka na kushamiri sana nchini Tanzania na duniani kwa ujumla ili waweze kukabiliana nayo.

“Lengo la kuendesha mafunzo haya ya siku tano mkoani Kagera ni kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na biashara hiyo kwa kufanya upelelezi mzuri wa namna biashara haramu ya binadamu inavyofanyika, namna ya kuandaa majalada yatakayopelekwa mahakamani na mwisho kesi zitaamriwa vizuri zinapofika kwa hakimu, na ndio sababu kubwa ya Mahakimu kujumuishwa katika mafunzo hayo.

“Hapo awali kesi nyingi za kusafirisha biashara haramu za binadamu zilikuwa zinaharibika katika ngazi ya upelelezi ambapo ilikuwa inasababisha wahanga wa biashara hiyo ambao walistahili kupata ulinzi wa kisheria, wanakosa haki na badala yake wanaishia kunyanyaswa na wanaofanya biashara hiyo,” amesema.

Edwin alisema dhumuni lingine ni kuongeza uelewa kwa jamii kupitia vyombo vya habari ili serikali iweze kuongeza nguvu zaidi kama ilivyoweka nguvu kwenye dawa za kulevya na hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza hivi vitendo vya usafirishaji haramu wa binadamu ambavyo vinaishia kuwanyonya na kuwaumiza wahanga.

“Mafunzo haya yametolewa mkoani Kagera kwa sababu una mipaka mingi inayotokana na kupakana na nchi jirani zaidi ya nne jambo linalosababisha watanzania wengi kutoka Kagera na mikoa jirani kutumikishwa katika nchi hizo jirani lakini pia raia wa nchi hizo kuletwa Tanzania hasa Kagera kwa lengo la kutumikishwa wakati pia mkoa huu kutumika kama njia kwa wafanyabiashara wa biashara hiyo kupitisha binadamu kutoka nchi jirani kwenda nchi nyingine,”alieleza.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, Kamishina Msaidizi, Awadh Juma alisema mapambano dhidi ya biashara hiyo kumekuwepo na opareshini za mara kwa mara kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama hasa Uhamiaji katika maeneo mbalimbali.

“Ukizingatia Mkoa wa Kagera unapakana na nchi jirani hivyo kumekuwepo na wimbi la raia wa nchi hizo kuja Tanzania kwa ajili ya kutafuta kazi. Na katika kukabiliana na hilo kumekuwepo na opareshini za mara kwa mara.

Pia tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii ya kuhakikisha tunakabiliana na janga hilo kwa sababu wapo wanaosafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine lakini pia wapo wanaotoka mkoa wa Kagera kwenda mikoa mingine na nchi jirani kwa ajili ya kutumikishwa katika shughuli zingine ambazo ni kinyume ma sheria za nchi hii,” alisema Awadh.

Alisema kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera wamejidhatiti katika mapambano hayo, kwa uchukuaji wa sheria kwa wote wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo haramu, vile vile utoaji wa elimu kwa umma.

Naye Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Magereza, Samweli Mwakatika alisema wamekuwa na jukumu kubwa la kuhifadhi waarifu ambao wako katika taratibu za mashitaka au wameshahukumiwa.

Wakati naye Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Uhamiaji, Thomas Fussi alisema katika kupambana na biashara hiyo haramu wamekuwa walifanya msako na doria mbalimbali katika maeneo tofauti hasa mipakani na barabarani kupitia vizuizi walivyoviweka.

“Tumekuwa tukikumbana na kesi ya watoto ambao wanakuwa wakisafirishwa pamoja na mama zao ambao ujikuta tukilazimika kuwawaekea uangalizi mzuri ili kunusuru maisha yao kutokana na kupitia mazingira magumu wakati wa kusafirishwa pamoja na unyama wanaotendewa wazazi wao wakati wakitumikishwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles