ABUJA, NIGERIA
OFISI ya Rais wa Nigeria imethibitisha kuwa wanafunzi 82 wa Shule ya Wasichana Chibok waliotekwa nyara na wanamgambo wa Boko Haram mwaka 2014 wameachiwa huru.
Maafisa wanasema hatua hiyo ilitokana na majadiliano ya muda mrefu na ubadilishanaji washukiwa wa Boko Haram, waliokuwa wamezuiliwa na mamlaka za hapa.
Wasichana hao ni miongoni mwa zaidi ya wasichana 270 waliotekwa nyara kutoka shule hiyo ya bweni katika mji wa Chibok, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Wasichana hao wote kwa sasa wanalindwa na jeshi la Nigeria mahali salama karibu na mpaka na Cameroon baada ya kuletwa kwa barabara kutoka maeneo ya vijijini.
Familia nyingi za Chibok zimefurahia taarifa hiyo mpya, lakini wapiganaji hao bado wanawashikilia wanafunzi wengine zaidi ya 100.
Utekaji nyara huo ambao ulifahamika baadaye kama “Wasichana wa Chibok’ ulisababisha kilio kikubwa kote duniani na kampeini za kutaka waachiwe huru ilienea katika mitandao ya jamii.
Hata hivyo, idadi ya washukiwa wa Boko Haram ambao wameachiwa huru na utawala wa Nigeria, bado haijajulikana.