29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wasichana 300 waambukizwa Ukimwi kwa wiki

Na Faraja Masinde – Dar es Salaam

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linalopambana na virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi (Unaids), limesema kundi la vijana wa kike nchini wenye umri kati ya miaka 15 na 24 ndio wamekuwa waathirika wakubwa.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo hapa nchini, Kate Spring wakati wa maadhimisho ya siku ya kupambana na ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya wanawake na wasichana wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Alisema kundi hilo linaongoza pia kwa kupata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ambapo kwa wiki wasichana 300 wanaoambukizwa nchini kote.

“Ni bayana jitihada mbalimbali zinachukuliwa katika kuhakikisha kuwa tunakabiliana na virusi vya Ukimwi.

“Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kwamba kundi la vijana, hususan wasichana wenye umri kati ya miaka 15 na 24 ndio wanaoongoza kwa kuwa na maambukizi mapya, kiwango ambacho ni zaidi ya mara mbili ya maambukizi ya vijana wa kiume.

“Hivyo bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa tunaondoa ubaguzi huu wa wanawake na wasishana,” alisema Kate.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Stella Ikupa, alisema jamii inapaswa kuacha ubaguzi kwa watu wenye virusi vya Ukimwi, huku akibainisha kuwa Serikali itazungumza na viongozi wa dini kuweka utaratibu wa kutoa elimu kwa waumini.

“Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunapiga vita unyanyapaa na ubaguzi huu ambao unaendelea kwenye jamii yetu, jambo ambalo naamini kuwa kama taifa tukishikamana kwa pamoja tunaweza kuondoa kabisa changamoto hii na hata ikiwezekana kumaliza maambukizi.

“Hili linawezekana kwa jamii kujengewa elimu ya mabadiliko na ubaguzi huu ambao umekuwa ukifanyika kwenye jamii, kwani watu wakielimushwa basi ni bayana kwamba tutakuwa tumepiga hatua katika kukabiliana na hali hii.

“Tutawaalekeza viongozi wa dini, ili makanisa na misikiti kuwa na sehemu maalumu za kutoa ushauri kwa waumini wao ambapo pia watatumia wataalamu mbalimbali wa kutoka hospitali kwa jili ya kutoa elimu,” alisema Ikupa.

Alisema bado kumeendelea kuwa na unyanyapaa mahala pa kazi hatua aliyoziagiza taasisi mbalimbali kupitia upya sera zao kwa kuleta usawa na kwamba Ukimwi ni ugonjwa kama ulivyo ugonjwa mwingine.

Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Jumanne Mpango alisema  pamoja na hatua ambazo wamekuwa wakichukua kukabiliana na maambukizi, suala la unyanyapaa bado linarejesha nyuma mapambano hayo.

“Ni bayana kwa namna ambavyo tunaenda, tunaona tumepiga hatua kubwa kwenye kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, suala la elimu ya unyanyapaa na ubaguzi kwa jamii linapaswa kuwa endelevu kwani limekuwa likiturudisha nyuma.

“Kiwango kikubwa unyanyapaa au ubaguzi unapoingia kwenye jamii, imekuwa ikiwafanya watumiaji wa dawa kushindwa kuzitumia vile wanavyotakiwa, hatua ambayo imeleta changamoto kubwa.

“Takwimu zinaonyesha kuwa unyanyapaa na ubaguzi ni asilimia 31 kwa vijijini, huku mijini ikiwa ni asilimia 15 hatua mbayo tunatazamia kama bado elimu ya Ukimwi haijatolewa kikamilifu,” alisema Mpango.

Alisema kundi la wasichana ndio wanaotakiwa kupewa kipaumbele zaidi ikilinganishwa na wanawake kutokana na kuwa na kiwango cha juu cha maambukizi.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (Nacopha), Leticia Mourice alisema  vitendo vya unyanyapaa kwa watu wenye Ukimwi bado vipo hatua ambayo imekuwa ikiwafanya wajisikie vibaya kwani wamekuwa wakiitwa majina ya ajabu.

“Jamii inatakiwa kupewa elimu kwani tumekuwa tukiitwa majina kama wauza vocha za mitandao yote, wakati mwingine tunaambiwa watunza funguo za mochwari na majina mengine yasiyofaa jambo ambalo jamii inapaswa kuelimishwa ili kutokomeza unyanyapaa huu,” alisema Leticia.

Itakumbukwa juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Unaids, Winnie Byanyima, akitoa ujumbe wake kwa dunia, alisema mapambano dhidi ya ugonjwa huo hayatenganishwi na kupigania haki za wanawake na pia mapambano dhidi ya aina zote za ubaguzi.

“Ukimwi unaweza kutokomezwa iwapo tutapambana na ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi, ambavyo vinaendeleza ugonjwa huo na ikiwa tutachochea zaidi uvumbuzi wa kisayansi kushughulikia mahitaji halisi ya wanawake na wasichana na watu wanaoshi na virusi vya Ukimwi.

“Ukimwi umesalia kuwa ugonjwa unaoongoza kwa kuua wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49, ili kutokomeza tunatakiwa kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na kutoa nafasi sawa,” alisema Byanyima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles