27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

WASHTAKIWA KESI YA BILIONEA MSUYA WALIA KORTINI

Na UPENDO MOSHA- MOSHI

MWENENDO wa kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, bilionea Erasto Msuya,  jana uliwaliza washtakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ya mauaji.

Washtakiwa hao walilia baada ya Jamhuri kuwasilisha notisi ya kukata rufaa kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza shauri hilo.

Washtakiwa hao walitoa machozi na kulaumu rufaa iliyokatwa na Jamhuri, dakika chache baada ya Jaji Salma kuahirisha shauri hilo huku baadhi ya ndugu wa marehemu wakifurahishwa na kitendo hicho, jambo lililochangia kurushiana maneno ya kejeli na washtakiwa.

Mmoja wa washtakiwa aliyeshindwa kujizuia na  kububujikwa na machozi mahakamani hapo ni mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa aliyefuatiwa na wenzake, Sadiki Jabir na Said Mohamed.

Washtakiwa hao walichukizwa na uamuzi wa Jamhuri kukatia rufaa uamuzi wa Jaji Salma, aliyekataa ushahidi wa mdomo uliotolewa na shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka, Inspekta Samuel Maimu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Mkoa wa Kilimanjaro

Hata hivyo, baada ya mahakama kutoa uamuzi huo, mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Wakili Majura Magafu, walisema kitendo kinachofanywa na mawakili wa upande wa Jamhuri cha kukata rufaa ni kutumia vibaya sheria na kuwaadhibu washtakiwa.

“Mnachokifanya mawakili wenzangu ni kuwatesa washtakiwa. Ni bora mtafute njia nyingine kesi hii imalizike,” alidai Wakili Magafu

Awali, kabla ya kuwasiliswa kwa rufaa hiyo, akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula, Inspekta Maimu alidai mshitakiwa wa saba, Ally Mjeshi, alikamatwa baada ya kupokea simu yake ya mkononi.

Mahojiano kati ya Wakili Chavula na Inspekta Maimu yalikuwa kama ifuatavyo.

Wakili: Ieleze mahakama tarehe 5 Oktoba mwaka 2013  ulikuwa wapi na nini kilitokea.

Shahidi: Tulikuwa Kigoma na tulimkamata mshitakiwa Ally Mjeshi na nilikuwa na sajenti Atwahi na DC Selemani.

Wakili: Ilikuwaje mkafika Kigoma.

Shahidi: Tulifika Kigoma kwa sababu tulipewa taarifa kwamba mtuhumiwa tunayemtafuta anasomeka kwenye mtandao kwamba yupo Mwanza na baadaye tulipata taarifa kwamba ameondoka na anaelekea Kigoma.

“Kwa hiyo, tarehe tatu Oktoba  tulielekea Kigoma na tarehe tano mwezi huo tulimkamata.

Wakili: Hebu ieleze mahakama mazingira ya ukamataji yalikuwaje.

Shahidi: Tulikutana naye barabarani na baadaye tulipomkamata, alituambia yeye ndiye Ally na ndiye aliyehusika katika mauaji ya Erasto Msuya.

Wakili: Kabla ya kumkamata mlikuwa mnamfahamu?

Shahidi: Kabla ya kumkamata nilikuwa simfahamu

Wakili: Mliwezaje kumkamata mtu msiye mfahamu?

Shahidi: Tulipewa namba yake ya simu na pia tulielekezwa sura yake na rangi yake na jinsi alivyo kwa ujumla.

Wakili: Nani aliwaeleza?

Shahidi: Ni ndugu wa marehemu Erasto Msuya ambaye alimuona kabla ya tukio. Lakini, kabla hatujamkamata, tulipiga simu yake na nilimuona akitoa simu mfukoni akitaka kupokea na hapo ndipo tukajua ni yeye.

Wakili: Shahidi hebu ieleze mahakama kulikuwa na umbali gani kabla ya kumkamata.

Shahidi: Umbali ulikuwa ni mita kama 20

Wakili: Nani aliyemkamata?

Shahidi: Ni mimi, nilimwambia mimi ni polisi na nilikuja kumkamata kutokana na kudaiwa kuhusika katika mauaji ya Msuya.

Wakili: Ieleze mahakama nini kilifuata.

Shahidi: Baada ya kumkamata, tulikwenda naye mpaka kituo cha polisi.

Wakili: Shahidi hebu ieleze mahakama uhusika wa mshitakiwa ulikuwaje.

Shahidi: Mshitakiwa anadai yeye alikwenda mpaka nyumbani kwa marehemu tarehe sita Agosti mwaka 2013  kumwambia kwamba ana madini anayauza.

Wakili: Alienda nyumbani kwake wapi?

Shahidi: Nyumbani kwa marehemu ambako ni katika hoteli yake iliyopo maeneo ya Sakina Arusha.

Baada ya mahojiano hayo, upande wa uetetezi uliweka pingamizi la ushahidi huo wa mdomo kwa madai kuwa haujazingatia sheria na pingamizi hilo lilikubaliwa na Jaji Salma.

Washtakiwa hao walirudishwa mahabusu hadi kesi yao itakaposikilizwa.

Bilionea Msuya aliuawa Julai 7, mwaka 2013 na kesi yake inasikilizwa katika Makahama Kuu, Kanda ya Moshi, ikihusisha washtakiwa saba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles