30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

GWAJIMA AMWACHA JPM AENDELEE NA KAZI

Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hivi sasa anaweza kufunga mdomo ili Rais Dk. John Magufuli aendelee na kazi yake.

Kauli hiyo aliitoa jana katika ofisi za Clouds Media Group alipofika kuwapa pole baaada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia usiku wa Ijumaa iliyopita akiwa ameambatana na askari wenye silaha.

Askofu Gwajima alitoa kauli hiyo akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka kujua kuhusu ugomvi alionao na Makonda.

Alisema hana ugomvi binafsi na Makonda wala Rais Dk. Magufuli bali aliamua kufuatilia vyeti vya kiongozi huyo wa mkoa ili kujua akili yake, baada ya jina lake kutajwa katika orodha ya wanaodaiwa kutumia au kuuza dawa za kulevya.

Askofu Gwajima alisema katika uchunguzi huo aligundua tofauti hiyo ya jina na kuamua kumsaidia Rais Magufuli ili mikono yake iwe yenye nguvu katika kulitengeneza taifa kutokana na tayari kulikuwa na wanafunzi zaidi ya 7,000 waliofukuzwa kwa vyeti feki, wengi wakiwa wanamalizia masomo ya vyuo vikuu pamoja na wafanyakazi serikalini.

“Nikaona haiwezekani mtu mmoja yeye aachwe wakati wengine wa makabila tofauti, Wakristo kwa Waislamu wakifukuzwa. Nikaona kusema ni sasa. Sina ugomvi binafsi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wala Rais, lakini nilisema siwezi kumshtaki Mkuu wa Mkoa mahakamani, lakini nitamwambia Rais ili atoe maamuzi.

“Nafikiri mlimsikia Rais, sasa ni vizuri tumwachie maamuzi sasa, afanye anachofikiri ni chema. Tunaweza kufunga midomo ili Rais aendelee na kazi yake. Lakini ukweli unabaki palepale kwamba haki lazima itendeke kwa kila mtoto wa Tanzania,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema katika orodha ya wanaoshukiwa katika matumizi au uuzaji na usambazaji wa dawa za kulevya, yeye alikuwa kiongozi wa dini pekee na alikwenda kupimwa ulevi wa aina zote pamoja na kuchunguzwa iwapo anatakatisha fedha, lakini hakupatikana na kosa.

Askofu Gwajima alisema baada ya kutangazwa huko hadharani, aliamua kuchunguza kuhusu kiwango cha elimu ya mkuu huyo wa mkoa.

“Baada ya hapo mimi nikaona hivi ni mtu gani mwenye akili timamu, ana kiwango gani cha elimu mwenye uwezo wa kuwataja watu hadharani bila kujali kuwa wana familia, watoto n.k, kwenye kufuatilia hiyo ni akili ya namna gani kupitia academic, ndipo nikaja kugundua alitoka Kolomije akaja Shule ya Msingi Nyanza, akaja Pamba Sekondari, akapata daraja sifuri akajiunga na Nyegezi Fisheries kupata cheti,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema huko kote alifuatilia kujiridhisha ili kupata ukweli na kwamba tangu Kolomije hadi Fisheries kwa mkuu wa chuo aliyemsajili, jina lililoonekana ni la Daud Albert Bashite.

“Elimu ya Makonda ina siri kubwa, naacha aseme mwenyewe, nikisema itashangaza,” alisema Askofu Gwajima.

Kiongozi huyo wa kiroho ambaye alikuwa na walinzi zaidi ya 10 na msafara wa magari sita, alisema alifika ofisi hizo za Clouds kwa kuwa ni mmoja wa waliotajwa katika habari ambayo video yake ilisambazwa mitandaoni.

“Nikaona sio busara watu wamevamiwa nami ni sehemu ya stori halafu nisiende kuwafanyia ‘consultation’. Muendelee na maisha ya kawaida, sio kama watu wanavyolichukulia kisiasa, hili si jambo la kisiasa. ‘There is nothing bad’ na Rais wa Tanzania nampenda, nam-‘support, there is nothing bad’ na Serikali ya Tanzania, tunawapenda na tuna-‘support’, tunapatikana ku-‘support’ Serikali wakati wowote, mahala popote kwa kusudi lenye kujenga na kuifanya Tanzania mpya iwe kweli na kwa hakika,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema anaamini Clouds walitoa ufafanuzi kwa nia njema ya kutaka kuombwa radhi na mhusika na si Serikali.

“Lakini sitaki kuleta hayo yote na hao ‘individual’ kuwa sehemu ya Clouds, nimekuja kuwafariji Clouds na kuwatia moyo na kuwaambia wanaweza kufanya vyema tena na kuendelea,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema hajawahi kujihusisha na siasa, lakini baada ya kutajwa katika sakata hilo na kwakuwa ni kiongozi wa maaskofu 27 chini yake, makanisa 400 hapa nchini na nje ya nchi 440, ilimlazimu kuelezea kanisani ili watu wote ndani na nje ya nchi wapate taarifa.

“Ingekuwa kitu ncha ajabu, umesingiziwa, umepimwa, umelala jela, halafu ukakaa ukanyamaza kimya, watu wataamini kweli umefanya, nilichofanya na nitafanya ni kufafanua. Sitafanya siasa kanisani, sijaitwa kuwa mwanasiasa,” alisema Askofu Gwajima.

Kuhusu suala la mtoto, alisema ana watoto watatu na kwamba binti aliyejitokeza kama alivyowahi kufafanua akiwa kanisani kwake wiki iliyopita, ana upungufu wa akili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles