28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Washiha wamlilia Dk. Magufuli

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kiongozi wa Waislamu Madhehebu ya Shia Ithnasheriya Tanzania, Sheikh Hemed Jalala amemsifu aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa ujasiri wake mkubwa na wa wazi wa kupambana dhidi ya mabeberu ambao waliokuwa wanainyonya nchi.

Kiongozi wa Waislamu Madhehebu ya Shia Ithnasheriya Tanzania, Sheikh Hemed Jalala

Akizungumza katika Khutba Swala ya Ijumaa, Masjid Ghadir, Kigogo Dar es Salaam Sheikh Jalala amesema hayati Dk. Magufuli atakumbukwa kwa kumtanguliza Mungu kwa kila jambo na kila hali.

“Hayati Dk. John Magufuli alitueleza jambo kubwa mno na jambo muhimu kuwa kutambua na kutueleza mbinu za mabeberu, mbinu za wanyonya damu, watu wanaotaka siku zote waishi kwa migongo ya Watanzania na migongo ya Waafrika.

“Kwa kweli kwa tendo lake la kuuzungumza ubeberu na kuwazungumza mabeberu, na kama si wao Waafrika tusingeishi katika mazingira ya umasikini na hali tuliyonayo na wala tusingekuwa na maradhi haya tuliyo nayo yanayotumaliza kila siku,” amesema Sheikh Jalala.

Aidha kiongozi huyo amesema Dk. Magufuli hatosahauliwa katika nyanja ya kudumisha na kuenzi amani, upendo, mshikamano na umoja na kuwataka Watanzania wasikubali kuhatarisha amani, mshikamano na umoja.

“Hayati Dk. John Magufuli alimtanguliza Mungu katika mambo yake yote, katika hotuba zake, katika mikutano yake, awe amekaa awe amesimama, kwa kweli Mungu alimtanguliza mbele. Wakati mwingine huenda viongozi wa dini walirudi nyuma lakini yeye alikuwa mstari wa mbele katika kumuamini Mungu,” amesema Sheikh Jalala.

Sheikh Jalala amewaomba Watanzania kwenye kipindi hiki ambacho ni cha majonzi kutafakari na kuzidi kudumisha umoja, mshikamano na kuenzi amani ya nchi.

“Hayati Dk. Magufuli alikuwa mpenda amani, mpenda umoja, mpenda mshikamano ambayo ndio misingi mikubwa ya Taifa letu la Tanzania. Taifa la Tanzania litapigiwa mifano na wenzetu wanaona gere utulivu tulionao, amani tulionayo na mshikamano tulionao.

“Tusiyakubali maneno ya mtu yeyote yanayoandikwa iwe katika facebook, iwe ni twitter, iwe ni Instagram, iwe ni mahala gani, ambapo yatajaribu kuwatikisa Watanzania na kuwatoa katika mstari wao wa umoja, amani na mshikamano, poleni sana Watanzania, pole sana mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,” amesema Sheikh Jalala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles