Na LEONARD MANG’OHA
MCHANGO wa wataalamu wa kada mbalimbali umekuwa ukitegemewa na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali inayozikabili kwa wakati husika na hata kwa siku za baadaye.
Mathalani, madaktari wamekuwa wakipata heshima kutokana na mchango wao wa adimu unaogusa maisha na hatima ya mwanadamu na viumbe wengine kupitia huduma wanazozitoa kupitia taasisi na vituo mbalimbali.
Walimu wanaheshimiwa kwa kazi yao ya ualimu ambayo wengi wetu tumepita huko na kupata stadi mbalimbali za maisha na maarifa ambayo yanatuwezesha kukabiliana na maisha ya kila siku.
Orodha ni ndefu kuiainisha, lakini itoshe tu kusema kwamba, kila taaluma ina umuhimu wake, hivyo ni vema anayehusika aifanye kwa weledi ili jamii inayomtegemea iweze kufaidika.
Ni katika misingi huo kila mwanataaluma ana umuhimu wake na zaidi thamani yake itatambulika kupitia mchango wake anaoutoa kwa jamii inayomzunguka.
Kupitia makala haya, nitajielekeza moja kwa moja kwenye eneo la uandishi wa habari na mawasiliano ya umma ambalo ndilo kusudio la andiko hili.
Kwa muda mfupi ambao nimekuwa katika taaluma hii ya uandishi wa habari nimeshuhudia mambo kadhaa ambayo naamini yanatweza utu na kuidhalilisha taaluma hii ambayo inatajwa kuwa ni mhimili wa nne wa dola baada ya Bunge, Mahakama na Serikali.
Taaluma hii inatajwa kuwa ni mhimili wa nne usio rasmi kutokana na umuhimu wake na namna unavyoweza kuisaidia jamii na taifa kupiga hatua za maendeleo kwa kasi kama utafanya kazi yake ipasavyo.
Naamini wengi wenu mtakubaliana nami kuhusu mchango wa wanahabari na tasnia nzima ya habari ilivyosaidia kuleta mabadiliko ya kidemokrasia nchini tangu kuanzishwa kwa mfumo unaoruhusu umiliki wa vyombo binafsi ulioanza mwaka 1994.
Ikumbukwe mfumo huu ulianzishwa ikiwa ni miaka miwili tu baada ya kuanza mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992, hivyo ni vyombo hivi vilivyotumiwa na vyama vya upinzani sambamba na chama tawala katika kupenyeza sauti zao kujitangaza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995 na mwaka 2015 alipochaguliwa Dk. John Magufuli.
Katika kipindi chote hicho wanahabari wameendelea kuwa mstari wa mbele kuibua kero mbalimbali katika jamii, ikiwamo ufisadi na kuifumbua macho jamii. Taaluma ya habari ni suala mtambuka zaidi hata ya mihili hiyo mingine.
Taaluma hii inaweza kubadilisha fikra za jamii kwa haraka zaidi kutatua changamoto mbalimbali, ikiwamo migogoro ya aina tofauti, bila kuzusha rabsha yoyote. Hata hivyo, taaluma hiyo inaweza kuwa kinyume cha hayo endapo itatumiwa vibaya na wahusika.
Licha ya wanahabari kutishwa kuumizwa na hata kuuawa, bado wameendelea kupaza sauti kwa mambo magumu yenye kuhatarisha usalama wa maisha yao ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Pamoja na mchango huo mkubwa katika jamii, bado haujaonekana kuwa wa thamani kutokana na watu mbalimbali kutowatendea haki waandishi wa habari, si tu kwa kuwapiga, kuwaumiza na kuharibu mali zao, bali hata kwa kuwatolea kauli zinazotweza utu wao.
Kwa vipindi tofauti nimekuwa nikishuhudia baadhi ya wanaoitwa maofisa habari katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi  maarufu kama ‘wasemaji’ wakitumia lugha zenye maudhi na dharau kwa waandishi.
Si ajabu kuwasikia hawa wasemaji wakisema sitaki au, sijaalika chombo fulani katika mikutano inayoandaliwa na taasisi zao.
Sipingi taasisi kujiwekea utaratibu wa kufanya kazi na vyombo vya habari, bali napinga lugha za kebehi na dharau zinazotolewa na baadhi ya ‘wasemaji’ wake.
Ni jambo lisilopingika kwamba, hivi sasa jiji la Dar es Salaam lina idadi kubwa ya vyombo vya habari na baadhi ya taasisi zina kumbi ndogo ambazo hazitoshi endapo vyombo vyote vilivyopo Dar es Salaam vitaingia kwa pamoja.
Niwasihi wasemaji kwamba, mwandishi ana haki ya kupata habari kutoka taasisi husika, hususan za serikali, kwakuwa zinaendeshwa kwa kodi zao. Kinachotakiwa ni kutumia busara kwa kuwaambia ukweli na ikibidi kuwapatia taarifa kwa kile kinachotakiwa kuzungumzwa na taasisi husika. Lakini baadhi wa wasemaji hawafanyi hivyo, na kusababisha malumbano yasiyokuwa na tija na waandishi.
Kwa mfano katika tukio la hivi karibuni mmoja wa wasemaji wa Chuo Kikuu Huria (OUT) Tawi la Dar es Salaam aliponieleza kuwa hakukialika chombo changu katika tukio aliloliandaa, hivyo hatakuwa na fedha ya kunilipa kutokana na bajeti aliyo nayo. Naheshimu uamuzi wake, lakini hakunitendea haki. Angeniruhusu nifanye kazi yangu halafu fedha zake asinipe.
Japo sikutaka kumwonesha palepale, nilighafilishwa na kauli ile, kwani ilikuwa kauli ya maudhi kwangu, kwa sababu wakati nakwenda pale OUT sikutegemea kulipwa fedha ili kufanya kazi ile. Huo ni mwendelezo wa matukio mengi mengine kama hayo yanayofanywa na wanaoitwa ‘wasemaji’ wa taasisi za umma na binafsi.