21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

APATA UZIO WAN MAJI MARA BAADA YA KUJINGUA

 

HASSAN DAUDI NA MITANDAO                 |             


LICHA ya kwamba inaweza kuonekana kuwa ni simulizi ya kusisimua, ukweli ni kwamba haya ndiyo maisha halisi ya bibiye Cherelle Farrugia, mkazi wa mjini Cradiff, Wales.

Baada ya kujifungua Januari, mwaka huu, mwanamke huyo amejikuta akiishi maisha magumu baada ya kupata uzio wa maji (allergy). Ambapo kila akitoka kuoga hutokwa na vipele mwilini.

Katika mahojiano yake na gazeti la Daily Mail, Cherelle mwenye umri wa miaka 25, anasema hali hiyo ilimjia mara tu alipojifungua mtoto wake wa kike aitwaye Willow.

Akiisimulia hali hiyo, anasema alianza kuona mwili wake ukitoka vipele viliyoambatana na maumivu makali kila alipotoka kuoga, kuosha vyombo au kufua.

“Mwanzoni, nilidhani labda ni aina ya sabuni niliyokuwa natumia, hivyo nikaamua kubadilisha… lakini niligundua kuwa bado tatizo linaendelea,” anasema mwanamke huyo.

Anaongeza: “Nilidhani labda maji yalikuwa ya moto lakini hata nilipoweka yaliyopoa, bado hali ile iliendela.”

Cherelle anasema humchukua dakika tano tu baada ya kugusa maji kuanza kuhisi mabadiliko katika mwili wake.

Anasema: “Mwili huanza kuwasha na hapo ndipo balaa huanza. Baada ya kuwashwa, mwili wote unakuwa na vipele ambayo hudumu kwa dakika 30 hadi 60 kabla ya ngozi kurejea katika hali yake.”

Anakumbuka kuwa wakati alipoiona hali hiyo kwa mara ya kwanza, alichanganyikiwa na mara nyingi aliishia kulia na hivyo kumfanya hata kuanza kupunguza kuoga.

Majanga hayo yalimfanya aende hospitali ambako dakari wa kwanza alishindwa kumtibu kwa sababu hakuwahi kuusikia ugonjwa huo hapo awali.

Anasema ilimchukua takribani miezi mitatu kujua rasmi tatizo linalomsibu.

Alilazimika kuhaha kutafuta tiba katika hospitali nyingine ndipo alipokutana na madaktari bingwa waliobaini kuwa na ugonjwa uitwao kitaalamu Aquagenic Uticaria, ambao kwa mujibu wa maelezo yao, ni wanawake 35 pekee duniani waliokutwa nao baada ya kujifungua.

Hata hivyo, walimwambia kuwa licha ya matibabu mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa, chanzo na tiba havijapatikana, kwa maana kwamba asitarajie kupona kabisa.

Kauli hiyo ilimfanya aumie zaidi kwani alianza kuhisi huenda akaingia katika hatari ya kushindwa hata kunywa maji, balaa ambalo amewahi kusikia limewakumba baadhi ya waliopatwa na hali hiyo.

“Ni kweli naweza kunywa maji kwa sababu sioni madhara yoyote, lakini nimesikia kuwa kuna watu wenye hali kama hii hawawezi kunywa maji kwa kuwa makoo yao yanauma,” anasema.

“Hali hii inaonekana kuwa endelevu, hivyo siku moja huenda nikashindwa hata kunywa maji.”

Hivi sasa, Cherelle amebuni mbinu mpya ya kuishi na hali hiyo akisema anaoga kila siku kama alivyokuwa akifanya zamani, lakini huvaa gauni refu ili asione vipele vinavyomtoka, lengo likiwa ni kujipunguzia huzuni.

“Halafu (baada ya kuoga) natafuta kazi yoyote ambayo itanifanya niwe ‘bize’ kwa saa kadhaa kwa sababu nikivifikiria vipele huwa nakosa raha kabisa.

“Hivyo, mara nyingi huwa nacheza na binti yangu au namchukua mbwa na kwenda naye matembezi ili tu nijiweke bize,” anasema.

Pia, hafichi kuwa amekuwa makini zaidi na hali ya hewa, hasa anapotaka kutoka, akiepuka mvua kumnyeshea.

“Kwa sasa kuna dawa natumia dakika 20 kabla ya kwenda kuoga na inaonekana kunisaidia kwa kiasi fulani, lakini niwe mkweli tu, bado nina tatizo.

Anaongeza kuwa amekuwa akijaribu kuharakisha kujifuta maji pindi anapotoka kuoga kwani amegundua anapochelewa kufanya hivyo, tatizo huwa kubwa zaidi.

Anaamini kitendo cha kujitangaza kinaweza kusaidia kuwapa uelewa wajawazito au wenye tatizo kama analokumbana nalo sasa, hivyo kuharakisha juhudi za kulitafutia ufumbuzi.

Anaeleza namna hali hiyo ilivyombadilisha, akisema awali alitumia muda mrefu kuoga, tofauti na sasa ambapo hutumia dakika tatu tu, ili awahi kuukausha mwili wake ambao kama utabaki na maji, basi vipele na maumivu makali huibuka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles