30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO WENYE ULEMAVU WASIDHARAULIWE, WASOMESHWE

Na CHRISTINA GAULUHANGA


IMEKUWA tabia kwa baadhi ya wazazi au walezi wengi kuwaficha, kuwaua na kushindwa kuwapeleka shule watoto wao wenye ulemavu kwa sababu ya maumbile waliyonayo.

Hali hiyo imechangia kundi hilo kujikuta wakikosa haki yao ya msingi ya kupata elimu na hata matibabu kwa sababu ya waangalizi wao kukata tamaa na kuona kama ni watu wasiofaa kupata huduma hizo muhimu.

Kukithiri kwa tabia hiyo kulichangia kudidimiza taifa jambo ambalo lilisababisha Serikali kuingilia kati ikiwa ni pamoja na kuanzisha shule, vyuo na hata miundombinu sehemu za kazi na kwenye huduma za kijamii kwa ajili ya watu wenye ulemavu ili kuondoa unyanyapaa uliokuwa ukifanyika.

Baada ya Serikali na wadau binafsi kuingilia kati suala hilo na kuanza kuwapeleka watoto wenye ulemavu shule, imeleta hamasa kubwa ndani ya jamii na kuondoa dhana ile kwamba familia kuwa na watoto wa aina hiyo ni mikosi au laana.

Wapo watu wengi wenye ulemavu ambao wazazi wao walithubutu kuwaepeleka shule na hatimaye walifanya maajabu kuanzia shuleni hadi sehemu za kazi.

Miongoni mwa watoto ambao walikuwa na ulemavu ni mapacha marehemu Maria Makwikuti na Consolata waliofariki hivi majuzi, baada ya kusumbuliwa na maradhi ambao walionyesha uwezo mkubwa wa kielimu na ndoto zao kwa bahati mbaya zimezimika ghafla.

Watoto hawa mbali ya kuwa walemavu pia ni yatima walijikuta wakilelewa katika mazingira tofauti na wasamaria wema lakini cha ajabu walifanya vizuri katika masomo yao kuanzia elimu ya awali hadi umauti ulipowakuta wakiwa chuo.

Nafasi waliyofikia watoto hao kielimu inaonesha jinsi jamii ilivyokuwa inawanyima haki watoto wenye ulemavu huku wengine wakithubutu hata kuwaua.

Jamii ichukue kama funzo maisha waliyoishi marehemu hawa kwa kuona watoto wenye ulemavu bado wana nafasi ya kuendelezwa na kupewa haki zao za msingi ikiwamo elimu na matibabu pia.

Dhambi ya kukatisha uhai dhidi ya watoto wenye ulemavu itaendelea kututesa endapo jamii itaendelea kukaidi tabia zao na mila potofu kuwa watoto wa aina hiyo ni laana ndani ya jamii.

Pongezi kwa Serikali na jamii iliyowainua watoto hawa na hatimaye kuweza kufanya vizuri kushinda hata watoto wasio na matatizo.

Pia hata wanafunzi waliosoma na watoto hao nao wamejifunza kitu huenda tuendako tutajenga jamii yenye uelewa kuwa watoto walemavu nao wana haki ya kuishi, kupata elimu na matibabu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles