23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wasanii watoa ya moyoni bajeti ya Sh bilioni 3

Jacob Stephen
Jacob Stephen

NA WAANDISHI WETU,

WAKATI Serikali ikitenga Sh bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya sanaa, ubunifu, utamaduni na michezo zitakazotumika kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Ubunifu, wasanii wa fani mbalimbali wameeleza mitazamo yao kuhusu bajeti hiyo.

Wasanii hao kwa mitazamo yao wamezungumzia namna ambavyo fedha hizo zimeelekezwa kusimamia urasimishaji wa shughuli za sanaa, kusimamia na kudhibiti filamu zitakazoingia sokoni bila kufuata taratibu na kuratibu uendeshaji wa kazi za sanaa nchini.

Muziki wa Reggae

Ras Innocent Nganyagwa, mwanamuziki wa muziki wa reggae ameanza kwa kutoa maoni yake juu ya bajeti hiyo kwa wasanii.

“Fedha zilizotengwa hazitoshi kwa kuwa zimeelekezwa kutekeleza miradi mbalimbali ya sanaa, ubunifu, utamaduni na michezo, hivi ni vitu vingi wakati utamaduni pekee ili ijiendeshe inahitaji fedha za kutosha na pia sanaa kwa ujumla imezungukwa na wizara tano ambazo zote zina miradi yake hivyo kwa fedha hizi ni ngumu kumnufaisha msanii.

“Wasanii hatuhitaji Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Ubunifu bali tunahitaji uboreshwaji wa mazingira ya sanaa kwa kuzingatia sheria zilizopo, kwa Sh bilioni tatu wizara tano zizitazame fedha hizo hatuwezi kunufaika nazo,” alieleza Nganyagwa.

Muziki wa Asili

Mkali wa kughani, Mrisho Mpoto maarufu Mjomba, amesema ni jambo jema kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya wasanii.

“Haijawahi kutokea bunge kutenga bajeti kwa ajili ya wasanii ila sasa bajeti hiyo ifanye kazi kweli na wasanii tujitahidi kutoa kazi nzuri zaidi kwa kutumia vipaumbele na heshima kubwa tuliyopewa katika bajeti,” alisema Mpoto.

Muziki wa Dansi

Mwanamuziki wa dansi, Ally Choki, amempongeza Waziri Nape kwamba kwa kuwa ni msanii anajua uchungu wa sanaa ndiyo maana amehakikisha sanaa imetengewa fedha tofauti na miaka iliyopita,” alisema.

Muziki wa Taarabu

Malkia wa mipasho, Khadija Kopa licha ya kuifurahia bajeti hiyo ameiomba Serikali ielekeze fedha hizo zitumike kweli kwa kuwasaidia wasanii na kuwabana wanaonufaika nazo bila kutolea jasho.

“Wasanii tunakufa masikini, wahindi wanatajirika kupitia  mgongo wetu, Serikali ilikomeshe hili ili wasanii tunufaike na bajeti hiyo kwa vitendo,” alisema Kopa.

Muziki wa Bongo Fleva

Mkali wa rap nchini, Afande Sele, alisema iwe katika utekelezaji badala ya kujaa maneno mengi kuliko vitendo, maana ahadi ni nyingi nchi hii bila vitendo.

“Mimi naomba utekelezaji uweze kubeba nafasi kuliko maneno hewa,” alimaliza Afande Sele.

Naye mkurugenzi wa kundi la Mkubwa na Wanaye, Said Fella, alisema ni kwa mara ya kwanza usimamizi wa kazi za wasanii umewekewa bajeti kikubwa kinachotakiwa uimarishwe ulinzi wa kazi za wasanii ili waweze kujipatia maendeleo kupitia kazi zao.

Stara Thomas alisema mwanzo mzuri kwa kuwa awali hali hiyo haikuwepo.

“Tumeangaliwa kwa jicho la huruma hivyo tujitambue na tuitumia vyema nafasi hii, pia upande wa wezi wa kazi zetu tutashukuru kama litafanyiwa kazi vizuri kwani wasanii wengi wamekuwa wakikata tamaa kutokana na kuibiwa kazi zao.”

Mwigizaji anayewakilisha wasanii wanaokuja juu kwa kasi, Da Zitta, alisema sanaa ni fani inayoingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia kodi lakini suala la kazi kuibiwa ndicho kitu kinachokwamisha wengi,  pia upande wa manunuzi ya kazi zetu mpaka ujisimamie mwenyewe hili tatizo Serikali liliangalie sana na wasanii pia kwa pamoja tuweze kushikana mikono ili tuweze kufika hatua stahiki.

Waigizaji

William Mtitu, mwigizaji na Mkurugenzi wa Kampuni ya 5 Effects, ameiomba Serikali kuhakikisha fedha hizo zinatumika kusaidia wasanii na kazi zao zisielekezwe katika semina na mikutano ya viongozi wa wizara.

“Kama fedha hizo zitaelekezwa kwa wasanii wenyewe zitasaidia na bajeti itakuwa na maana lakini kama zitatumika kwa vikao vyao bajeti haitakuwa na maana kwa wasanii, pia Serikali izuie filamu za nje katika soko la ndani ili filamu za ndani zipate soko la kutosha na kunufaisha wasanii wake,” alisema Mtibu.

Mwigizaji Yobnesh Yusuph ‘Batuli’ amesema: “Mimi naishauri Serikali itumie vizuri fedha ilizozitenga zifanye kazi katika vitengo husika na lengo ni kuboresha sekta ya sanaa ili zilete mabadiliko ya kimaendeleo kwa wasanii,” alieleza.

Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon  Mwakifamba, amesema: “Bajeti ni nzuri tunaomba ikabidhiwe kwa wizara mapema ili iweze kufanyakazi yake isibaki katika makaratsi tu, pia tunamshukuru sana waziri Nape kwa kujituma kwake na kutambua umuhimu wetu kama wasanii katika jamii.

Mzee Chillo amewaomba wasanii watambue kwamba fedha hizo ni kwa ajili ya maendeleo ya wasanii na si kwamba kila msanii atapata za kwake bali zitaleta mwanzo mzuri kuelekea kwenye mafanikio.

Jacob Steven (JB) alisema kazi kubwa iliyobaki ni kwa wasanii kujitambua na kutekeleza majukumu yao kama wasanii.

Wachekeshaji

King Majuto amesema sanaa kutengewa fedha ni jambo la kupongezwa kwa kuwa haijawahi kutokea ila ameomba fedha hizo zifanye kazi kweli isiwe kwa ajili ya kutufurahisha kisha wananufaika wengine.”

Naye Haji Salim maarufu Mboto amefurahishwa na bajeti hiyo na anaipongeza Serikali kwa kuona uwepo wa sanaa nchini, kwani tasnia ya filamu imekosa uangalifu na utetezi.

“Ehe! Tumekumbukwa, jamanii,” alijibu kwa kuchekesha.

Wachora Katuni

Wachoraji Katuni wa Gazeti la Mtanzania, Regis Simon na Said Michael, wameshauri kwamba fedha hizo zinatakiwa ziwe na usimamizi mkubwa ili ziweze kufanikisha mambo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa matamasha ya maonyesho ya kazi za wasanii ndani na nje ya nchi ili yakuze uwezo na sanaa zao.

Naye mchoraji katuni kutoka Maisha Plus, Fransis Bonda, alisema kutojitambua na kutokuwa na elimu ya sanaa kwa wasanii ni tatizo kubwa kwa bajeti hiyo.

“Wachoraji wa Tanzania tumesahaulika wakati sisi ndio tunaoongoza kwa wachoraji katuni kuliko nchi zote za Afrika Mashariki, lakini hata mikopo ya taasisi mbalimbali ikiwemo TMF hatupati inabidi tuangaliwe upya maana michoro ya magazetini na mitandaoni hailipi kwetu,” alimaliza.

Habari hii imeandaliwa na NA JASMINE SEIF (DSJ), BEATRICE KAIZA, GLORY MLAY NA ESTHER GEORGE

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles