26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Wasanii tafakarini mnayoipelekea jamii

wasanii

Na JOSEPH SHALUWA

HAITASHANGAZA nikisema kuwa sanaa ni sauti kuu katika jamii. Kupitia wasanii jamii inaweza kufikiwa kwa wakati mmoja. Uhitaji wa wasanii kwenye mambo mbalimbali inaweza kuwa kielelezo ya ninachokiongelea hapa.

Ni wapi umeona kuna shughuli iliyokosa muziki? Ulihudhuria mahafali gani yakakosa wasanii wa maigizo, ngonjera, kwaya, ngoma za asili, muziki na sanaa nyingine?

Umeona wapi harusi ikakosa burudani ya muziki? Hadi kwenye mazishi kuna muziki. Hii inamaanisha kuwa, wasanii kupitia sanaa zao mbalimbali wana kazi kubwa ya kuwasilisha ujumbe kwa jamii.

Mtu asiyejulikana anaweza kufanya kihoja fulani na kisiripotiwe kwenye vyombo vya habari, lakini akiibuka mfano msanii kama Vanessa Mdee na kufanya tukio hilohilo linakuwa habari.

Yote hiyo ni kutokana na kujulikana kwa wasanii husika. Lakini tatizo ni kwamba, wasanii wetu badala ya kupeleka mambo yenye kufaa kwa jamii, wanaharibu.

Ni kweli siyo wote wanafanya hivyo, lakini kiukweli ni kwamba jamii na hasa vijana wamekuwa wakiiga kila kitu kutoka kwa wasanii. Wasanii wanaofanya mambo hayo, nao huiga kutoka kwa wenzao wa Magharibi.

Kuna mambo mengi yasiyofaa ambayo yanafanywa na baadhi ya wasanii wetu. Wapo wanaotumia madawa ya kulevya, kuvaa mavazi yasiyo na staha, kushiriki uhusiano wa jinsi moja nk, yote hayo ni uharibifu wa maadili kwa jamii yetu.

Pengine wasanii wetu hawaelewi hilo vizuri lakini ukweli ni kwamba wanawasha bomu hatari kwa jamii ambalo linakaribia kulipuka.

Niwaleze tu kwamba, si kila kinachofanywa na wasanii wa nje ni kizuri. Ni vyema kuchuja. Bahati nzuri elimu ya maadili na desturi zetu Watanzania zinaeleza wazi namna tunavyopaswa kuishi kwa heshima.

Mfano msanii wa kiume kuvaa hereni, kutoboa pua, kuvaa suruali chini ya makalio na mengine kama hayo; anayefanya hivyo anakuwa amedhamiria nini?

Siyo dhambi kuiga, lakini basi ni vizuri kuchagua cha kuiga. Achaneni na mambo ya kimagharibi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles