NA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM
WASAFIRI 1,526 walioingia nchini wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DCR) wamechunguzwa afya zao dhidi ya maambukizi ya Ebola au la.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipofungua semina ya kuwajengea uwelewa juu ya ugonjwa huo.
Alisema wasafiri hao ni wale walioingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Uwanja wa Ndege Songwe, mipaka ya Rusumo, Mtukula na Kabanga.
Alisema taarifa zinaonyesha wasafiri wote waliochunguzwa hawakukutwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
“Mlipuko wa sasa umetokwa eneo la Kivu Kaskazini kuna muingiliano mkubwa wa watu kutoka Kongo kwenda Uganda, Rwanda na Tanzania.
“WHO imeeleza tupo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi” alisema.
Alisema takwimu zinaeleza tangu Agosti Mosi, mwaka huu ugonjwa huo uliporipotiwa kuwapo DRC hadi sasa watu 116 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo na 77 kati yao wamefariki dunia.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini lakini endapo utaripotiwa ni namna gani wamejiandaa usisambae.
“Nimeangalia madhara ya Ebola ilipotokea Afrika Magharibi (2013-16) biashara ilifungwa, mipaka na hata safari za ndege, jarida la The Times walitoa ripoti wakaeleza madhara ya Ebola yanagusa hadi uchumi wa nchi.
“Ugonjwa huu wa Ebola kwa kweli ni ugonjwa hatari, wanasema madhara ya uchumi juu ya Ebola yangeuwa watu wengi zaidi kuliko ugonjwa wenyewe.