27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Warioba: Umma utamhukumu Nape Nnauye

Jaji Joseph Warioba
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

SHABANI MATUTU NA ELIZABETH MJATTA, DAR ES SALAAM

KAULI iliyotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kwamba wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wanatumia mchakato wa Katiba kama mradi binafsi wa kujinufaisha, ni wazi imeonekana kumkera Jaji Joseph Warioba, ambaye sasa ametamka bayana kuwa mwanasiasa huyo anasubiri kuhukumiwa na nguvu ya umma.

Jana vyombo vya habari vilimkariri Nape akimshutumu aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba pamoja na wajumbe wake kwa kuutumia mchakato wa Katiba kujitafutia maisha, historia na heshima mbele ya jamii, huku wakitoa lugha zisizo na staha, chuki na kejeli dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kuhusu shutuma hizo, Jaji Warioba alisema kuwa maneno aliyoyatoa Nape dhidi yake na waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yatahukumiwa na wananchi ambao wengi wao walitazama mdahalo huo.

“Mdahalo wa Jumatatu nimeelezwa kwamba ulitazamwa na wananchi wengi, hivyo basi kama kweli Nape anachokisema kuwa tulitumia lugha zisizokuwa na staha, chuki, dharau na kejeli dhidi ya Rais Jakaya Kikwete kwenye mdahalo huo ni za kweli, wao ndio watakuwa waamuzi,” alisema Warioba.

Alisema baada ya kuona taarifa hiyo iliyotolewa na Nape na kusomwa mbele ya waandishi wa habari, kwa sasa anafanya kazi ya kutafakari hatua atakazozichukua.

“Nimefanikiwa kuona ‘statement’ iliyotolewa na Nape juzi, hivyo kwa sasa naitafakari na iwapo nitaona kama kuna ulazima wa kuzungumzia nitafanya hivyo,” alisema Warioba.

BUTIKU

Mjumbe mwingine aliyeshiriki katika mdahalo huo wa Jumatatu uliolalamikiwa na CCM ni kada wao mkongwe wa chama hicho, Joseph Butiku. Alipotafutwa na MTANZANIA Jumamosi kuelezea kauli hiyo iliyotolewa dhidi yao, alisema kwa sasa hana la kuzungumza.

Butiku, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alipoulizwa zaidi, alisisitiza kwa kifupi kwamba “Sina maneno”.

PROFESA LIPUMBA

Akizungumzia kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alipinga kauli hiyo ya Nape aliyodai kuwa ina nia ya kuwaziba mdomo Jaji Warioba na wajumbe wake ili wasitoe ufafanuzi kwa masuala yanayopotoshwa kuhusu Rasimu ya Katiba.

Profesa Lipumba alisema amesikitishwa na kauli ya Nape ya kuwalalamikia wajumbe hao kutumia lugha za matusi katika mdahalo huo wa Jumatatu, ambao alisema kimsingi ulikuwa na nia ya kuongeza uelewa wa wananchi katika masuala yaliyokuwa yakipotoshwa katika jambo hilo nyeti la Katiba.

“Sikusikia tusi likitamkwa wala kejeli iliyotolewa na wajumbe walioshiriki kutoa mada kwenye mdahalo huo zaidi ya kurekebisha masuala yaliyopotoshwa, kwa mfano, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alipopotosha kwamba Tume hiyo imepeleka muswada mwingine Ikulu, wakati haikuwa kweli,” alisema.

Prof. Lipumba aliituhumu CCM kuwa na kawaida ya kutafuta njia za kubana hoja nzito bila kujali kama zimo ndani ya rasimu iliyopendekezwa na wananchi, wakitaka Katiba isimamie uwazi, uwajibikaji na uadilifu.

“Kwa hilo la kutojali na kuheshimu maoni ya wananchi, inaonyesha wazi kabisa hawana nia ya kuheshimu uhuru wa maoni ambao ni haki ya kila Mtanzania kikatiba,” alisema.

Aliongeza kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wanaowajibu wa kuzungumzia Katiba, kwa sababu ndio wanaojua walichokiandika na sababu yake kwenye rasimu hiyo na hata inapojitokeza Watanzania wakahitilafiana au rasimu kuchezewa, waweze kutoa tafsiri.

“Linalonisikitisha ni kwamba, Serikali tayari imeshafunga hata ile tovuti iliyokuwa na randama ya maoni ya mchakato wa rasimu hiyo, imefutwa,” alisema.

Profesa Kabudi

Kwa upande wake, Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema kwa sasa anatumia hekima kwa kutozungumzia kwa upana madai hayo ya Nape.

“Sitaki tena kuingia huko kwenye majibizano, tuyaache kwanza, kwani wakati mwingine unatakiwa kutumia busara na hekima kutafakari mambo, hivyo basi leo ngoja nitumie zaidi hekima,” alisema Profesa Kabudi.

Juzi Profesa Kabudi, alipozungumza na MTANZANIA kuhusu njama zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM na Serikali kuwanyima haki ya kujadili rasimu Watanzania ambao wako nje ya Bunge, alisema suala hilo litakuwa linakwenda kinyume cha Katiba ambayo inampatia kila Mtanzania uhuru wa kutoa maoni na mawazo.

“Kama wamesema hivyo, wakumbuke kuwa mchakato wa Katiba ni safari, na safari yoyote ina mabonde, milima, ina kona na nyingine ni kali sana na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu sana, na haijengwi kwa kuzuia maoni ambayo unatofautiana nayo,” alisema.

Profesa Kabudi aliongeza kuwa mjadala wa Katiba uruhusiwe kujadiliwa ili taifa liwe katika mjadala ambao watu wake hawatashupaa.

“Na ndiyo maana nimewahi kusema hata kwenye semina niliyoitwa kwenye Bunge wakati wa kujadili muswada wa sheria mara ya kwanza, niliwaambia kwamba mpumbavu hushupaa, lakini mjinga huduwaa,” alisema.

Alitoa wito kwa Watanzania kujadili Katiba kwa nia ya kuitafutia mwafaka na maelewano, huku kukiwa na tahadhari kubwa kutokana na ukweli kwamba nchi inapita katika kipindi kigumu, inahitaji kila mwananchi awe makini.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Nashauri vyombo vya usalama (polisi) vitoe tahadhari kwa wanaoshupalia na kuwaaasa wananchi kufanya vurugu na umwagaji damu kwamba watakuwa suspect namba wani!!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles