29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Sakata la SIKIKA latua mezani kwa Ghasia

Hawa Ghasia
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia

Na Khamis Mkotya, Dar es Salaam

SAKATA la kufungiwa kwa Shirika la SIKIKA wilayani Kondoa limechukua sura mpya baada ya shirika hilo kumwandikia barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia.

Barua hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Irenei Kiria, ilipelekwa ofisini kwa Ghasia Jumatano zikiwa zimepita wiki mbili tangu shirika hilo kufungiwa wilayani humo.

Katika barua hiyo, Sikika imemuomba Ghasia kuingilia kati suala hilo ili hatimaye shirika hilo liweze kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Kondoa.

Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo lilipiga marufuku shughuli za Sikika wilayani humo kwa madai shirika hilo limewadhalilisha madiwani wake kwa kuwatuhumu hawajui kusoma, hali iliyofanya washindwe kuisimamia halmashauri hiyo.

“Sikika imesikitishwa na taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ya kusitisha shughuli zake katika wilaya hiyo kupitia barua yenye kumbukumbu namba KDC/LGC/M/3VOL.11/7 ya tarehe 31/07/2014.

“Kwa mujibu wa barua hiyo, uamuzi huo ulitolewa katika mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika Julai 26, mwaka huu baada ya kuituhumu Sikika kwamba imesema madiwani hawajui kusoma.

“Awali tuhuma hizo ziliwasilishwa kwa Sikika Julai 9, 2014, tulikanusha taarifa hizo na kuomba tupewe uthibitisho wa tuhuma hizo ili tuzifanyie kazi, lakini hatukuwahi kupewa ushahidi wowote zaidi ya kulazimishwa kwamba ni tuhuma za kweli.

“Baraza la madiwani nalo limefanya uamuzi bila kuchunguza ukweli wa tuhuma zenyewe. Hivyo tunakuomba uingilie kati ili haki itendeke kwa manufaa ya wananchi wa Kondoa.

“Hata hivyo, kwa kuwa taarifa hizo zilianza kutolewa na halmashauri kupitia vyombo vya habari, katika hatua za awali bodi yetu imelazimika kutoa maelezo kwa umma kupitia vyombo vya habari ambayo tumeiambatanisha.

“Pamoja na barua hii, tunaambatanisha nyaraka nyingine zilizotumika kwa mawasiliano kati ya Sikika na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa,” ilieleza barua hiyo.

Jana gazeti moja la kila siku (si Mtanzania), liliripoti kauli ya Ghasia akisema yupo tayari kuunda timu itakayokwenda Kondoa kuchunguza utata na sakata zima lililojitokeza kutokana na shirika hilo kufungiwa.

Hata hivyo, katika taarifa hiyo, Ghasia alisema hajapokea malalamiko rasmi kutoka kwa shirika hilo linalofuatilia uwajibikaji katika sekta ya afya nchini.

Tayari Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD-Coalition), umetoa tamko la kulaani kufungiwa kufanya kazi kwa muda usiojulikana kwa shirika hilo wilayani Kondoa.

Mtandao huo unaohusisha mashirika zaidi ya 100 yanayotetea haki za binadamu yamepinga uamuzi uliofanywa na baraza la madiwani la halmashauri hiyo dhidi ya shirika hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles