Na HAFIDH KIDO -
MWANAHISTORIA Mohammed Said, katika kitabu chake cha “Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes” sura ya tisa ukurasa wa 260, anazungumza mkutano wa Tabora mwaka 1958 uliokuwa chachu ya kupatikana Uhuru wa Tanganyika.
Mkutano huu ulilenga kuwashawishi wananchi waliokuwa chini ya makucha ya kikoloni kukubali kushiriki uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria (Bunge), kwasababu kulikuwa na mvutano ndani ya chama cha TANU (Tanganyika African National Union), baadhi walitaka kususia uchaguzi na wengine walitaka kushiriki, wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa TANU.
Sina haja ya kuuzungumzia mkutano huu wa Tabora, uliotoa azimio lililopewa jina la Uamuzi wa Busara, inadaiwa Mwalimu Nyerere alitumia hekima nyingi na busara kuwashawishi wajumbe wa mkutano mkuu wa chama uliofanyika Tabora katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Parish Hall, kwa siku sita kuanza Januari 21 hadi 26, 1958, lengo ni kunusuru chama kugawanyika.
Kumbuka wanachama wa TANU wakati wakipitia kipindi kigumu Waingereza walishaandaa mazingira ya kuwakabidhi nchi, maana yake mivutano ya aina ile iliwaonyesha kuwa walikuwa hawajakomaa kupewa nchi.
Mwalimu Nyerere aliwatumia wazee wa Tanga na baadhi ya maeneo ya nchi ili mambo yaende sawa.
Wapinzani wa kura tatu walikuwa na sababu za msingi kususia uchaguzi ule, kwa kuwa Waingereza waliweka masharti magumu kwa Waafrika. Kura zenyewe zilikuwa zikiendeshwa kwa misingi ya utaifa.
Kulikuwa na viti vitatu: Kimoja kwa ajili ya wazungu, kingine Waasia na Waafrika. Hata hivyo, Mwafrika aliwekewa masharti magumu kushiriki uchaguzi huo, alitakiwa awe na kipato kisichopungua Pauni 400 za Kiingereza kwa mwaka. Awe na elimu ya kuanzia darasa la 12 na awe ameajiriwa katika kazi maalumu.
Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuwashawishi wanachama wa TANU kushiriki uchaguzi huo wa kinyonyaji kwa lengo moja tu, kuwaonyesha Waingereza kuwa wanaweza.
Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU, Zuberi Mtemvu, alijiuzulu wadhifa wake baada ya kuona kambi yake imeshindwa kushawishi kugomea uchaguzi, hivyo akaanzisha chama chake, African National Congress (ANC). Tangu siku hiyo ikawa mtu msaliti anaitwa Congress.
Nimejaribu kueleza hayo kwa muhtasari, nikiunganisha matukio yanayoendelea nchini, hasa hili la vyama vya upinzani kususia chaguzi.
Awali kilianza Chama cha Wananchi (CUF), kiliposusia uchaguzi wa marejeo mwaka 2015 visiwani Zanzibar, vikafuatiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia chaguzi mbili za udiwani pamoja na uchaguzi mdogo wa wabunge unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani.
Kinachoshangaza hata Chama cha ACT-Wazalendo ambacho kilikuwa mbali na taratibu hizi, nacho kimeingia katika mkumbo huo. Si ishara nzuri kwa vyama vinavyojinasibisha na kutetea wanyonge.
Katika hali ya kawaida wanaoumia ni Watanzania wanyonge ambao walitumia nguvu nyingi kuwaondoa viongozi ving’ang’anizi katika maeneo yao ambao walikuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Uchaguzi wa marudio unafanyika, kinachotokea ni kususia, tafsiri ya kususia ni moja; CCM watarudisha kata zote walizopoteza na majimbo yote waliyopoteza, ikiwamo la Kinondoni na lile alilojiuzulu Lazaro Nyalandu, mkoani Singida.
Januari 28, 2016, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Buguruni, jijini Dar es Salaam, alitoa sababu za kususia uchaguzi wa marejeo uliofanyika Machi 20, 2016 Visiwani Zanzibar kuwa ni kutokana na sababu zilizofanya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ZEC, Jecha Salum Jecha, alitangaza kufuta matokeo baada ya kutokea kile alichokiita kuvurugwa kwa taratibu za uchaguzi na wanachama wa CUF.
Pamoja na malalamiko hayo, katika uchaguzi ule CUF walifanya kosa kubwa la kimkakati, kwanza waliwaachia CCM kuutawala uchaguzi na kufanya walichotaka. Pili; waliwadhulumu wawakilishi ambao tayari walikuwa na mvuto katika maeneo yao, hasa Pemba.
Hadi sasa ndani ya CUF hali si shwari, kwa sababu wapo wawakilishi waliobaki na hati zao za ushindi vyumbani, huku wakilia ukata, hali ngumu ya maisha kwa sababu tu CUF imeamua kukaa nje ya siasa kwa miaka mitano.
Ukiangalia Baraza la Wawakilishi limejaa CCM watupu na baadhi ya wajumbe walioteuliwa na Rais Dk. Ali Mohammed Shein kutoka katika vyama vya kina Hamad Rashid Mohammed na wengine mbavyo hata havikufikiriwa kuingia katika Baraza la Wawakilishi.
Kikatiba kupiga kura ni haki ya mwananchi, lakini kuibiwa, kuiba au kulinda kura ni haki ya viongozi wa chama. Haiwezekani eti vyama kama CUF, NCCR Mageuzi na Chadema vilivyoshiriki uchaguzi kwa miaka yote viogope kuibiwa kura.
Bora ACT-Wazalendo kutokana na uchanga wake labda kinaamua kufuata upepo, siwezi kukilaumu sana.
Lipo suala jingine ambalo viongozi wa Ukawa na ACT-Wazalendo wanapasa kueleza, lakini si hofu ya kuibiwa kura. Huenda wakajinasibu kuwa hizi ni mbinu za kuiondoa CCM madarakani ifikapo mwaka 2020, lakini wafahamu kuwa, kwa kuwaruhusu CCM kushika kata nyingi zaidi, wasitegemee chochote kizuri katika mwaka wa uchaguzi ambacho huenda hakijulikani au kinajulikana, lakini kinapuuzwa na wapinzani. Ukweli ni kuwa, kura nyingi zinapatikana vijijini, watu wa mjini ni waoga kupiga kura, pia ni wagumu kuwashawishi kuliko watu wa vijijini.
Huko vijijini wazee wengi bado wana imani na CCM, ingawa malalamiko ya hali duni ya maisha yako palepale.
Kwa hali hiyo, vyama vya upinzani wanapaswa kutumia chaguzi hizi za kata na majimbo kuzungumza na wananchi kuwaeleza mbadala wa CCM yupo na akiingia madarakani atakuwa tayari kubadili hali ya uchumi. Kuleta tija katika kilimo, kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, ikiwamo dawa za kuua visumbufu na mbolea za kupandia na kukuzia, lakini pia uhakika wa masoko baada ya kuvuna.
Miongoni mwa mikakati waliyonayo ACT-Wazalendo ni kuwasaidia wananchi katika suala la kilimo, lakini hawawezi kufanya hili hivi hivi, lazima watengeneze mazingira ya kutangaza sera yao hii kupitia majukwaa ya kisiasa.
Ushauri wangu, kwa kuwa utawala wa sasa umekataza kufanya siasa, vyama vya upinzani vingetumia mwanya huu wa chaguzi za marudio kueleza yale waliyotaka kuyaeleza baada ya uchaguzi mkuu kukamilika. Hata kama kura zao zitaibiwa wananchi ni mashahidi, watajua nani alikuwa na sera nzuri na nani alikuwa na pumba, haya watayajua wakati wa kampeni.
Kususia ni kuwanyima haki wananchi, haki ya kusikiliza sera nzuri zitakazowasaidia kuondoa changamoto za kimaisha maeneo ya vijijini. Maeneo ya mjini wananchi hawategemei vyama vya siasa kutatua kero zao, kwa sababu kila kitu kinafanyika kwa ustadi ili kuweka mazingira mazuri ya uzalishaji mali.
Hivyo, busara ya uchaguzi wa kura tatu uliomsaidia Mwalimu Julius Nyerere kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mzalendo na baadaye kukabidhiwa nchi mwaka 1961, busara hiyo hiyo itumiwe na viongozi wa upinzani kuondoa matatizo ya wananchi, kama ambavyo mwaka 1958 TANU kiliitwa chama cha upinzani na kikafanikiwa.