24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

‘WAONDOENI WANANCHI NDANI YA HIFADHI’

Na Mwandishi Wetu-Arusha


WAZIRI  wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuhakikishaa wananchi wote waliolima ndani ya eneo hilo kinyume cha sheria wanaondoa mazao yao pamoja na kusitisha  shughuli zozote za kibinadamu.

Waziri Maghembe, alitoa agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na hifadhi hiyo ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.

“Naagiza, kuanzia leo ni marufuku mtu yeyote kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari hapa, atakayeonekana piga pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani ya hifadhi tukae kimya, ni lazima tuchukue hatua.

“Watangaziwe na wapewe muda wa kuondoa mazao yao, ndani ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka,”  alisema Profesa Maghembe.

Naye Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga alisema eneo hilo ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41, limekuwa na mgogoro tangu mwaka 1990, baada wananchi wa Kijiji cha Olkung’wado kuvamia eneo hilo huku wakitoa hoja kadhaa ikiwemo madai kuwa shamba hilo ni maeneo yao ya asili waliyokuwa wakimiliki tangu zamani.

Alisema hoja nyingine wanazozitoa ni kuwa walipewa mashamba hayo na Serikali wakati wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka 1975 na 1976, hoja nyingine ni kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato wakati wa ugawaji wa mashamba hayo na kwamba TANAPA pia haina hati miliki ya mashamba hayo.

Alisema hoja zote hizo zilikinzana na ukweli kuwa shamba hilo lilimilikishwa TANAPA tangu mwaka 1980, baada ya kutolewa tangazo kwa wadau wanaoweza kuliendeleza kutokana na mwekezaji wa awali, James Preston Mallory kushindwa kuliendeleza na hivyo kufutiwa hati miliki na  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1979.

“Wadau mbalimbali waliomba umiliki, ikiwamo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Halmashauri ya Kijiji cha Olkung’wado, Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa Arusha, iliishauri Serikali mashamba hayo yamilikiwe na mamlaka… tukaandikiwa barua rasmi ya kukubaliwa kupewa shamba,” alisema Ndaga.

Alisema shirika lilinunua eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 966 kwa lengo la kupanua Hifadhi ya Taifa ya Arusha, ambapo baada kupewa iliagizwa kulipa fidia ya mali zilizokuwapo mwaka 1983.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dk. Alan Kijazi alisema wataanza kutekeleza agizo mara moja moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles