26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Waombwa kutoa vifaa vya kujikinga corona kwa wenye mahitaji maalumu

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

JAMII imetakiwa kuwasaidia wenye matatizo mbalimbali kwa kuwawezesha vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 ambao unasababishwa na virusi vya corona.

Diwani wa Kata ya Ukonga, Jumaa Mwipopo, akizungumza wakati akipokea msaada wa barakoa kwa watu wenye mahitaji maalumu, alisema jamii inatambua adha ya ugonjwa huo, hivyo ni vema kuwalinda watu wenye mahitaji maalumu.

Alisema kata hiyo ina wazee wengi wasiojiweza na wajane, hivyo wanahitaji misaada ya hali na mali ili waweze kujikimu kimaisha na kuwakinga wasipate maambukizo ya ugonjwa huo.

“Natumia fursa hii kumshukuru Neema Edward ambaye ni mlemavu lakini ameguswa na wengine wenye shida na kuamua kutoa alichonacho kama sadaka yake kwa Mungu,” alisema Mwipopo.

Pia aliomba Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kufikiria kuongeza muda wa riba kwa vikundi vya wajasiriamali vya kina mama walemavu kwakuwa kipindi hiki cha Covid-19 wengi hawajafanya biashara.

Akikabidhi msaada huo, Neema alisema ameguswa na hali ya kimaisha waliyonayo wengine, hivyo kupitia ofisi yake ya  Mkwelele Wellness Foundation, ameamua kutengeneza barakoa na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu.

Alisema anatambua gharama za kununua barakoa, hivyo ana imani kidogo alichokitoa kitasaidia kuokoa maisha ya watu endapo hawataambukizwa na maradhi mbalimbali.

 “Natambua adha ambazo wanazipata watu wenye ulemavu pamoja na wazee, kwakuwa barakoa zimekuwa zikiuzwa kwa gharama kubwa, hivyo kwa nafasi yangu nimeona kidogo nilichonacho kitasaidia kupunguza matatizo waliyonayo,” alisema Neema.

Aliwataka wajasiriamali wengine na taasisi mbalimbali kuendelea kuliwezesha kundi hilo ambalo wengi wao hawana msaada kutoka kwenye familia zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles