23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wanyama wanavyosubiri kifo kwa kukosa chakula

Na ANDREW MSECHU-dar es salaam

WAKATI zuio la kuuza wanyama hai nje ya nchi likiwa limetimiza miaka mitatu sasa, muda huo umekuwa janga kwa wanyama hao ambao wakati Serikali ikitoa katazo hilo, walikuwa wameshatolewa porini tayari kusafirishwa.

Wengi wa wanyama hao wanaelezwa kuwa wamekufa njaa kutokana na kile wenye mashamba ya kuwatunza, wanachosema ni kuelemewa na gharama ya malisho.

Wapo waliobadili mashamba yao kuwa bustani za wanyama (zoo) ili kupata kiingingilio kwa watu wanaotaka kuwaangalia, lakini nao wanadai hali ni mbaya na kiingilio hakitoshi kugharamia malisho.

Mkurugenzi wa Bahari Zoo, Willy Kusaga, anasema mwanzo biashara yake kuu ilikuwa kuuza nje wanyama hai, lakini baada ya zuio la Serikali alibadilisha shamba lake kuwa bustani ya wanyama.

Alisema kwa sasa hana uwezo wa kuendelea kuwatunza wanyama hao na hawezi kuwarudisha porini katika mazingira yao ya asili.

 “Nimekuwa nikiwatunza wanyama hawa tangu Serikali ilipotangaza kusitisha biashara ya wanyama nje ya nchi mwaka 2016, wanyama hawa ambao tayari wako kwenye bustani hii wanaendelea kuzaana na siwezi tena kuwasafirisha.

“Nimekuwa nikijitahidi sana kuwalisha kwa fedha yangu ya mfukoni, nimejikuta kwenye madeni makubwa kutokana na matunzo yao, gharama ya kuwatunza ni kubwa sana na sasa naona pumzi inakata,” alisema Kusaga.

Alisema mlo mmoja wa simba mmoja ni kilo 20 kwa wiki ambazo ni sawa na Sh 140,000.

“Kwa hiyo simba wawili wanatumia Sh 280,000 kwa wiki na kwa mwezi wanatumia Sh milioni 1.12.

“Ukiangalia gharama hiyo kwa mwaka inakuwa Sh milioni 13.4 kwa simba tu na kwa sasa nimeshawatunza karibu miaka minne,” alisema.

Kusaga alisema kwa wanyama wanaokula nyasi, hulishwa katika eneo la bustani hiyo na inapotokea upungufu hununua nyasi maeneo mengine.

Alisema kwa mujibu wa taratibu, walishaingia gharama ya vibali vya kuwakamata wanyama hao.

Kusaga alisema hakuna njia ya kipato zaidi ya kuwauza nje wanyama hao, kwa kuwa Watanzania wenye mwamko wa kwenda katika bustani ya wanyama na kulipa kiingilio ni wachache.

“Ukweli ni kwamba mnyama aliyezaliwa kwenye bustani hakuna namna ya kumrudisha porini. Wanapoendelea kuzaliana idadi yao inakuwa kubwa, tunalazimika kuwatunza kwa gharama zetu. Hakuna tena biashara, tumejaribu kuzungumza na Serikali, lakini bado hatujafanikiwa.

“Niombe Serikali wajaribu kuangalia namna ya kutusaidia, wakutane na sisi tuwaeleze hali halisi tunayokabiliana nayo,” alisema.

Alisema awali taratibu zilikuwa hazipo vizuri na wafanyabiashara walikuwa hawazifuati kwa sababu ilionekana kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kulikuwa na leseni zaidi ya 300, huku nyingine zilikuwa za mfukoni, na waliokuwa wakifuata taratibu hawakuzidi 10.

Kusaga alisema kwa sasa wanaendelea kupata hasara kwa kuwa wana madeni benki na wamejikuta wakitumia fedha ambazo walilipwa na wateja wao kwa kuwauzia wanyama.

“Siku zote tulijua kuwa itafikia muda Serikali itaruhusu biashara iendele kwa sisi wa ndani kwa sababu maelekezo ya awali ilikuwa ni zuio kusafirisha wanyama kutoka kwenye hifadhi, siyo hawa walioko kwenye mashamba.

“Sasa tulikuwa na wateja wetu ambao walishatuma fedha kununua wanyama, tuliwaambia wasubiri, mwisho wake kadiri muda unavyokwenda tukajikuta tumeshatumia hata fedha zao, sasa ni madeni kila kona,” alisema.

Alieleza kuuza wanyama wanaozaliwa katika bustani ya wanyama ndiyo njia ya kurudisha gharama za matunzo kwa sababu hawana namna nyingine ya kuendelea kuwatunza.

 “Tunaomba waje wajionee, hata kama viongozi wakuu wa Serikali wakishindwa kututembelea, hata Kamati ya Bunge ije wajionee.

“Hii itasaidia kutunusuru kwa sababu hali hii ikiendelea, hawa wanyama wataendelea kuteseka na watakufa. Hawa nao ni viumbe hai, hatuwezi kuongeza ila sasa inafikia hatua tunaona tuache ‘nature’ ichukue mkondo wake,” alisema.

Alisema awali biashara yake ilikuwa ni kuuza wanyama nje, lakini aliingia katika uwekezaji wa bustani baada ya kuhamasishwa na Serikali kupitia Idara ya Wanyamapori  baada ya kutungwa sera ya kuhifadhi na kuzalisha wanyama.

Kusaga alisema walikubali kuingia katika uwekezaji huo na hawakuwahi kutarajia kuwa ipo siku mambo yatabadilika wanyama wazaliane washindwe kuwauza.

Alisema ni vyema Serikali ingeangalia uwezekano wa kuwezesha wenye bustani ili wamudu matunzo ya wanyama hao.

Mwekezaji mwingine wa shamba la wanyama lililopo Mlandizi mkoani Pwani, chini ya Kampuni ya Buibui Investment, Kessy Mwaipopo, alisema amepata hasara kwa sababu yeye alifanya uwekezaji mkubwa katika shamba lake.

Alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia kwa undani suala lake kwa sababu lipo mahakamani likisubiri uamuzi.

“Kwa sasa hali yetu ni mbaya. Tulishapewa vibali awali tukalipia na wanyama tukawachukua na kuwahifadhi kwenye mashamba haya.

“Utaratibu ni kuwa wanavyoendelea kuzaana na sisi tunawatafutia soko nje. Lakini sasa hivi wanaendelea kuzaana na hakuna kwa kuwapeleka.

“Hawa wanyama wanaozaliwa kwenye mashamba au bustani kwa utaratibu hawawezi kurudishwa tena porini kwa kuwa wanakuwa wana tabia tofauti na wale wa porini.

“Kwa sehemu kubwa hawa wanahudumiwa karibu kila kitu, kuwarudisha porini ni kuwapa mazingira mapya ambayo hawatayamudu,” alisema Mwaipopo.

Alisema anaumia kuliko wengine kwa kuwa amewekeza kwa kiwango kikubwa kuliko wamiliki wengine wa mashamba ya wanyama, hivyo muda unavyokwenda bila kupata suluhisho, aliamua kukimbilia mahakamani kuomba msaada wa kisheria.

MSIMAMO WA SERIKALI

Akizungumzia malalamiko hayo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi (Utalii na Huduma za Biashara) katika Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Imani Nkuwi, alisema msimamo wa Serikali katika suala la kusafirisha wanyamapori hai nje ulishatolewa kuwa biashara hiyo imesitishwa rasmi.

Alisema kwa waliowahi kuingia katika biashara hiyo na wanaendelea kuendesha mashamba hayo, wanatakiwa kubadilisha mpango biashara wao, kwa kuwa kusafirisha wanyamapori nje si njia pekee ya kutumia mashamba.

“Na kwa kuwa tunaandaa mkakati wa kitaifa, utatoa fursa nyingine kwa wamiliki wa mashamba ya wanyamapori nchini,” alisema.

Alisema mashamba ya wanyamapori yanaanzishwa chini ya utaratibu wa kisheria ambao uko wazi kwa yeyote anayehitaji kuingia katika biashara hiyo, na kwamba hakuna anayezuiwa na Tawa ambayo ndiye msimamizi mkuu hufanya ukaguzi kila robo ya mwaka wa Serikali.

“Mkakati wa Tawa kwa sasa, tangu tulipochukua jukumu hili kutoka Idara ya Wanyamapori ni kwanza, kukamilisha mkakati wa kitaifa wa mashamba na pili, kuhuisha kanuni za mashamba za mwaka 2013,” alisema.

Nkuhi alieleza kuwa kwa wanaotaka kujitoa katika biashara hiyo kwa sasa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla alishasema kuwa Serikali itawarejeshea fedha walizotumia kulipia huduma serikalini kama leseni na nyinginezo.

“Hili jambo la kufunga biashara na mambo ya kuwalipa ni suala la kisera, hivyo waziri ndiye anayeweza kulizungumzia kwa undani zaidi kwa kuwa alishatoa kauli yake wakati wa Bunge la Bajeti mwezi Mei 2019,” alisema.

MAONI YA MTAALAMU

Mkuu wa Idara ya Zoolojia na Uhifadhi wa Wanyamapori katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chacha Werena, alisema amekuwa akifuatilia kwa karibu suala hilo na  wamekuwa wakitumia mashamba hayo kwa mafunzo, lakini hali kwa sasa si nzuri.

Alisema amekuwa akishuhudia mzigo walio nao wamiliki, hasa kutokana na gharama za kuwatunza wanyama hao, ambao wanategemea kuletewa kila kitu walipo, huku wamiliki wakiwa hawana vyanzo vya mapato vinavyotokana na uwepo wa wanyama hao katika mashamba yao.

“Mnyama kama simba, au twiga, au hata fisi, akiwa porini anajitafutia mwenyewe. Kuwahifadhi wanyama wa aina hii na kuwatunza ni gharama, ili uwatunze lazima ufanye biashara, sasa hawa biashara waliyokuwa wakiitegemea haipo tena.

“Serikali iangalie namna ya kuwafidia au basi kuwatafutia vyanzo mbadala vya kuingiza mapato kutokana na wanyama hao.

“Kwa kuwa tatizo la kufunga biashara hiyo ilikuwa ni kukiukwa kwa utaratibu, Serikali ilikuwa haipati mapato, uwekwe utaratibu mzuri, hawa waliosajiliwa kisheria waruhusiwe,” alisema.

MARUFUKU YA SERIKALI

Agosti 2016 Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ilipiga marufuku biashara ya kusafirisha wanyama hai nje ya nchi hadi pale itakapowekwa misingi mizuri ili nchi nayo iweze kunufaika.

Profesa Maghembe alisema Serikali iliamua kuangalia upya utaratibu huo wa kuuza wanyama hai na kusitisha biashara hiyo hadi taratibu na misingi mizuri ya biashara hiyo itakapowekwa.

 “Haiwezekani uuze wanyama hai nje halafu anayenufaika ni yule anayenunua na kuiacha nchi bila faida yoyote ya uwepo wa maliasili hiyo.

“Kama nchi, tumeamua kupiga marufuku biashara hiyo hadi pale misingi mizuri ya kibiashara itakapowekwa na kuiwezesha Tanzania kunufaika na rasilimali zake,” alisema Profesa Maghembe.

KAMPENI DHIDI YA SERIKALI

Katika taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii, Shirika la kutetea haki za wanyama la Ban Animal Trading South Africa, linaendesha kampeni ikieleza hali mbaya inayowakabili wanyama kwenye shamba la Bahari Zoo.

Kampeni hiyo iliyoanza Julai Mosi, mwaka huu,  inasema wanyama hao wanafanyiwa ukatili usioelezeka.

 “Wanyama hawa wanakufa taratibu, tena kifo chenye maumivu makali. Tupaze sauti zetu na kuwaokoa wanyamapori na kuiamuru Serikali ya Tanzania kuwanusuru wanyamapori hawa ambao wanateswa na kupuuzwa, kwa kuanzia na Bahari Zoo ambayo inahitaji kufungwa na wamiliki wapelekwe kwenye mkono wa sheria,” inasema sehemu ya kampeni hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles