24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Polepole : Sijaona wala kusikia malalamiko ya akina Kinana

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole  amesema hajaiona nakala ya barua ya malalamiko ya kudhalilishwa iliyowasilishwa  na makatibu wakuu wawili wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.

Zaidi Polepole aliliambia MTANZANIA Jumapili kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia mtandao wa WhatsApp kuwa hajasikia malalamiko hayo kwa kuwa kwa sasa yupo kwenye ziara vijijini.

Wakati Polepole akisema hajasikia malalamiko hayo ambayo si tu yameandikwa na vyombo vya habari, waraka wake pia umesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwamo WhatsApp na hivyo kuzua mjadala mkubwa  kabla na baada ya  baadhi ya wabunge wa chama hicho kuendelea kujitokeza kila siku kuwajibu wastaafu hao.

Polepole ambaye alitafutwa na gazeti hili kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa CCM kuhusu barua hizo na hatua ambazo itachukua dhidi ya malalamiko ya viongozi hao wastaafu wa chama hicho, alisisitiza kuwa atakapoiona atatujuza.

Jumapili iliyopita Makamba na Kinana walimwandikia barua Katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa CCM, Pius Msekwa wakilalamika kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi na uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa serikali na kushangaa chama hicho kukaa kimya.

Kabla Msekwa hajajibu barua yao hiyo ya malalamiko akizungumza na gazeti dada la hili la MTANZANIA Jumatatu wiki hii alisema wanasubiri vikao rasmi vya chama hicho tawala kuamua juu ya yale yaliyolalamikiwa na wastaafu hao kwa kuwa wao kama baraza la Wazee wastaafu wajibu wao kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ni kutoa ushauri tu iwapo wataombwa kufanya hivyo.

Alisema tayari barua ya malalamiko ya wastaafu hao nakala yake pia ilifikishwa  kwa Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais Dk. John Magufuli na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally.

Msekwa ambaye alisema barua hiyo ambayo ni ya kwanza kuwafikia wao kama baraza la wazee wastaafu, kwa kawaida itapelekwa kwenye chama hicho ambacho ndicho kinachopaswa kuitisha vikao vyake kwa ajili ya kushughulikia malalamiko yaliyotajwa.

Mara kadhaa sasa gazeti hili limemtafuta bila mafanikio kupitia simu ya mkononi, Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru.

Makamba na Kinana waliopata kushika nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM kwa kufuatana wakati wa serikali ya awamu ya nne, walitoa taarifa ya maandishi kwa umma Jumapili iliyopita wakiweka bayana kwamba wamezingatia katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122.

“Tumewasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kushughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.

“Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo,”walisema katika barua hiyo.

Vilevile walisema wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu taarifa wanazodai za uzushi kwa nyakati mbili tofauti.

Walisema mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo, ambaye amemtaja lakini jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, anatumwa na nani?

“Pili anakingiwa kifua na nani? Tatu anatumika kwa malengo gani? Na nne nini hatima ya mikakati yote hii.

“Tafakari yetu inatupeleka kupata majibu yafuatayo;kwanza kwa ushahidi wa kimazingira mtu huyu anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.

“Pili zipo ishara kwamba watu hawa wanaomkingia kifua wana mamlaka, baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu kwa watu maalumu na kwa malengo maovu,”walisema katika barua hiyo.

Katika hoja yao ya tatu walisema mtu huyo anatumika kwa malengo ya kuwazushia, kuwakejeli, kuwavunjia heshima, kuwatia hofu na kuwanyamazisha viongozi, taasisi na watu ambao ni walengwa waliokusudiwa.

“Nne, kuna kila dalili kuwa lengo na hatima ya mkakati huu ni kuandaa tufani ya kuwahusisha walengwa, wastaafu na walio kazini katika nafasi mbalimbali na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini ili kuhalalisha hayo wanayokusudia kuyafanya.

Katikati ya wiki hii  Msekwa aliwajibu akisema yeye kama Katibu hana mamlaka ya kutoa uamuzi wowote na kuahidi kuwasilisha barua hiyo kwa wajumbe wa baraza, ili kupata maelekezo yao juu ya nini kifanyike.

Pia alisema wakati anasubiri majibu kutoka kwa wajumbe hao aliwapongeza akina Kinana  kujibu tuhuma wanazotuhumiwa kwa kuwa ni jukumu la mtu yeyote aliyetuhumiwa kusafisha jina lake jambo ambalo alisema wamekwishalitekeleza kwa kuandika barua hiyo.

Zaidi aliwaonya kutotumia njia za mkato kushughulikia jambo hilo na hivyo kuvunja Katiba ya CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles