28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wanunuzi korosho sasa wapewa amri

Na Waandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho kupeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionyesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua.

Agizo hilo lilitolewa jijini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipotoa tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa korosho.

“Wanunuzi waliojiandikisha wakiwamo na wale wote ambao wamekuwa wananunua katika minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo (jana) Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi kwa saa 24,” alisema.

Majaliwa alisema baada ya kupita siku hizo Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali inayoonekana sasa ni kama wanawakomoa wakulima na hawatakubali hali hiyo.

“Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua kwa sababu ofisi yangu ipo wazi saa 24, wana nafasi ya kuleta barua wakati wowote wakionesha nia yao na kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo Serikali haitaruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena,” alisema.

Pia alisema katika msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu, walishuhudia kusuasua kwa minada na Serikali ilikutana na wanunuzi wa korosho katika kikao kilichoongozwa na Rais Dk. John Magufuli na walikubaliana kununua kwa bei inayoanzia Sh 3,000 na kuendelea.

“Mjadala ulikuwa wa wazi na wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo ilikuwa inaanzia shilingi 3,000, hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi katika minada imeendelea kusuasua na hata tani zilizokuwa zikinunuliwa zilikuwa kidogo. Sisi tunaiona hali hii kama mgomo baridi ambao si sawa kwa sababu malengo yetu sisi na sekta binafsi ni kumfanya mkulima apate bei nzuri.

“Hali hii haifurahishi kwa sababu Serikali imedhamiria kuboresha mazao yanayolimwa na wakulima kwa kuwasaidia kuanzia katika hatua za utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na masoko ili waweze kunufaika na kilimo na kupata tija katika mazao hayo,” alisema.

Majaliwa alisema baada ya kugundua bei imekuwa tatizo, Serikali ilifanya jitihada za kupeleka wataalamu wake katika masoko makuu duniani na kupata bei halisi ambayo bado inatosha kumlipa mkulima Sh 3,000.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya korosho kununuliwa kwa bei ya chini na idadi ya wanunuzi kuwa ya chini licha ya uzalishaji wa mwaka huu kuwa mdogo ukilinganisha na msimu wa mwaka jana.

Alisema msimu wa mwaka jana uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 300,000 na mwaka huu zinatarajiwa tani zaidi ya 200,000 na wafanyabiashara wanao uwezo kununua korosho zilizopo.

Pia aliwataka wakulima wa korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo.

SERUKAMBA ATAKA

SOKO LIAMUE BEI

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Peter Serukamba, ameitaka Serikali kuacha nguvu ya soko kuamua bei za mazao badala ya kuweka masharti mbalimbali.

Serukamba alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2019/2020.

Alitolea mfano sakata la korosho akisema kama mtu anamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari 10 hawezi kusubiri Serikali imtafutie soko bali atatafuta mwenyewe.

“Hatawaomba pembejeo kwa hiyo nasema tufike sehemu haya mawazo kwamba kila mtu anaweza kulima hayawezekani. Serikali iache demand and supply ifanye kazi.

“Serikali kuingia ku-detect terms sio sawa, ndiyo matokeo yake wataingia watu katikati watatuvuruga. Bei za mazao kuanguka imekuwepo hivyo duniani kote inategemea soko la dunia lakini kwanini tuongelee zao moja? Watu wa mahindi, mtama hali ni mbaya,” alisema Serukamba.

Aliitaka Serikali kuacha nguvu ya soko ndiyo iamue bei na kwamba mwaka mmoja bei ya mazao ikiwa mbaya basi mwakani Serikali itafute motisha ili kuwainua wakulima.

Alisema haiwezekani kuhangaikia kuanguka kwa soko la bidhaa moja na kuhoji hata kama Serikali ikiamua kununua yenyewe fedha za kufanya hivyo wanatoa wapi.

“Kwa hiyo ningeiomba Serikali tuache marketing forcing zi-determine (ziendeshe) biashara. Tuko katika soko huria kurudi kwenye commanding soko maana yake lazima tulete tume ya bei. Tukileta tume ya bei inabidi turudi kule kule,” alisema.

Serukamba alisema kama taifa suala la  kilimo cha biashara limekuwa haliongelewi na bila aina hiyo ya kilimo matatizo yanayotokana na shughuli hiyo hayatakwisha.

“Matatizo yote ya kilimo yatatatuliwa na mashamba makubwa, sisemi tunyang’anye mashamba Mungu katupa ardhi na watu wenye uwezo mkubwa watakuja,” alisema.

 

MGOMO WA WAKULIMA

Oktoba 22, mwaka huu wakulima mkoani Mtwara waligomea mnada wa korosho na kisha mingine miwili ikafuata kabla ya Majaliwa kufanya kikao na wakuu wa mikoa inayolima korosho kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Pia minada mitatu ya korosho ya Tandahimba, Newala, Masasi, Ruangwa, Nachingwea na Liwale ilikwama baada ya wakulima ambao mwaka jana walijivunia mamilioni ya shilingi kutokana na bei iliyofikia zaidi ya Sh 3,000 kwa kilo, kukataa bei mpya ya chini ambayo ni kati ya Sh 1,700 na Sh 2,700 kwa kilo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles