32.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 13, 2024

Contact us: [email protected]

Wanufaika wa TASAF Kibaha waishukuru Serikali

Na Gustafu Haule, Pwani

WANUFAIKA wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) waliopo katika Mtaa wa Miwaleni Kata ya Visiga katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha wameishukuru Serikali kwa kitendo cha kuendelea kutoa fedha  zinazosaidia kubadilisha maisha yao.

Wamesema kuwa mfuko wa Tasaf umekuwa na msaada mkubwa kwao na kwamba bila Rais Samia kuendelea kutoa fedha katika mfuko huo ni wazi kuwa wangekuwa katika hali ngumu ya maisha.

Wametoa kauli hiyo Julai 10, mbele ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete aliyefanya ziara kwa ajili ya kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Tasaf awamu ya tatu.

Mmoja wa wanufaika hao akiwemo, Ester Bilinge, amesema kuwa kabla ya kufikiwa na Tasaf alikuwa anaishi maisha magumu kiasi cha kukosa chakula, watoto kushindwa kuwapeleka shule na hata kukosa mavazi.

Bilinge amesema baada ya kuingia katika mpango wa Tasaf maisha yake yamebadilika kwani kwasasa watoto wake wanakwenda shule, wanakula milo mitatu kwa siku na tayari ameweza kupata shamba la kukodi ambalo linamwingizia kipato kwa kulima mbogamboga.

“Mimi namshukuru Rais Dk. Samia kwa kuendeleza Tasaf hapa nchini maana umekuwa mpango wenye kuleta manufaa kwangu, nilikuwa naishi katika kibanda kibovu mvua ikinyesha maji yanaingia mdani wote tunaloa lakini kwasasa nimejenga kibanda changu cha matofali na maisha mazuri,” amesema Bilinge.

Nae Mariam Pazi, amesema awali alikuwa anashindwa kuvaa nguo nzuri lakini kwasasa wanaishi vizuri kama watu wengine huku akimuomba Rais azidi kuwasaidia zaidi katika kuimarisha mfuko wa Tasaf.

“Kitendo cha Rais Dk. Samia kuendelea kutusaidia sisi kaya maskini kupitia Tasaf kinaleta tumaini kubwa kwetu wananchi na hakika Mama Samia tunamshukuru na tunamuombea sana ili aweze kutimiza malengo yake ya kuisaidia nchi yetu,”amesema Pazi.

Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Miwaleni, Asnath Chipata, amesema Tasaf imeleta mafanikio makubwa katika Mtaa wake kwani familia nyingine zimekua kiuchumi kupitia fedha wanazopata kutoka katika mfuko huo.

Chipata amesema baada ya utekelezaji wa Mpango wa Tasaf kuanza mtaani hapo wameanzisha mradi wa kuweka akiba na kukuza uchumi wa kaya kwa kaya 32 zilizopo za eneo hilo.

Amesema kuwa,tangu kuanza kwa mpango huo Mtaa wa Miwaleni umehawilisha kiasi cha Sh milioni 68.432 ambapo kupitia fedha hizo waliunda vikundi viwili vikiwemo Tumuamini Mungu na Tujiamini na kuweza kukopeshana.

Akizungumza katika mkutano huo Kikwete, amepongeza namna ambavyo kaya za Mtaa huo zilivyotumia vizuri mpango huo kwani vipo vikundi vinapewa pesa nyingi lakini vinashindwa kujiendeleza na hivyo mitaji yao kufa.

Kikwete ametoa maagizo hayo kwa watendaji wanaoshughulika na kaya maskini kuwa wafanye mpango wa kuwafuata watu wote wa vigezo wa kuingia katika mfuko huo ili wawasajili kwani mpango wa rais ni kutaka kuona watu wote wenye sifa wanafikiwa na mpango huo.

Hata hivyo, Kikwete amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mshamu Munde, kuhakikisha kaya hizo zinapata fursa ya kupata mkopo kutoka halmashauri kwakuwa vikundi hivyo vinakopesheka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles