28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

WANNE WAFARIKI WAKICHIMBA DHAHABU CHUNYA

Na ELIUD NGONDO, MBEYA


WATU wanne, wamefariki dunia na wengine wamejeruhiwa baada ya kufukiwa kwenye shimo walipokuwa wakichimba dhahabu.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, aliwaambia waandishi wa habari jana, kwamba tukio lilitokea eneo la Nanyuki, Kijiji cha Itumbi, Kata ya Matundasi, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya.

Katika maelezo yake, Kamanda Kidavashari, alisema tukio hilo lilitokea jana asubuhi na kwamba wakati wa tukio hilo, kulikuwa na wananchi zaidi ya 50 waliokuwa wamevamia shimo hilo la dhahabu linalomilikiwa na Vincent Minja, mkazi wa Dar es Salaam.

“Inasemekana watu walikuwa wamejazana  kwenye shimo hilo baada ya kupata taarifa kuwa linatoa dhahabu nyingi.

“Kwa hiyo, walikuwa wanachimba bila tahadhari na kusababisha shimo kuporomoka na kuwafukia watu 11,” alisema Kamanda Kidavashari.

“Lakini, watu wale tunawachukulia kama wezi kwa sababu walivamia eneo lenye leseni ya mtu mwingine,” alisema.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Andrew Paulo (26), Mark Fredrick (22) na Isack Mwanjale (30) wote wakazi wa Kijiji cha Itumbi na Hamis Mailosi (25) mkazi wa Kijiji cha Mapogoro.

Kwa upande wa waliojeruhiwa, aliwataja kuwa ni Saimon Majaliwa (25), mkazi wa Itumbi, Mazoea Mahona (25), mkazi wa Mkoa wa Tabora, Ben Bahati (23), mkazi wa Kijiji cha Mapogoro na James Alinanuswe (26), mkazi wa Tukuyu, wilayani Rungwe.

Diwani wa Kata ya Matundasi, Kimo Choga, alisema wananchi hao walianza kuvamia eneo hilo Jumatatu wiki iliyopita na kwamba walizuiliwa na mwenye leseni ya eneo hilo lakini hawakumwelewa.

“Ilipofika Alhamisi, wananchi hao walielimishwa vizuri na kukubali kusimamisha kazi ya kuchimba madini hayo baada ya mwenye eneo kuwaeleza kuwa kufikia Jumatatu (jana), atakuwa ameweka utaratibu mzuri wa namna ya kuchimba.

“Lakini, jana asubuhi walivamia tena shimo moja wakidai mmiliki wa leseni ya eneo hilo alikuwa akiendelea kuchimba, hivyo nao wakasema lazima wachimbe,” alisema Diwani Choga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles