26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake watakiwa kumuunga mkono Rais Samia

Na Allan Vicent, Tabora

Wanawake hapa nchini wametakiwa kumuunga mkono na kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kuliongoza taifa kwa mafanikio makubwa.

Ushauri huo umetolewa juzi na baadhi ya wanawake makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tabora walipokuwa wakitoa salamu za rambi rambi kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Dk. John Magufuli.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu ya CCM mkoani hapa, Maimuna Abas alisema kuwa Mama Samia Suluhu anatosha kuwa Rais wa Tanzania kwa sababu ni mwanamke jasiri, mwenye uwezo na kipaji kikubwa cha uongozi.

Alisema katika nafasi zote alizowahi kushika serikalini ikiwemo kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba na Makamu wa Rais alionesha uwezo mkubwa.

“Rais Samia anatosha, tuna imani kwake, hatetereki, naomba wanawake wote tumuunge mkono na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa viwango kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake’, alisema.

Maimuna alisisitiza kuwa, kuwa Mwanamke sio kushindwa kufanya kazi, bali kujiamini na kumtanguliza Mungu mbele ili aendelee kukuongoza katika kila jambo, hata kama hukutegemea kuwa katika nafasi hiyo Mungu alishakupangia.

Upande wake Mwalimu mstaafu, Jane Kabeho ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM kata ya Gongoni alisema hayati Dk. Magufuli ameondoka wakati taifa bado linamhitaji, ila hawana la kufanya.

Alisema kuwa Dk. Magufuli amemaliza kazi aliyotumwa na Mungu kwa Watanzania hivyo kuapishwa kwa Mama Samia kuwa Rais wa 6 wa Tanzania ni mapenzi ya Mungu, hivyo akaomba akinamama wote kumuunga mkono.

Alibainisha kuwa Watanzania wote wako nyuma yake na wana imani kubwa kwake kutokana na uwezo mkubwa alionao na ujasiri wake hivyo akashauri kuwa lolote jema atakalowafanyia wananchi aamini kuwa yuko sahihi.

Katibu wa Jumuia ya Wazazi Mkoa wa Tabora, Rehema Mohamed alisema kuwa kifo cha Dk. Magufuli kimeacha simanzi kubwa miongoni mwa wana-CCM na jamii kwa ujumla kutokana na maono makubwa ya kimaendeleo aliyokuwa nayo.

Alifafanua kuwa kazi ya Mungu haina makosa hivyo kuondoka kwa Magufuli na kuapishwa kwa Rais Samia Suluhu, Mungu ana makusudi yake kwa Watanzania, tutamwombea ili Mungu amwongoze kama alivyomwogoza hayati Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles