Na Amina Omari,aliyekuwa MOROGORO
TANZANIA ni miongoni mwa nchi yenye hazina ya madini mbalimbali yakiwemo madini adimu kama ya vito na metali ambapo mchango wa sekta ya madini ni muhimu katika ukuaji wa uchumi.
Sekta hiyo ni moja wapo ya fursa zinazosaidia kutengeneza ajira zilizorasmi na zisizo rasmi na kwa kuwawezesha wananchi kupata kipato cha uhakika na
pamoja na serikali kwa ujumla.
Hata hivyo mikakati ya serikali ni kuhakikisha kwamba rasilimali hiyoya madini inalinufaisha Taifa na watu wake kwa kuweka mipango madhubuti na endelevu ambayo itawezesha kufikia lengo hilo.
Moja ya hatua ambayo serikali ya awamu ya tano imeweza kuchukua ili kudhibiti ulanguzi wake ni pamoja na kutoruhusu malighafi za madini hayo kusafirishwa nje ya nchi bila kuongezwa thamani.
hatua hizo ikiwemo kuweka na kusimamia mfumo thabiti wa kukagua shughuli za migodi, kukusanya takwimu za madini na kufuatilia maduhuli yake yatokanayo , na madini kwa malengo mapana ya kuongeza mapato ya Serikali.
Wakati serikali ikiweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wa madini kuweza kunufaika na raslimali hiyo nao wadau mbalimbali wameanza kuunga mkono juhudi hizo za serikali.
Ambapo kwa hivi karibuni taasisi ya Best Dialogs ya nchini Marekani waliweza kuendesha utafiti kuhusu changamoto zilizoko kwenye sekta ya madini nchini ili kusaidia juhudi za serikali katika kufufua uchumi wa
sekta hiyo.
Hata hivyo utafiti huo ulilenga katika kuibua changamoto zilizoko katika sekta hiyo hususani kwa upande wa wanawake ambao katika shughuli za umiliki wa migodini na uchimbaji ni wachache .
Ambapo baadhi ya changamoto zilizoweza kubainika ni kutoeleweka kwa sera ya madini kwa wachimbaji wenyewe na baadhi ya watendaji wa serikali, mitaji midogo , ushiriki mdogo wa wanawake katika shughuli za
uchimbaji na umiliki wa migodi.
Yunus Negele ni Mwenyekiti wa chama cha Wachimbaji wanawake nchini TAWOMA ambapo anasema kuwa kupitia utafiti huo waliweza kubaini kuwa ukosefu wa mitaji umesababisha wanawake wengi kutoweza kushiriki katika shughuli za uchimbaji na umiliki.
Anasema kuwa kutokana na ugumu wa sekta hiyo umesababisha wanawake kutoweza kushiriki katika shughuli hiyo ya kiuchumi hivyo kukosa nafasi ya kuweza kujiongezea kipato chao.
“Unajua shughuli za uchimbaji zinahitaji mitaji hivyo kupitia utafiti huo tumeweza kupata mwanga kuwa kumbe nasi tunanafasi ya kushiriki ipo kama tutaweza kujiunga katika vikundi na kupata mitaji ambayo
itasaidia kuendesha shughuli hizo,”amesema Negele.
Pia Amesema kuwa utafiti huo umeweza kubaini kuwa uchimbaji wa kuhamahama nao ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wengi kwa sasa hivyo kujikosesha fursa ya mapato.
Anasema kuwa kwa wachimbaji wadogo wamekuwa wanaendesha shughuli za uchimbaji kiholela kutokana na kutokuwa na vifaa vya kubaini eneo lenye madini hivyo kuishia kuendelea na uchimbaji wa kuhamahama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Aidha Negele amesema kuwa kwa kiasi kikubwa wachimbaji wadogo wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu madini wala maeneo ambayo yanamadini hivyo kuishia kuendesha shughuli za uchimbaji kwa kubahatisha na kwa mazoweya.
“Kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu madini pamoja na maeneo yenye madini ni changamoto inayowakabili wachimbaji hususani wadogo huku wakitumia zana duni ambazo huishia kupata mavuno machache,”amesema
Mwenyekiti huyo.
Jambo hilo linaungwa mkono na Lucas Chuwa ambaye anasema kuwa wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa wakichimba madini ambayo kwa asilimia kubwa hata hawajui thamani yake.
Anasema kuwa hawana uelewa wa aina ipi ya madini inayohitajika sana katika soko hivyo wakati mwingine huishia kupata hasara huku wakiwa wametumia nguvu kubwa katika uchimbaji.
“Unakuta kama madini ya vito ambayo si rahisi kupatikana lakini hujui kito aina ipi ndio inahitajika sana sokoni hivyo unaishia kuchimba mali ambayo sio yenyewe na ukiipeleka sokoni uuzaji wake aidha unakuwa mgumu au unauza kwa bei ya hasara,” amebainisha Chuwa
Aidha ameongeza kuwa wachimbaji wengi wadogo hawana ufahamu wa kutosha kuhusu aina ya madini wanayoyachimba hivyo kutofikia malengo yao.
“Serikali ingeangalia uwezekano wa kuwafanya wamiliki wa ubia na wawekezaji wachimbaji ambao wanagundua maeneo ya madini kabla ya kupima maeneo na kuwamilikisha wawekezaji ,”amesema Chuwa.
Anasema kuwa hatua hiyo itawezesha wachimbaji wadogo kukua kishughuli na kiutendaji badala ya kuchimba kwa kutumia zana duni sasa wataweza
kutumia zana bora na za kisasa.
Hata hivyo Mchimbaji Said Bomani amesema kuwa kutokueleweka kwa sera za madini kwani imeandikwa kwa lugha ya kingereza hivyo kusababisha wadau wengi kutoweza kuelewa kilichomo ndani ya sera hiyo.
“Ingependeza sera hiyo iweze kufikia hadi katika ngazi za mikoa na wilaya ili watendaji wa serikali waweze kuielewa kwani wamekuwa wanatoa maagizo ambayo wakati mwingine yanapingana na sera hiyo,”amesema Bomani.
Aidha ameishauri serikali kuona namna bora ya kuyagawa maeneo yenye madini ambayo wawekezaji wameshindwa kuyafanyia kazi na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuyaendeleza.
Nae Negele ameipongeza Serikali kwa kuendesha zoezi la urasimishaji wa leseni za uchimbaji wa madini ili kuweza kutambua idadi kamili ya wachimbaji nchini kwa ajili ya malengo ya uchumi endelevu.
Amesema kuwa kukamilika kwa zoezi hilo kutasaidia kujua idadi kamili ya leseni,na serikali itaweza kujua makusanyo halisi ya mapato yatokana na na leseni za uchimbaji huku kwa upande wa uchimbaji kutaweza kuibua fursa ya ajira rasmi.
Kwani zoezi hilo litaweza kusaidia kuepuka uchimbaji wa kuhamahama unaoendelea kufanywa na wachimbaji hususani wadogo kwa ajili ya kutafuta madini .
Huku akiiomba serikali kuwasaidia wachimbaji wadogo fedha za mikopo kwa ajili ya kukuza shughuli zao ili waweze kufanya uchimbaji vizuri kwa kutumia vifaa vya kisasa.
“Mchakato wa uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata madini utasaidia kuvutia wachimbaji wengi hivyo ni wakati mwafaka kwa serikali kuweka mazingira bora ya sekta hiyo iweze kunufaisha wananchi wake kiuchumi,”amesisitiza Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Katibu wa TAWOMA Salma Kundi amesema kuwa ukosefu wa taarifa sahihi za kijiolojia umesababisha wachimbaji wengi wadogo kukata tamaa ya kuendelea na shughuli za uchimbaji.
Anasema kuwa ukiangalia idadi ya leseni za uchimbaji imeweza kushuka kwani mwaka 2016 kulikuwa na maombi 9827 ukilinganisha na mwaka 2017
maombi 5171 pekee.